Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-11 16:28:41    
Bi. Wang Xuan anayeishitaki serikali ya Japan mahakamani

cri

Japan ni nchi pekee iliyowahi kutumia silaha za vijidudu katika vita kuu ya pili duniani, na China ni nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi na silaha za vijidudu wakati wa uvamizi wa Japan. Hadi leo, katika sehemu nyingi nchini China, baadhi ya wakazi walioathiriwa na silaha za vijidudu wanaendelea kuvumilia maumivu yaliyosababishwa na silaha hizo, lakini serikali ya Japan haikuwahi kuomba radhi au kuwafidia wachina walioathirika. Bi. Wang Xuan, ambaye ni mtoto wa mtu aliyeathiriwa na silaha za vijidudu, amefanya uchunguzi na kukusanya ushahidi kwa miaka 10 hivi, kujitokeza kwenye mahakama ya Japan, na kufichua ukweli wa matumizi ya silaha za vijidudu ya wavamizi wa Japan.

Bi. Wang Xuan mwenye umri wa miaka 53 mwaka huu alisema kuwa, katika familia yake, watu 8 waliathiriwa na silaha za vijidudu. Kabla ya miaka kumi iliyopita, Bi. Wang Xuan alifanya kazi katika kampuni ya Japan. Siku moja alisoma habari kwenye gazeti moja la Kiingereza ikisema kuwa, kongamano la kwanza kuhusu silaha za vijidudu lilifanyika mkoani Heilongjiang, Wajapan wawili walitangaza ripoti yao ya uchunguzi kuhusu hali ya maambukizi ya tauni yaliyosababishwa na silaha za vijidudu vilivyoanzishwa na wavamizi wa Japan katika kijiji cha Chongshan cha mji wa Yiwu, mkoani Zhejiang, mashariki mwa China. Kijiji cha Chongshan ni maskani ya Bi. Wang Xuan, hivyo aliona kuwa anawajibika kushiriki katika uchunguzi huo, ili kuwafahamisha watu ukweli wa mambo ya kihistoria. Anasema:

"Baada ya kusoma habari hizo, niliwapigia simu wapenda amani wa Japan waliofanya uchunguzi katika kijiji cha Chongshan. Niliwaambia kuwa, nataka kushiriki kwenye uchunguzi huo, na nitawaunga mkono kadiri niwezavyo."

Mwaka 1995, Bi. Wang Xuan alianza kushirikiana na kikundi cha raia cha Japan kufanya uchunguzi kuhusu silaha za vijidudu zilizotumiwa katika vita vilivyoanzishwa na wavamizi wa Japan nchini China. Mwanzoni kazi yake ilikuwa ni mkalimani. Katika mchakato wa uchunguzi huo, Bi. Wang Xuan alifahamu mambo mengi zaidi na zaidi kuhusu silaha za vijidudu zilizotumiwa na wavamizi wa Japan kwenye maskani yake.

Hatia zilizofanywa na wavamizi wa Japan zilimshtuka sana Bi. Wang Xuan. Lakini baada ya vita kuu ya pili, kutokana na lengo la serikali ya Japan kuficha historia yake ya uvamizi, watu wachache tu wanafahamu ukweli wa mambo hayo. Wale walioathiriwa na silaha za vijidudu au watoto wao hawajui namna ya kupata fidia kutoka kwa serikali ya Japan. Hivyo Bi. Wang Xuan aliteuliwa kuwa mkuu wa kikundi cha washitaki 180 walioathiriwa na silaha za vijidudu kutoka kwenye mikoa ya Zhejiang na Hunan

Mwezi Agosti mwaka 1997, baada ya matayarisho ya miaka miwili, kwa niaba ya washitaki hao 180, Bi. Wang Xuan aliingia katika mahakama ya Tokyo kwa mara ya kwanza kuishitaki serikali ya Japan, kuitaka serikali ya Japan iombe radhi na kutoa fidia kwa wachina walioathirika. Bi. Wang Xuan anasema:

"Tofauti na hatia nyingine za kivita, hatia ya kuanzisha vita kwa silaha za vijidudu ni hatia ya kikatili zaidi. Lakini hadi leo, serikali ya Japan bado ilikataa kukiri hatia hiyo, wala haijatangaza hadharani data husika."

Baada ya kusikiliza kesi kwa mara zaidi ya 20 katika muda wa miaka mitano, tarehe 27 Agosti mwaka 2002, mahakama ya Tokyo ilitoa hukumu ya kesi hiyo, na ilihukumu kwa mara ya kwanza kuwa, wavamizi wa Japan waliwahi kutumia silaha za vijidudu nchini China, na kukiri kuwa, vita hivyo vimeleta madhara makubwa kwa Wachina, lakini ilikataa dai la kutitaka serkali ya Japan kuomba radhi na kutoa fidia, na kikundi cha washitaki wa China kiliamua kukata rufani mara moja.

Katika miaka minane iliyopita, ili kukusanya ushahidi, Bi. Wang Xuan ametembelea karibu nusu ya eneo la China na kwenda na kurudi kati ya China na Japan kwa kujigharimia. Kwa sababu washitaki hao 180 wote wamezeeka, na 26 kati yao wamefariki dunia wakati wa mchakato mrefu wa kesi yao. Bi. Wang Xuan anapaswa kushindana na wakati.

Nia imara ya Bi. Wang Xuan ya kutafuta haki imewasisimua wachina na wa dunia nzima. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Habari cha Nanjing Bi. Yangfang aliwahi kusikiliza hotuba ya Bi. Wang xuan. Anasema:

"Naona Bi. Wang Xuan ni mwanamke anayestahili kuheshimiwa. anashikilia kuwasaidia watu walioathiriwa na silaha za vijidudu, baada kuishitaki serikali ya Japan mahakamani, vitendo vyake vinahitaji ushupavu na moyo imara wa kutafuta haki." Hivi sasa watu wengi zaidi wameanza kufuatilia historia hiyo, baadhi ya watu hata wanajiunga na kikundi hicho cha washitaki, kukusanya mashahidi husika. Tarehe 19 mwezi Julai mwaka huu, kesi hiyo ilivutia ufuatiliaji mkubwa duniani. Mahakama ya Tokyo ilitoa hukumu, washitaki wa China walioathiriwa na silaha za vijidudu walishindwa kwa mara ya pili. Bi. Wang Xuan alisema kuwa, ataendelea kukata rufani kwenye mahakama kuu ya Japan. Alisema kuwa, kama hatia ya wavamizi wa Japan kutumia silaha za vijidudu haiadhibiwi ipasavyo, itakuwa aibu kwa ustaarabu wa binadamu.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-11