Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-02 15:16:40    
Barua 0802

cri

       Msikilizaji Stephen Magoye Kumalija sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania, ametuletea barua akituambia kuwa safari hii atatutumia picha zake mbili moja ikiwa ni ya ukubwa wa pasipoti na nyingine ikiwa amekaa akiandika maoni yake mbalimbali ya kuja Radio China kimataifa. Vilevile anaomba kama tukiweza tuziweke hizo picha zake mbili kwenye tovuti yetu ili wasikilizaji wenzake waweze kumwona na kumfahamu, kama ikiwezekana pia iwekwe kwenye toleo letu la pili la Daraja la urafiki. Anasema atafurahi sana kama tutaweza kufanya hivyo., Pia anaomba majina ya washindi wa chemsha bongo ya miaka 55 ya ujuzi wa China mpya yachapishwe katika toleo la pili la Daraja la urafiki pamoja na jina la mshindi maalum.

Vilevile katika barua yake hii anapenda kuipongeza Jamhuri ya watu wa China hususan mwakilishi wa China katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa, kwa kuliunga mkono bara la Afrika kuwa na mjumbe kwenye baraza la usalama la Umoja wa Matafia, wakati mwakilishi huyo wa China katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa alipokuwa akizungumza kwenye mkutano na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Benjamin William Mkapa tarehe 1 Juni mwaka huu, ikulu mjini Dar es salaam, Tanzania.

Anamaliza barua yake kwa kusema anatutakia wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa baraka tele na mafanikio mema katika mwaka huu wa 2005, pia tuzidi kusonga mbele na urafiki wetu miaka mingi ijayo.

Msikilizaji wetu kutoka kampuni ya Ulinzi ya Eveready wa sanduku la posta 57333 Nairobi Kenya anasema katika barua yake kuwa yeye angependa kutoa shukrani zake kwa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa kutoa Jarida la Daraja la urafiki kwa wasikilizaji wake wa Afrika. Pongezi zake yeye kama mpenda vipindi vya CRI anatutakia heri njema na kasi yake iwe ya ufanisi mwema. Amepokea jarida hilo kwa dhati na subira njema, anasema hongera na asante kwa kufikiria na kuwajali wasikilizaji wanaosikiliza vipindi vya Radio China kimataifa kwa kuwapatia jarida hilo.

Anasema kuna jambo ambalo angependa kusisitiza na kama litakuwa limetekelezwa atashukuru sana. Jambo lenyewe ni kuhusu kadi za salamu, nafasi iliyotengwa kwa ajili ya kuwasalimia watu na anuwani zao ni ndogo mno, heri tupunguze idadi ya watu toka 8 hadi 6 ili wasikilizaji wawe na nafasi pana kidogo ya kusomewa kadi zao.

Anapenda pia kutushukuru kwa upendo wetu kwa wasikilizaji wetu wa hapo Kenya, huu ni upendo wa kuelewa na kufikiria sana, hakuna anayependa wasikilizaji kama Radio China kimataifa, sababu inayomfanya kusema hivyo ni kwamba, tunawatumia kadi na tena tunawatumia bahasha ambayo imelipiwa gharama za posta. Hii ni ishara kuwa tunawajali na hata kuwakumbuka jinsi walivyo kimapato na uwezo mdogo. Hii ni mojawapo ya upendo tunavyowajali wasikilizaji.

Tunamshukuru msikilizaji wetu kutoka kampuni ya ulinzi ya Eveready kwa maoni na ushauri wake, ushauri wake mzuri tunaweza kuutekeleza. Na pia tunapenda kumwambia kuwa, Bwana Wang Gengnian ni mkuu wa Radio China kimataifa, siyo mkuu wa idhaa ya kiswahili, kama ulivyoandikwa kwenye barua yako, nadhani hapa ulielewa vibaya. Radio China kimataifa kila siku inatangaza kwa lugha 43, zikiwemo lugha 38 za nchi mbalimbali na nyingine za kichina, idhaa ya kiswahili ni idara moja ya Radio China kimataifa.

Msikilizaji wetu Erick Muyemba wa sanduku la posta 215 Sumbawanga Rukwa Tanzania ametuletea barua akisema kuwa anafuraha kutujulisha kuwa yeye huko anaendelea na shughuli zake za ujenzi wa taifa lake Tanzania, na vilevile hajasahau kusikiliza vipindi na habari motomoto zinazowafikia kutoka Radio China kimataifa. Anatushukuru na kutupongeza sana kwa juhudi zetu kubwa za kazi katika idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

Anasema idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa pia inaweza kujitahidi kuongeza na kuwapatia vipindi vingi na vya kutosheleza katika mwaka wa 2005. Ikiwa ni pamoja na kuwaletea makala na masimulizi kutoka kwa wasikilizaji ambazo zinahusu mila na desturi za makabila mbalimbali yanayopatikana katika nchi za Afrika mashariki.

Hivyo basi anapenda kutoa shukrani za dhati kwa watangazaji na wasikilizaji wenzake kwa simulizi na tungo ambazo walikubali kuzituma katika vipindi na mtangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anakamilisha barua yake kwa kusema akiwa msikilizaji wetu mwenezi ataendelea kuwasiliana nasi na kutoa maoni na mapendekezo yake hata katika mwaka 2006.

Tunamshukuru sana kwa barua yake ya dhati na ya kututia moyo tuendelee kuchapa kazi kwa ajili ya kuwahudumia wasikilizaji wetu, nasi tunakuahidi wewe na wasikilizaji wengine kuwa tutaendelea kushirikiana.

Msikilizaji wetu Bramwel Sirali wa sanduku la posta 1325 Kitale Kenya anasema katika barua yake kuwa amepokea barua yetu, anashukuru sana kwa jarida la Daraja la urafiki tulilochapisha, jarida hilo limemfurahisha kutokana na mpangilio wake. Ingawa mengi yaliyokuwemo kwenye jarida ni yale aliyosikiliza kwenye radio, lakini jarida ni kama runinga kwake. Baada ya kazi ya msikio pia macho yamepata kazi, anatushukuru pia kwa msikilizaji mwenzao Bwana Xavier L. Telly Wambwa ambaye amepata ushindi katika shindano la chemsha bongo la mwaka jana na kupata nafasi ya kutembelea Beijing na mji mwingine.

Anasema hajaona dosari kubwa baada ya kulisoma jarida la Daraja la urafiki la toleo la kwanza isipokuwa pengine jinsi tulivyowajulisha kwenye mpangilio wa tatu, hapo chini palipo na picha yetu, neno "wakati" halikuleta mtiririko wa maana halisi. Pia anasema kwa kuwa sasa hivi hajui toleo la mwakani litahusu nini na litatolewa lini, kwa hiyo hawezi akatoa mapendekezo zaidi. Isipokuwa anaamini kuwa litakuwa jarida zuri.

Tunamshukuru sana kwa barua yake na maoni yake, mpango wetu wa kuchapisha jarida dogo ni kila baada ya miezi mitatu, tunatarajia toleo la pili litaweza kuchapishwa si muda mrefu baadaye, dosari zilizopo kwenye toleo letu la kwanza tutazisahihisha baadaye. Tunawashukuru wasikilizaji wetu wanaotusaidia kuandaa vizuri zaidi jarida hilo.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-02