Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-04 15:58:12    
Uasi wa kijeshi watokea nchini Mauritania

cri

Tarehe 3 alfajiri kwa saa za huko, askari walioongozwa na kikosi cha ulinzi wa rais na idara ya usalama wa taifa wa Mauritania walifanya uasi wa kijeshi. Alasiri ya siku hiyo, askari hao walitangaza kuundwa kwa kamati ya kijeshi ya "Demokrasia na Haki" badala ya madaraka ya Rais Taya wa nchi hiyo.

Kamati hiyo ilitoa taarifa tarehe 3 alasiri kwa kupitia shirika la habari la Mauritania, ikisema kuwa, wananchi wa Mauritania "walivumilia mateso mengi" katika miongo kadhaa iliyopita, jeshi la ulinzi na kikosi cha usalama vimeamua kwa kauli moja kukomesha utawala wa rais Taya. Taarifa hiyo imeahidi kuwa, kamati hiyo itaweka mazingira ya demokrasia yenye haki na uwazi yanayoruhusu uhuru wa kutoa maoni, na haitashika madaraka kwa zaidi ya miaka miwili, ili kutayarisha na kujenga chombo halisi cha utawala wa demokrasia. Taarifa hiyo pia imesema kuwa, kamati hiyo pia imeahidi kufuata makubaliano na miktaba yote ya kimataifa iliyoshirikiwa na kusainiwa na nchi hiyo.

Kikosi cha ulinzi wa rais na jeshi la usalama la nchi hiyo zilianzisha ghafla uasi huo wakati rais Taya wa nchi hiyo alipokwenda kuhudhuria mazishi ya mfalme Fahd wa Saudi Arabia. askari walioshiriki kwenye uasi huo hivi sasa wamezikalia idara muhimu za serikali, zikiwemo Ikulu ya nchi hiyo, uwanja wa ndege, vituo vya redio vya taifa, vituo vya televisheni na makao makuu ya jeshi la polisi, na wamedhibiti mji mkuu Nouakchott. Ingawa magari ya kijeshi yameingia kwenye mitaa ya mji huo, na milio ya risasi bado inasikika, lakini inaonekana kuwa uasi huo haukukutana na upinzani mkali. Habari zinasema kuwa, askari walioshiriki kwenye uasi huo pia waliwaachia huru viongozi wa kundi la upinzani la kiislam na viongozi wa uasi wa zamani waliofungwa. Hivi sasa, rais Taya wa nchi hiyo hawezi kurudi nchini Mauritania. Saa kadhaa baada ya kutokea kwa uasi huo, aliwasili mji mkuu wa Niger Niamey kwa ndege kutoka Saudi Arabia, na kupokewa na Rais Mamadou Tanja na maofisa wa serikali ya Niger. na atabaki nchini humo kwa muda.

Mauritania ni moja ya nchi tatu za kiislam zilizoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel, lakini askari walioshiriki uasi hawakushambulia shabaha za Israel nchini humo. Balozi wa Israel nchini humo imearifu wizara ya mambo ya nje ya Israel kuwa, wanadiplomasia wa Israel hawakuathiriwa baada ya kutokea wa uasi huo.

Baada ya askari walioshiriki kwenye uasi kutangaza kupinduliwa kwa utawala wa rais Taya, hali ya nchini humo bado haikutulia. Askari hao tarehe 3 walianza kujadiliana na kumpendekeza kiongozi mmoja mpya, lakini mpaka sasa bado hawajafikia makubaliano.

Aidha, uasi huo ulilaaniwa na jumuiya ya kimataifa. Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bw. Alpha Oumar Konare siku hiyo alitoa taarifa, akisema kuwa, Umoja wa Afrika una wasiwasi kuhusu hali ya nchini Mauritania baada ya kutokea kwa uasi, na Umoja huo unalaani vitendo vyovyote kunyang'anya madaraka kwa nguvu ya kijeshi, na kupinga kithabiti vitendo vyovyote vya kubadilisha utawala kwa njia ya mabavu. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan siku hiyo pia alionesha wasiwasi wake kuhusu tukio hilo, alitaka idara husika zitatue migogoro ya kisiasa kwa amani na kwa njia ya kidemokrasia. Msemaji wa serikali ya Marekani Bw. Tom Casey tarehe 3 alisema kuwa, Marekani inalaani uasi huo na kutumai kuwa serikali inayoongozwa na rais Taya itaweza kuanza kufanya kazi tena mapema.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-04