Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-02 19:07:25    
Mchakato wa amani ya Sudan wakabiliwa changamoto kutokana na kifo cha Bw John Garang

cri
    Rais Omar el-Bashir wa Sudan tarehe 1 mwezi Agosti alitoa taarifa akisema kuwa, japokuwa makamu wa kwanza wa rais wa Sudan ambaye pia ni mwenyekiti wa serikali ya kusini Bw. John Garang alifariki dunia katika ajali ya ndege, serikali ya Sudan imepania kuendeleza mchakato wa amani nchini Sudan.

    Bw. Garang alikuwa mwanzilishi na mwenyekiti wa chama cha ukombozi wa watu wa Sudan ambacho ni chama muhimu cha kisiasa katika sehemu ya kusini ya Sudan. Chama hicho kilikuwa nguvu muhimu ya kijeshi iliyoipinga serikali katika sehemu ya kusini, ambacho shughuli zake za kujaribu kuipindua serikali ya nchi hiyo zilisababisha vita ya pili ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan na kusababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 2 na watu milioni 4 kukimbia makazi yao. Kutokana na kusuluhishwa na jumuiya ya kimataifa, pande mbili za kusini na kaskazini za Sudan zilianza kuwa na mazungumzo katika miaka ya 90 ya karne iliyopita. Mwezi Januari mwaka huu, Bw Garang na rais Bashir walisaini mkataba wa amani huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya na kumaliza vita hiyo iliyodumu kwa miaka 21 nchini humo. Kutokana na mkataba huo, Bw Garang alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Sudan tarehe 9 mwezi Julai.

    Tarehe 30 mwezi Julai Bw Garang alifanya ziara binafsi nchini Uganda. Tarehe 31 akiwa njiani kurejea Sudan, helikopta ya rais wa Uganda aliyopanda ilianguka kutokana na hali mbaya ya hewa, Bw Garang na watu wengine 6 walioambatana naye pamoja na marubani na wafanyakazi wa helikopta hiyo wote walipoteza maisha yao.

    Baada ya habari kuhusu kifo cha Bw Garang kutangazwa, hali ya wasiwasi iliwahi kutokea katika Khartoum, mji mkuu wa Sudan. Vijana wengi kutoka sehemu ya kusini walioko Khartoum walikwenda barabarani kupora maduka na kuteketeza magari kwa kuonesha hamaki yao, tena walipambana na askari polisi. Polisi ya nchi hiyo ilisema kuwa ghasia zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 20. Baada ya serikali ya Sudan kuimarisha hatua za usalama na kuweka askari polisi wengi, hali ya Khartoum ilikuwa shwari toka alasiri ya tarehe 1, hivi sasa hakuna watu wengi kwenye barabara za Khartoum isipokuwa wapita njia wachache na askari wa jeshi la usalama. Ili kuzuia hali kuwa mbaya tena, serikali ya Sudan inatekeleza utaratibu wa kupiga marufuku watu kutoka nje wakati wa usiku kutoka saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi.

    Ili kukabiliana na hali mpya ya kisiasa iliyotokea baada Bw Garang kufariki dunia, rais Bashir wa Sudan tarehe 1 aliitisha mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri akitarajia chama cha ukombozi wa watu wa Sudan kitachagua haraka kiongozi atakayechukua nafasi ya Bw Garang na kushika madaraka ya makamu wa kwanza wa rais. Waziri wa habari wa Sudan Bw. Abdel Basit Sabdarat alisema kuwa mkataba wa amani umeagiza uteuzi wa makamu wa kwanza wa rais, ambao wadhifa huo utachukuliwa na kiongozi anayechaguliwa na chama cha ukombozi wa watu wa Sudan.

    Baada ya Garang kufariki katika ajali, chama cha ukombozi wa watu wa Sudan tarehe 1 kilitoa taarifa ikithibitisha kutokea kwa kifo cha Bw Garang na kusisitiza kuwa helikopta aliyopanda ilianguka kutokana na hali mbaya ya hewa wala siyo sababu nyingine. Taarifa hiyo inatoa wito wa kutaka watu wasisikilize uvumi na kuisaidia serikali kupita katika wakati mgumu kwa uvumilivu na kusema kuwa chama hicho kitaendelea kutekeleza mkataba wa amani uliofikiwa pamoja na serikali ya Sudan mwezi Januari mwaka huu. Naibu mwenyekiti wa chama cha ukombozi wa watu wa Sudan tarehe 1 katika mkutano uliofanyika na waandishi wa habari huko Nairobi alitoa wito wa kutaka chama cha ukombozi wa watu wa Sudan kidumishe umoja, kuendelea kufuata nia ya Bw Garang ya kuanzisha Sudan yenye amani. Chama cha ukombozi wa watu wa Sudan siku hiyo kilimchagua Bw. Salva Kiir Miyardeit kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Sudan na kuwa amirijeshi mkuu wa jeshi la ukombozi wa watu wa Sudan linaloongozwa na chama cha ukombozi wa watu wa Sudan.

Idhaa ya Kiswahili