"Kamati ya kijeshi ya demokrasia na haki" ya Mauritania iliyoshika hatamu za kiserikali tarehe 3 baada ya kufanya mapinduzi, tarehe 10 ilianzisha rasmi serikali ya mpito ya Mauritania ambayo waziri mkuu wake ni Sidy Mohamed Ould Boubacar. Hii ni hatua muhimu iliyopigwa na utawala wa kijeshi wa Mauritania katika kutuliza mambo ya kisiasa na kufufua utaratibu wa katiba.
Shirika la habari la taifa la Mauritania limeripoti kuwa, serikali hiyo ya mpito ina mawaziri 19, makatibu wanne wa mambo ya kitaifa, katibu mkuu mmoja wa serikali na mkurugenzi mmoja wa ofisi ya kamati ya kijeshi. Hakuna mjumbe hata mmoja wa "Kamati ya kijeshi ya demokrasia na haki" anayeweza kuingia katika serikali ya mpito. Zaidi ya hayo, serikali ya mpito haikuweka wadhifa wa waziri wa ulinzi, sasa mambo ya ulinzi wa taifa yanashughulikiwa na utawala wa kijeshi.
Baada ya utawala wa kijeshi wa Mauritania kuunda serikali ya mpito, vyama mbalimbali vya Mauritania vimetoa maoni yao tofauti. Kwa kuwa wajumbe wengi wa baraza la mawaziri la serikali ya mpito walitoka kwenye chama cha republican cha jamii ya demokrasia kinachotawala, viongozi wa vyama vya upinzani wanailalamikia sana serikali hiyo, wanaona kuwa wajumbe wa vyama vya upinzani wanapaswa kuingia kwenye serikali ya mpito. Kiongozi wa chama cha muungano wa maendeleo ya umma yaani chama kikuu cha upinzani Bwana Ahmed Ould Daddhah siku hiyo alisema kuwa, kutimiza lengo la kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ndani ya miaka miwili lililotolewa na utawala wa kijeshi ni muhimu zaidi kuliko kuunda serikali ya mpito.
Hali inayostahili kufuatiliwa ni kuwa, hivi sasa msimamo wa jumuiya ya kimataifa juu ya utawala wa kijeshi wa Mauritania unabadilika kimyakimya. Kiongozi wa ujumbe wa ngazi ya mawaziri wa Umoja wa Afrika unaotembelea Mauritania ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa Nigeria Bwana Oluyemi Adeniji, tarehe 10 huko Nouakchott alisema kuwa, Umoja wa Afrika utafanya ushirikiano na utawala wa kijeshi wa Mauritania. Alisema, baada ya kufanya mawasiliano mengi na vyama mbalimbali vya kisiasa na watu wa sekta mbalimbali za jamii, ujumbe huo umeona sababu na ulazima wa kutokea kwa mabadiliko ya utawala nchini Mauritania. Kutokana na hali ya hivi sasa, watu wa sekta mbalimbali wa Mauritania wamefikia maoni ya pamoja ya kupokea utawala mpya wa kijeshi. Hivyo Umoja wa Afrika utaweza kuanzisha ushirikiano na utawala wa kijeshi wa Mauritania siku zijazo. Bwana Adeniji alisiitiza pia kuwa, Umoja wa Afrika hautafufua uanachama wa Mauritania katika Umoja wa Afrika uliosimamishwa baada ya uasi kutokea nchini Mauritania, hadi utawala wa kijeshi wa Mauritania utkapotimiza ahadi yake ya kufanya tena uchaguzi mkuu na kufufua utaratibu wa katiba. Aidha, Marekani iliyowahi kuunga mkono utawala wa Taya wa Mauritania na kushikilia kumwaacha Taya arudi nyumbani kuendelea na madaraka tena, hivi sasa pia imebadilisha msimamo wake juu ya utawala wa kijeshi wa Mauritania. Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Bwana Adam Ereli tarehe 9 alibainisha kuwa, Marekani itashirikiana na utawala wa kijeshi wa Mauritania ili kuhakikisha Mauritania inaweza kufanya mapema iwezekanavyo uchaguzi wa rais na bunge.
Vyombo vya habari vinaona kuwa, utawala wa kijeshi wa Mauritania ulifanya majadiliano na vyama mbalimbali vya kisiasa nchini humo, kutokana na msingi huo, utawala huo uliunda serikali ya mpito katika muda mfupi wa wiki moja bila vikwazo, hii imeonesha kuwa utawala wa kijeshi umefanikiwa kudhibiti hali ya nchini humo, hali hiyo itausaidia uimarishe hadhi yake ya kushika hatamu za kiserikali, na kutambuliwa na wengi kwenye jumuia ya kimataifa.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-11
|