Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-08 15:58:52    
Suala la nyuklia la Iran lachacha tena

cri

Hivi karibuni, suala la nyuklia ya Iran limechacha tena, ambapo Iran ilikataa mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kutatua suala la nyuklia la Iran na kusisitiza kuanzisha upya shughuli za uranium. Katika hali ya kushindwa kufanya jambo lolote, Umoja wa Ulaya ulitaka kuitisha mkutano wa baraza la shirika la nishati ya atomiki la kimataifa na kujaribu kuilazimisha Iran iache shughuli za kubadilisha uranium kwa shinikizo la kimataifa. Kutokana na jambo hilo, Iran ilieleza kuwa kama suala hilo likiwasilishwa kwenye baraza la usalama, Iran haitakuwa na wasiwasi. Hali ya mazungumzo yaliyoendelea kati ya pande hizo mbili kwa miezi kadhaa imegeuka kuwa ugomvi.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zilizouwakilisha Umoja wa Ulaya kufanya mazungumzo na Iran tarehe 5 ziliipa Iran mapendekezo kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran. Mapendekezo hayo yanakubali Iran kuwa na haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa amani, lakini yanaitaka Iran iahidi kutojitoa katika "mkataba wa kutosambaza silaha za nyuklia" na kuruhusu shirika la nishati ya atomiki la kimataifa lifanye ukaguzi wa ghafla kwa zana zake za nyuklia. Mapendekezo hayo pia yanaitaka Iran isimamishe kabisa shughuli za ubadilishaji, uyeyushaji na utengenezaji wa uranium na kuziachia nchi nyingine ziipatie nyenzo za nyuklia na kurejesha nyenzo hizo zilizotumiwa nayo. Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya uliahidi kuimarisha ushirikiano na Iran katika siasa, uchumi, sayansi na teknolojia. Siku hiyo Marekani ilieleza kuunga mkono mapendekezo ya Umoja wa Ulaya.

Lakini Iran haijaridhishwa na mapendekezo ya Umoja wa Ulaya. Siku mbili zilizopita, Iran ilikataa mapendekezo hayo kwa mara nyingi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bw. Hamid-reza Asefi tarehe 6 alieleza kuwa Umoja wa Ulaya haukutekeleza ahadi yake kwa Iran na mapendekezo hayo hayakuhakikisha haki halali ya Iran kuhusu uranium nzito na kwenda kinyume cha kanuni za "mkataba wa kutosambaza silaha za nyuklia". Msemaji huyo tarehe 7 alisisitiza kuwa Iran itaanzisha upya shughuli za uranium za zana za nyuklia za Isfahan kwa kusimamiwa na shirika la nishati ya atomiki la kimataifa. Rais mpya wa Iran Mohamed Ahmadinejad tarehe 6 alieleza kuwa, Iran haitasujudu kwa tishio la nchi za magharibi.

Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa Iran inachukua msimamo mkali kutokana na kuwa haki yake ya kuanzisha upya shughuli za mabadiliko ya uranium zimelindwa na mikataba husika ya kimataifa. Kwa upande mwingine, Iran inaona kuwa Iran ni nchi kubwa ya pili inayouza mafuta nchi za nje ikiifuata Saudi Arabia katika OPEC. Kutokana na hali ya sasa ya kupanda kwa bei ya mafuta, nchi za magharibi haziwezi kuthubutu kulichochea baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liiwekee vikwazo Iran. Vyombo hivyo vya habari pia vinaona kuwa maendeleo ya suala la nyuklia la Iran yanahusika na kupokezana kwa rais mpya na rais wa zamani wa Iran. Kwa hiyo, havijathibitisha kama rais mpya wa Iran atashikilia msimamo mkali hadi mwisho au atapatanishwa na Umoja wa Ulaya utakaorudi nyuma kwenye suala hilo kama Iran ilivyofanya zamani.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-08