Duru la 4 la mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea yanayofanyika hapa Beijing tarehe 28 yaliingia katika siku yake ya 3, ambapo pande mbili za Korea ya kaskazini na Marekani zilifanya majadiliano, mazungumzo ya siku hiyo yaliendelea katika hali ya utulivu sana, wachambuzi wanaona kuwa hali hiyo ya utulivu inaonesha matumaini.
Pande mbili Korea ya kaskazini na Marekani ziliendelea kuonesha udhati wa kutatua masuala, siku hiyo asubuhi, pande hizo mbili zilifanya majadiliano ya mara tatu tangu zifike Beijing. Habari zilizodokezwa zinasema kuwa, pande hizo mbili ziliheshimiana, majadiliano kati yao ni ya kiujenzi kwa kufuata hali halisi. Msemaji wa ujumbe wa China katika mazungumzo hayo Bwana Qin Gang aliainisha kuwa, pande mbili Korea ya kaskazini na Marekani zinaweza kukaa pamoja na kuwa na mazungumzo, hii ni dalili moja nzuri.
Aidha, Korea ya kaskazini na Marekani zote zimeonesha matumaini mema ya kuyawezesha mazungumzo ya pande 6 yapate maendeleo. Bwana Qin Gang alidokeza kuwa, ili kuziwezesha pande mbalimbali zifanye majadiliano ipasavyo na kwa kina, na ili kupunguza migongano na kusukuma maendeleo ya mazungumzo, mpaka sasa pande mbalimbali zinazoshiriki kwenye mazungumzo hayo bado hazijathibitisha tarehe ya kumalizika kwa mazungumzo ya pande 6. Hivi sasa pande mbalimbali zinafanya mkutano wa wajumbe wote au kufanya majadiliano ya pande mbili mbili ili kuelewana na kuafikiana, na kila upande unaeleza msimamo, mawazo, mpango na pendekezo lake juu ya utatuzi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea.
Siku hiyo adhuhuri, naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Dai Bingguo aliwaandalia tafrija viongozi wa ujumbe wa nchi mbalimbali. Pande zote zimekubaliana kuwa lazima kuyawezesha mazungumzo hayo yapate matokeo halisi pamoja na kutoa waraka wa pamoja.
China ikiwa nchi mwenyeji na mshiriki wa mazungumzo ya pande 6, inaendelea na juhudi za kiujenzi za kufanya usuluhishi na kuhimiza amani. Mpaka sasa China imefanya majadiliano mara 12 ya pande mbili mbili na nchi zinazohusika, imefanya juhudi zisizolegea katika kusukuma mbele maendeleo ya mazungumzo hayo. Hata tafrija iliyoandaliwa na naibu waziri wa mambo ya nje Bwana Dai Bingguo ndiyo fursa iliyotolewa kwa viongozi wa ujumbe mbalimbali kuongea katika hali ya furaha na ya kawaida baada ya kufanya mazungumzo rasmi ya siku kadhaa. Kwenye tafrija hiyo Bwana Dai Bingguo alisema kuwa, mazungumzo ya pande 6 yanasonga mbele kwa mwelekeo sahihi. Pia alisema kuwa, kutokana na utatanishi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea, kuwepo kwa tofauti na migongano ni hali ya kawaida. Anatumai kuwa pande mbalimbali zinazohusika zithamini fursa ya kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya pande 6 na mwanzo wake mzuri wa hivi sasa, kufanya juhudi za kupanua maoni ya pamoja, kupunguza migongano, na kusukuma mbele kwa pamoja maendeleo ya mazungumzo hayo.
Wachambuzi wameainisha kuwa, ingawa Korea ya kaskazini na Marekani zimefanya mawasiliano mara kwa mara, tena pande hizo mbili zote zimeonesha udhati wa kuyawezesha mazungumzo yapate maendeleo, lakini kutokana na kukosa uaminifu kati ya pande hizo mbili, mpaka sasa bado hazijaweza kupata mpango wa pamoja wa utatuzi wa suala unaoweza kukubalika kwa pande zote mbili kuhusu "maana ya sehemu isiyo na nyuklia" na "mchakato wa kuifanya peninsula ya Korea kuwa sehemu isiyo na nyuklia". Kama mazungumzo ya duru hilo yatapata maendeleo au la, bado inategemea hali ya mazungumzo ya tarehe 29.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-28
|