Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-11 20:40:31    
Suala la nyuklia la Iran laendelea kupamba moto

cri

Tarehe 10, chini ya usimamizi wa shirika la nishati ya atomiki la kimataifa, wataalamu wa Iran walifungua lakiri zote zilizobandikwa kwenye zana za nyuklia huko Isfahan, na kuanzisha tena shughuli za kusafisha uranium. Siku hiyo, mkutano wa dharura wa baraza la shirika la nishati ya nyuklia la kimataifa uliathirisha mkutano wa wajumbe wote uliopangwa kufanyika siku hiyo kutokana na kuwa pande mbalimbali bado zina maoni tofauti kuhusu njia ya kutatua suala hilo na majadiliano yasiyo rasmi kwa ajili ya kutunga mswadas wa azimio bado hayajapata maendeleo.

Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki liliitisha mkutano huo kutokana na ombi la Umoja wa Ulaya. Wachambuzi wanaona kuwa, kitendo hicho cha Umoja wa Ulaya kinalenga kufikisha suala hilo kwenye baraza la shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, na juhudi zilizofanyika na Umoja huo hazikufanikiwa kubadilisha msimamo thabiti wa Iran baada ya mazungumzo ya muda mrefu.

Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki lina nchi 138 wanachama, na baraza la shirika hilo linaundwa na nchi 35. kutokana na kanuni za shirika hilo, mswada wa baraza hilo hupitishwa kwa kukubaliwa na wajumbe wote. Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa, ingawa Umoja wa Ulaya na Marekani zimefanya juhudi kubwa katika kuzishawishi nchi mbalimbali zikubali kupitisha "mswada mmoja wenye nguvu" kuhusu suala la nyuklia la Iran, lakini si rahisi kutimiza lengo hilo.

Kwanza, nchi mbalimbali zina uelewa tofauti kuhusu matumizi ya nishati ya nyuklia kwa amani. Ingawa Umoja wa Ulaya na Marekani zimekubali kuwa Iran ina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa amani, lakini haziiruhusu nchi hiyo ianzishe shughuli za kusafisha uranium. Hivyo baadhi ya nchi zinazoendelea zinaionea huruma kwa hali ya kubaguliwa na kuonewa kwa Iran. Hisia hiyo inaonekana kidhahiri zaidi kwenye baraza la shirika la kimataifa la nishati ya atomiki ambalo nchi zisizofungamana na upande wowote zinachukua theluthi ya viti ya baraza hilo.

Wawakilishi wa baadhi ya nchi wanaona kuwa, Iran kuanzisha tena shughuli za uranium chini ya usimamizi wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki hakukiuki mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia. Na pia ni vigumu kwa baraza la shirika hilo kupitisha mswada wa hatua kali dhidi ya Iran kwa kutokuwa na ushahidi wa kutosha. Habari nyingine zinasema kuwa, baadhi ya nchi kubwa zinazoendelea kama Afrika ya Kusini, Brazil na India zikiwa na hali maalum kuhusu suala la nyuklia, mtizamo wa nchi hizo kuhusu suala la nyuklia la Iran unaonekana kuwa nyeti zaidi.

Uchambuzi unaonesha kuwa, ili kupata uungaji mkono, Umoja wa Ulaya lazima 'ulainishe' mswada wa azimio uliotungwa zamani kwenye mazungumzo kati yake na pande mbalimbali. azimio litakaopitishwa kwenye mkutano wa mwisho litataka Iran isimamishe shughuli za uranium, kufikia tena mapendekezo ya Umoja wa Ulaya kuhusu kutatua suala la nyuklia la Iran na kuendelea na mazunguzmo kati yake na Umoja huo. Azimio hilo huenda litatoa onyo kwa Iran, lakini halitapendekeza moja kwa moja kufikisha suala la nyuklia la Iran kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Wataalamu wanaohusika wanaona kuwa, hivi sasa, tofauti za maoni kuhusu suala hilo kwenye baraza la shirika la kimataifa la nishati ya atomiki zimeanza tu kutokea, kama suala hilo likiendelea kupamba moto, mgogoro kati ya Iran na nchi za magharibi utakuwa mkubwa zaidi, na wakati huo huenda tofauti kubwa zaidi zitatokea kwenye baraza hilo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-11