Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-01 16:48:43    
Mchoraji Chen Zhizhuang

cri

Marehemu Chen Zhizhuang ni mchoraji aliyejulikana baada ya kufariki dunia. Alizaliwa mwaka 1913 na kufariki dunia mwaka 1976 katika wilaya ya Rongchang mkoani Sichuan. Wakati alipokuwa hai, alikuwa anaitunza familia yake yenye watu 7 kwa mashahara wake mdogo aliokuwa akilipwa kutoka kwenye jumba la utamaduni na historia la Sichuan. Maisha yake yalikuwa ya kimasikini, na mke wake alikuwa na matatizo ya akili. Katika hali hiyo ya umasikini, Chen alishikilia kuchora picha.

Marehemu Chen alipenda kujifunza kutoka kwa wachoraji maarufu waliomtangulia. Kwenye michoro yake tunaweza kugundua taathira ya wachoraji maarufu wa kale na wa sasa kama vile badashanren, Shi Tao, Hung Binghong, Qi Baishi na Feng Zikai. Lakini mzizi wake wa sanaa ulijikita kwenye maisha ya kawaida. Mandhari za kawaida na za kuvutia za kila mahali alipofika, zote ziliweza kuwa mada za picha alizochora.

Marehemu Chen alikuwa amezoea kuchora picha kwenye karatasi ndogo, baadhi ya karatasi alizotumia kuchorea zilikuwa na ukubwa wa kitabu. Michoro yake ilikuwa ni ya miti iliyosambaa katika vichaka vya mianzi, maboma rahisi na nyumba za manyasi zilizoonekana kama kwamba zinataka kuanguka zikiwa kati kati ya misonobari michache minene. Ingawa michoro ya Chen ilikuwa rahisi, lakini ilikuwa inawapa watu mawazo mengi. Kati ya wachoraji wa zama hii tuliyo nayo, Chen ni mchoraji mwenye mtindo wa kipekee wa uchoraji. Kwenye michoro yake rahisi, marehemu Chen alionyesha matumaini na mahitaji yake katika maisha, hii ndiyo siri iliyoifanya michoro yake iwapendeze watu.

Mwezi Machi mwaka 1988, kulifanywa maonyesho ya michoro ya Chen Zhizhuang kwenye jumba la sanaa la China mjini Beijing. Kwenye maonyesho hayo kulionyeshwa michoro 300 ya mandhari za milima na mito, maua na ndege. Siku ya kwanza baada ya maonyesho hayo kufunguliwa, watu 12,000 waliyatembelea maonyesho hayo. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa maonyesho ya michoro ya mchoraji aliyefari ambaye alikuwa hajulikani, kufanyika kwenye jumba la sanaa nchini China.

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-28