Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-05 18:12:58    
Serikali mpya ya Somalia yatarajia kufanya ushirikiano wa dhati na China

cri

Waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia Bwana Ali Mohamed Ghedi na waziri wa nishati wa nchi hiyo Bw. Bakar siku chache zilizopita walipohojiwa na mwandishi wa habari wa China huko Giohar, makao makuu ya muda ya serikali hiyo walisema kuwa, serikali mpya ya Somalia inatarajia kufanya ushirikiano wa dhati na China katika mchakato wake wa kulinda amani na kufanya ukarabati, ikitumai kupata uungaji mkono wa serikali ya China na watu wake kwa mara nyingine tena.

Tarehe 13 Juni mwaka huu, serikali ya mpito ya Somalia iliyoundwa zaidi ya miezi saba iliyopita nchini Kenya, ilitangaza kuondoka Nairobi na kurejea nchini Somalia. Serikali ya mpito ya Somalia ilitumai kuionesha jumuiya ya kimataifa kuwa, serikali hiyo ni serikali inayowajibika, kwa hiyo imeamua kurejesha haraka amani ya nchi hiyo, kukarabati uchumi wake na kujipatia msaada wa kiuchumi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Ofisa mwandamizi wa Somalia alidokeza kuwa, serikali ya Somalia inapojitahidi kutuliza mgogoro wa sehemu ya kusini na kuweka mazingira mazuri ya kijamii, itatunga sheria ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji mwingi kutoka nchi za nje. Hivi sasa kampuni 30 za kimataifa zinafikiria kuwekeza nchini humo. Bw. Bakar alisema kuwa, serikali ya Somalia pia itatunga mpango wa kuhimiza maendeleo ya raslimali na nishati ikifuata kanuni ya "Atakayefanikiwa kutafuta raslimali atapewa kibali cha kuchimba na kuleta manufaa kwa pande zote mbili.".

Bw. Bakar alitumaini kuwa, kampuni za China zitakwenda kufanya ukaguzi wa kibiashara katika sehemu ya Puntiland mapema. Somalia iliyokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi ni nchi yenye raslimali nyingi za uvuvi na madini. Kila mwaka inaweza kuvua tani laki tano za samaki, pia ina migodi mingi ya makaa ya mawe iliyo wazi na yenye sifa bora, na aina nyingi za madini kama vile chuma, mafuta, bati na manganese. Licha ya hayo, Somalia pia inatumai kuwa, kampuni za China zitasaidia kuendeleza nishati ya mwangaza wa jua na upepo katika sehemu za pembezoni, kuanzisha kituo cha kuzalisha umeme ili kuwasaidia wakulima wa nchi hiyo katika eneo la umwagiliaji maji na kukuza kilimo. Zaidi ya hayo, kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi, miundo mbinu ya nchi hiyo imeharibika vibaya, viwanja vya ndege, reli, barabara, majumba ya wakazi na hospitali zote zinahitaji kukarabatiwa.

Maofisa wa ngazi tofauti wa serikali ya Somalia wamewahi kueleza mara nyingi kuzikaribisha kampuni za China kuwekeza vitega uchumi nchini Somalia, wakaona kuwa, ukarabati wa Somalia unahitaji sana misaada ya jumuiya ya kimataifa, hasa China. Bw. Bakar alisema kuwa, "ukweli wa mambo umethibitisha kuwa, China ni mshiriki mwaminifu wa Somalia, kiwango cha ujenzi wa miradi na sifa za bidhaa za China zinakubalika kwa watu wa Somalia." Hivyo Somalia inatazamia kufanya ushirkiano zaidi na China katika mchakato wa ukarabati.

Biashara kati ya China na Somalia inaendelea vizuri, kampuni za China zinasafirisha bidhaa za viwanda vyepesi, nguo, dawa na zana za mitambo midogo nchini Somalia, na kuagiza mastic gum na ngozi kutoka Somalia. Kuanzia mwaka 1982, kampuni za China zilianza kusaini mikataba ya miradi ya ujenzi na kusafirisha nguvukazi nchini Somalia.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-05