Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-10 16:15:43    
Mkutano wa kuamua mambo kuhusu suala la nyuklia la Iran

cri

Kutokana na ombi la Umoja wa Ulaya, baraza la shirika la nishati ya atomiki duniani liliitisha mkutano wa dharura tarehe 9 mjini Vienna, kujadili hasa suala la nyuklia la Iran. Azimio gani litatolewa kwenye mkutano huo, ni jambo ambalo linafuatiliwa sana na watu.

Mkutano huo ungefunguliwa tarehe 9 asubuhi kutokana na mpango uliowekwa, lakini uliahirishwa mpaka alasiri ili kuwahi kuandaa mswada wa azimio. Baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo, maoni tofauti yalionekana kati ya wanachama 35 wa baraza hilo. Kutokana na ajenda ya baraza hilo, azimio la mkutano huo litapitishwa baada ya kukubaliwa na wanachama wote. Hivyo, sekretarieti ya mkutano huo ilitangaza kusimamisha mkutano huo hadi tarehe 10 alasiri, wajumbe wa nchi mbalimbali wataweza kushauriana faraghani katika mapumziko ya mkutano huo. Wachambuzi wanaona kuwa kama mswada wa azimio utakaotolewa na Umoja wa Ulaya utakuwa mkali, huenda utapingwa na baadhi ya nchi zinazoendelea. Kama mswada wa azimio ungeweza kukubaliwa na pande mbalimbali ungetolewa kwa mashauriano. Habari zinasema kuwa wakati wa kurejeshwa kwa mkutano huo utaahirishwa tena.

Kwa kuwa Iran ilikataa mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya tarehe 5 mwezi huu, na kutangaza tarehe 8 kuanzisha upya baadhi ya kazi za kushughulikia uranium, kwa hiyo suala la nyuklia la Iran lililojadiliwa kwa muda mrefu limekuwa lenye matata makubwa. Mwezi Aprili mwaka huu, Iran ilitoa pendekezo kwa nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kuhusu kubakiza kituo kidogo kisichopungua kimoja cha uranium nzito kilichoko mjini Natanz. Lakini Umoja wa Ulaya na Marekani zote zimechukua mpango wa uranium nzito wa Iran kama sehemu ya mpango wake wa silaha za nyuklia na kuona kuwa baada ya Iran kukamilisha kituo cha uranium nzito cha Natanz, itaweza kuzalisha uranium nzito yenye uwezo wa kisilaha haraka na kujitoa kwenye "mkataba wa kutosambaza silaha za nyuklia" wakati wowote. Kwa hiyo, Umoja wa Ulaya na Marekani zote zinaitaka Iran iteketeze zana zote za kusafisha uranium nzito na kusimamisha mpango wa uranium nzito.

Wanachama mbalimbali wa baraza la shirika la nishati ya atomiki duniani wana maoni tofauti katika suala la Iran kuzalisha uranium nzito. Mjumbe wa Malaysia anayeziwakilisha nchi zisizofungamana na upande wowote ana msimamo wa kuihurumia na kuiunga mkono Iran. Anaona kuwa kuzalisha uranium na kuahidi kutosambaza silaha za nyuklia kwa nchi fulani ni mambo mawili. Alisisitiza kuwa haki ya nchi mbalimbali kutumia nishati ya nyuklia kwa amani isizuiliwe. Russia siku zote inaiunga mkono Iran itumie nishati ya nyuklia kwa amani, lakini wizara ya mambo ya nje ya Russia tarehe 9 ilitoa taarifa ikiitaka Iran isimamishe mara moja shughuli za kubadilisha uranium.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Bw. Mohamed El-Baladei tarehe 9 alipohutubia sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo alieleza matumaini yake kuwa maendeleo ya hali ya hivi sasa ni tatizo dogo, bali sio kuvunjika kabisa kwa mazungumzo. Aliitaka Iran irejee kwenye msimamo wa kusimamisha kwa hiari shughuli za uranium nzito na alizihimiza pande husika ziwe na uvumilivu.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-10