Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-01 15:15:47    
Mwandishi wa Habari Mwanamke Fan Chunge

cri

Siku chache zilizopita, maonesho ya picha zilizopigwa na mwandishi wa habari mwanamke Fan Chunge yalifanyika katika Jumba la Makumbusho la Taifa mjini Beijing. Maonesho hayo yameonesha jinsi msafiri mkubwa wa bahari Zheng He alivyokuwa katika safari zake saba katika miaka 600 iliyopita.

Katika ukumbi mkubwa wa jumba la makumbusho kuna picha nyingi zilizotundikwa ukutani?picha ya hekalu la Zheng He na sanamu yake ndani ya hekalu hilo nchini Indonesia, picha ya mandhari ya machweo ya kisiwa cha Kish nchini Iran, picha iliyopigwa katika kisiwa cha Cochin nchini India ambayo inaonesha wavuvi wakivua samaki kwa "wavu wa Kichina". Mwandishi Fan Chunge alisema, picha zote ni alama za utamaduni katika sehemu alizopitia Zheng He.

Mwandishi Fan Chunge ana umri wa miaka 46, alianza kushika kazi ya uandishi wa habari baada ya kuhitimu chuo kikuu, na sasa amefanya kazi kwa miaka 21. Mwandisi huyo anapenda sana kazi yake, aliwahi kusafiri hadi magharibi mwa China kwa baiskeli, na kufika kwenye mlima wenye theluji katika mkoa wa Tibet wenye mwinuko wa mita 4000 juu ya usawa wa bahari kwa lori. Lakini safari inayompa sana kumbukumbu ilikuwa ni kufuatana na kundi la uchunguzi kwenda kwenye ncha ya kusini ya dunia. Bi. Fan Chunge alisema,

"Safari ya kwenda nchi ya kusini ya dunia haisahauliki, na kweli imenisaidia sana kwenye safari yangu ya kufuata nyayo za Zheng He. Meli niliyosafiria ilipopita mlango wa bahari wa Drake mawimbi yalikuwa makubwa na hata kufikia mita 20, hali ilikuwa hatari sana. Safari hiyo ya kwenda ncha ya kusini ya dunia ilinisaidia sana kuelewa jinsi safari ya Zheng He ilivyokuwa hatari, nikawa na heshima kubwa kwa Zheng He na wafuasi wake."

Bi. Fan Chunge ni mwandishi wa habari wa gazeti la jioni la Wuhan. Mji wa Wuhan uko katika sehemu ya katikati ya China, ni kituo cha usafirishaji mizigo katika sehemu ya katikati ya Mto Changjiang. Bi. Fan Chunge alikuwa na hamu ya kuandika habari kuhusu usafiri wa bahari toka zamani. Kwa bahati alisoma habari kuhusu wasafiri wakubwa duniani katika gazeti la "Jiografia" la Marekani, habari hiyo ilimpa wazo la kuandika habari kuhusu safari ya Zheng He. Bi. Fan Chunge alisema,

"Safari ya Zheng He kilikuwa ni kitendo kikubwa kwaa usafiri wa bahari katika historia ya China, ni kitendo ambacho kilikuwa ki kikubwa kabisa na cha mapema kuliko safari zote za wasafiri wa Magharibi. Lakini safari yake haikuacha alama nyingi, na watu wa sasa hawajafahamu sana kama wanavyostahili kuifahamu safari ya Zheng He. Kutokana na hayo viongozi wangu waliamua kufuatilia nyayo zake ili kuwafahamisha wenzetu ustaarabu mkubwa wa usafiri wa bahari katika historia ya China."

katika mwaka 2000 Bi. Fan Chuge alianza safari yake ngumu. Katika muda wa miaka miwili alivuka bahari ya Hindi, alifika kwenye nchi 18 za Asia na Afrika. Popote alipofika aliuliza uliza habari kuhusu Zheng He. Nchini Combodia, aligundua mahekalu sawa na yaliyoelezwa na Zheng He na wafuasi wake. Nchini Indonesia aliona nanga iliyoachwa na Zheng He iliyosimuliwa katika hadithi za mapokeo, na nchini Sri Lanka aliona jiwe lenye maandishi aliloacha Zheng He. Katika safari yake aliandika andika na kupiga piga picha, alipeleka habari za maandishi yenye maneno laki mbili na picha elfu kumi kwa gazeti lake.

Kutokana na kuwa maisha yake hayakuwa ya kawaida na ya kuhamahama kutoka nchi hadi nchi, Bi. Fan Chunge aliugua katika hosteli. Tukio la "11 Septemba" nchini Marekani lilisababisha mtafaruku mkubwa duniani, na pia lilimletea shida nyingi za kazi, lakini hakuacha kazi yake, kwani aliona kuwa, kwa kuwa mwandishi wa habari hata mazingira yakiwa magumu namna gani lazima atimize jukumu lake. Alisema,

"Matumaini yangu ni kuwa kuikumbuka historia sio kwa ajili ya siku fulani ya maadhimisho bali iwe historia ya kukumbukwa daima, na kila Mchina anapaswa kuikumbuka kwa vitendo katika nafasi yake ya kazi, na aiendeleze historia hiyo."

Kukusanya habari kwa kusafiri mbali ni kazi ngumu na ya hatari, lakini Bi. Fan Chunge anafurahia kazi hiyo. Alisema, kukusanya habari katika sehemu ya mbali imekuwa aina yake ya maisha. Kuipenda kazi ya kukusanya habari kwa kusafiri mbali kunatokana na athari ya wazazi wake. Wazazi wa Fan Chunge ni wachoraji picha, na mara kwa mara walisafiri ng'ambo kuchora picha. Mandhari nzuri za ng'ambo zilizochorwa na wazazi wake zilimwingia sana akilini alipokuwa mtoto, akitamani ataweza kusafiri mbali na kuingiliana na watu wenye mila na desturi tofauti. Alisema, kazi ya uandishi wa habari ilitimiza ndoto zake. Bi. Fan Chunge ni mwandishi wa habari na sio mpiga picha za habari, na hakuwahi kufundishwa elimu ya upigaji picha, lakini kutokana na athari ya wazazi wake, picha anazopiga ni nzuri.

Bi. Fan Chunge alisema, anaweza kuwa hodari zaidi kuliko waandishi wa kiume, kwani waandishi wa kike wana sifa nyingi bora kuliko waandishi wa kiume, alisema,

"Waandishi wa kike wana macho makali na wenye huruma nyingi zaidi, wanachunguza mambo kwa makini zaidi."

Bi. Fan Chunge alipata sifa bora kutokana na juhudi zake, picha alizopiga zilipata tuzo kubwa na yeye mwenyewe amepata tuzo kubwa ya uandishi wa habari nchini China. Lakini Bi. Fan Chunge hakujali tuzo hizo, juhudi zake anazofanya ni kwa ajili ya kuinua uwezo wake. Alisema, ataendelea kukusanya habari kutoka mbali, na ataleta habari nyingi zaidi za kuvutia.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-01