Iran tarehe 8 ilianzisha tena kazi za zana za uzalishaji wa uranium ya gesi, na ilichagua siku moja kabla ya kufanyika kwa mkutano wa dharura wa baraza la uratibu la shirika la atomiki duniani, jambo ambalo limefuatiliwa sana na vyombo vya habari vya nchi za magharibi.
Naibu mwenyekiti wa shirika la atomiki la Iran Bw. Mohammad Said tarehe 8 huko Isfaham alitangaza kuwa, chini ya usimamizi wa wahandisi wa shirika la atomiki duniani, baadhi ya zana za uzalishaji wa uranium ya gesi zilizoko Isfaham zilianza upya uzalishaji. Kabla ya hapo Umoja wa Ulaya ulionya kuwa, kama Iran ikianzisha tena shughuli zinazohusika na usafishaji wa uranium, basi Umoja wa Ulaya utaacha mara moja mazungumzo na Iran kuhusu suala la nyuklia. Marekani nayo ilionya kuwa suala la nyuklia la Iran litapelekwa kujadiliwa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na Iran itakabiliwa adhabu ya kimataifa.
Uzalishaji wa uranium ya gesi, ni kubadilisha madini ya uranium kuwa uranium ya gesi ambayo ikisafishwa itaweza kutumika katika kuzalisha umeme na kutengeneza uranium nzito ambayo inatumika katika uzalishaji wa silaha za nyuklia. Hivyo uzalishaji wa uranium ya gesi siyo sawasawa kabisa na usafishaji wa uranium, lakini ni maandalizi ya lazima ya usafishaji wa uranium nzito. Lakini ni kwa nini Iran inashikilia uzalishaji wa uranium ya gesi bila kujali vitishio vya nchi za magharibi?
Kwanza, Iran inaona kuwa kufanya utafiti na majaribio ya kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani ni haki inayotambuliwa na kulindwa na mikataba husika ya kimataifa, na ni yenye msingi wa kisheria. Hivyo inaona kuwa nchi za magharibi hazina haki ya kuinyima haki yake, nchi za magharibi zinafanya hivyo kutokana na msimamo potofu wa kisiasa, na ni uonevu na ubaguzi kwa Iran. Naibu mwenyekiti wa shirika la atomiki la Iran Bw. Mohammad Said alisema kuwa hata kama mkutano wa baraza la uratibu la shirika la atomiki duniani utapitisha azimio la kuilaani Iran, azimio hilo litakuwa linakwenda kinyume na "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia" na "siyo la halali."
Pili, baadhi ya vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa baada ya kufanya mazungumzo kwa miezi minane, Iran imefahamu kuwa haiwezi kupata vitu inavyotaka katika mazungumzo hayo. Mwezi Novemba mwaka jana, Iran ilisimamisha shughuli zote zinazohusika na usafishaji wa uranium na kuwa na mazungumzo na nchi tatu za Umoja wa Ulaya za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza. Mazungumzo hayo yalifanyika kwa raundi 7, lakini baadaye yalikwama. Katika mpango wa utatuzi uliotolewa na Umoja wa Ulaya hivi karibuni, Umoja wa Ulaya bado unashikilia kuwa Iran inapaswa kuacha milele shughuli za usafishaji wa uranium. Hivyo Iran ilieleza wazi kuwa mpango huo hauwezi kutimiza matarajio yake ya chini kabisa, na kuifanya ikate tamaa.
Tatu, Iran inaona kuwa kuna baadhi ya mambo katika mazingira ya kimataifa ya hivi sasa, yanayosaidia kuinua haki yake kwa msimamo mkali. Hivi karibuni matukio ya ugaidi yalitokea nchini Uingereza na Misri, na jeshi la Marekani limedidimia katika shida mpya, vyombo vya habari duniani vinafuatilia mapambano dhidi ya ugaidi, wakati utatuzi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea unaendelea polepole, Iran inaona sasa ni fursa nzuri ya kutumia mbinu yake hiyo.
Nne, mabadiliko ya uongozi wa serikali ni sababu ya kimsingi ya kutenda kitendo hicho kikubwa. Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa kitendo hicho cha Iran cha kurejesha baadhi ya shughuli za nyuklia zainamaanisha kuwa, suala la nyuklia la Iran limeingia katika kipindi kipya, mvutano kati ya Iran na nchi za magharibi utakuwa mkali zaidi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-09
|