Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-10 21:11:28    
CMOS mpya inayosaidia kompyuta kujikinga dhidi ya virusi vya kompyuta

cri

Hivi sasa, kompyuta zinatumiwa na watu wengi, wengi wanahitaji kompyuta, wakati wa kazi, masomo na burudani. Wakati kompyuta inapowarahisishia kazi, vilevile inawaletea matatizo. Bi. Yang Li ni mfanyakazi wa kampuni moja ya hapa Beijing, yeye anasumbuliwa sana na matatizo kwenye kompyuta, alisema:

"Jumatatu moja, nilifika ofisini, nikagundua kuwa kompyuta yangu haifanyi kazi. Baada ya kuiwasha, haikuwaka. Niliambiwa kuwa kompyuta yangu ilishambuliwa na virusi vya kompyuta, na kulikuwa hakuna uwezekano wa kuitengeneza upya, maana ya hali hiyo ni kuwa nilipoteza kumbukumbu za nyaraka zote zilizohifadhiwa kwenye kompyuta hiyo."

Bi. Yang alisema, kwa kawaida anazingatia sana suala la usalama wa kompyuta, ameweka software zinazoweza kuikinga kompyuta dhidi ya virusi vya kompyuta na kuviua virusi hivyo, alidhani kuwa kwa kufanya hivyo, kompyuta yake itakuwa salama, lakini ajali bado ilitokea bila matarajio.

Hilo ni suala linalowakabili watu wengi. Baada ya virusi vya kompyuta kugunduliwa, viwanda vya kutengeneza software vitafanya utafiti juu ya virusi hivyo, na kutengeneza software za kuviua virusi hivyo, lakini kama aina mpya za virusi vya kompyuta zikitokea, yaani aina zisizojulikana, software hizo hazitaweza kufanya kazi.

Hivyo, katika miaka ya karibuni, kadiri virusi vya kompyuta vinavyoenea, ndivyo suala la usalama wa kompyuta linavyofuatiliwa siku hadi siku, serikali na viwanda vya nchi nyingi vinatilia maanani kuhusu utafiti wa CMOS inayoweza kuikinga kompyuta dhidi ya virusi vya aina mbalimbali. Naibu mkuu wa idara ya utafiti ya kampuni ya Lenovo, ambayo ni kampuni kubwa kabisa ya kutengeneza kompyuta nchini China, Bw. Wei Wei alisema kuwa, njia ya kimsingi ya kutatua suala la usalama wa kompyuta, ni kuiwekea kompyuta CMOS inayoweza kukinga virusi vya kompyuta. Alisema

"CMOS ya aina hiyo inaweza kugundua mabadiliko yanayoletwa na virusi vya kompyuta, halafu itarudisha kompyuta kwenye hali ya mwanzo."

Kampuni ya Lenovo ilianza utafiti kuhusu CMOS ya aina hiyo mwaka 2003, na watafiti zaidi ya 100 walishiriki kwenye utafiti huo, hatimaye utafiti huo ulifanikiwa, hali ambayo imeifanya China izifuate Marekani na Japan kuwa moja ya nchi zenye teknolojia hiyo.

Mwandishi wetu wa habari alifahamishwa kuwa, ukubwa wa CMOS ya aina hiyo ni kama kunde, na haiwezi kufanya kazi bila kushirikiana na CMOS nyingine ndani ya kompyuta. Kutokana na bei yake nafuu, bei za kompyuta zenye CMOS ya aina hiyo na kompyuta za kawaida zinafanana.

Anayeongoza mradi wa utafiti wa CMOS ya aina hiyo wa kampuni ya Lenovo Bw. Xie Wei alisema kuwa, hivi sasa CMOS ya aina hiyo imeanza kutumika. Alisema:

"Hivi sasa, CMOS ya aina hiyo inaweza kutumika kwenye kompyta ya mezani na kompyuta ndogo(laptop). Kampuni yetu imefanikiwa kutengeneza kompyuta ya mezani yenye CMOS ya aina hiyo, na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kompyuta aina ya laptop itapatikana."

Ni mwelekeo wa hivi sasa kutengeneza kompyuta zenye CMOS inayoweza kujikinga dhidi ya virusi vya Kompyuta. Takwimu zilizotolewa na kampuni maarufu ya takwimu duniani, IDC, zinaonesha kuwa, ifikapo mwaka 2007, asilimia 70 ya kompyuta za watu binafsi duniani zitawekewa CMOS ya aina hiyo; na ifikapo mwaka 2009, kompyuta za aina hiyo zisizopungua milioni 5 zitahitajika na idara za serikali na jeshi la China, mbali na zitakazohitajika na watu binafsi.

Kwa kuwa CMOS ya aina hiyo inayotengenezwa na kampuni ya Lenovo siyo tu inatumika kwenye kompyuta zinazotengenezwa na kampuni hiyo, bali pia inatumika kwenye kompyuta zinazotengenezwa na makampuni mengine, hivyo hivi sasa viwanda vingi vya kutengeneza kompyuta vinafanya mazungumzo na kampuni ya lenovo kuhusu biashara ya CMOS ya aina hiyo.

Kutokana na kuwa na utaalam mkubwa wa utengenezaji wa CMOS inayoweza kukinga virusi vya kompyuta, kampuni ya Lenovo inatengeneza aina mpya ya CMOS ya aina hiyo. Bw. Wei, alidokeza kuwa mbali na CMOS ya aina hiyo, kampuni ya lenovo itafanya utafiti kuhusu software za kukinga virusi vya kompyuta na software za uendeshaji wa kompyuta, ili kuunda mfumo kamili wa kujilinda wa kompyuta na kuhakikisha usalama wa kompyuta.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-10