Tume ya uchaguzi mkuu wa Guinea Bissau tarehe 10 ilitoa hadharani matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu, na kuthibitisha mgombea huru ambaye pia alikuwa rais wa nchi hiyo Bw. Joao Bernardo Vieira kuwa rais mteule.
Uchaguzi rais wa Guinea Bissau ulifanyika kwa maduru mawili. Kutokana na matokeo ya duru la pili yaliyotangazwa tarehe 28 mwezi Julai na tume ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, Bw Joao Bernardo Vieira alipata asilimia 55.25 ya kura na kumshinda mpinzani wake, mgombea wa chama tawala kiitwacho chama cha uhuru cha Guinea na Cape Verde Malam Bacai Sanha aliyepata asilimia 44.75 ya kura, hivyo Vieira alishinda kwenye uchaguzi huo. Lakini Malam Bacai Sanha aliyeongoza katika duru la kwanza la uchaguzi huo hakukubali matokeo ya duru la pili ya uchaguzi huo kwa kisingizio cha kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi kwa baadhi ya sehemu na kutaka sehemu hizo zihesabu kura upya.
Kutokana na hali ya hatari iliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Guinea Bissau, Umoja wa Afrika na Umoja wa Uchumi wa Afrika Magharibi uliwatuma mabalozi maalum nchini humo kufanya usuluhishi. Wakaguzi waliotumwa na Umoja wa Ulaya wanaona kuwa uchaguzi mkuu wa Guinea Bissau wa safari hii ni haki, wenye demokrasia na ulifanyika wazi.
Bw Joao Bernardo Vieira alizaliwa mwaka 1939 katika familia ya wafanyakazi mjini Bissau. Mwaka 1960 alijiunga na chama cha uhuru cha Guinea na Cape Verde. Toka mwaka 1961 hadi mwaka 1964, alikuwa kiongozi wa kijeshi wa mkoa wa Catio, kusini mwa Guinea Bissau. Mwaka 1965 alikuwa mjumbe wa tume ya vita. Mwaka 1973 alichaguliwa kuwa mwanachama wa ofisi ya kudumu ya sekretarieti ya chama cha uhuru cha Guinea na Cape Verde.
Baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Guinea Bissau mwaka 1973, aliteuliwa kuwa spika wa bunge la umma la awamu ya kwanza na waziri wa ulinzi. Mwezi Novemba mwaka 1980 aliongoza jeshi lake kuanzisha harakati za mageuzi na kuipindua serikali ya wakati huo na kuwa waziri mkuu wa serikali na kiongozi wa jeshi. Mwezi Novemba mwaka 1981 alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa chama cha uhuru cha Guinea na Cape Verde na kuwa rais wa nchi hiyo mwezi Agosti mwaka 1994.
Mwezi Mei mwaka 1999, Vieira alipinduliwa katika uasi na kukimbia Ureno. Guinea Bissau ni nchi ambayo iko nyuma kabisa duniani. Uasi umetokea mara nyingi nchini humo tangu mwaka 1974 ilipopata uhuru. Idhaa ya kiswahili 2005-08-11
|