Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-12 20:44:37    
Uongozi bora huleta maendeleo na ufanisi

cri

Kutokana na mwaliko wa Radio China Kimataifa, mkuu wa utangazaji wa Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) Bwana John Osoro mwezi Julai mwaka huu aliitembelea China. Ziara yake ya siku tisa nchini China iliyompa picha nzuri zaidi ni uongozi bora wa serikali ya China unaoleta maendeleo mazuri. Anasema:

"Madhumuni yangu ya kutembelea China ni kujifunza zaidi kuhusu uongozi wa utangazaji, kuona maendeleo ya wakati huu nchini China, na pia kutembelea sehemu mbalimbali za kihistoria."

 

"Nimetembelea ukuta mkuu, kasri la kifalme la enzi ya Ming na Qing, makaburi ya wafalme wa China ya kale, bustani ya majira ya joto(Summer Palace) na sehemu nyingine. Vitu nilivyoviona kule ni vitu vya ajabu, na vinaonesha uzuri wa uongozi bora. Hii inamaanisha kuwa, na sisi Waafrika tutambue kwamba, tukiwa na uongozi bora, watu wetu wataweza kuondokana na matatizo ambayo yanawakabili wakati huu. Yote haya yatawezekana kama viongozi watakuwa wanajitolea, na kuwa mfano wa uongozi ambao unafaa kwa watu wao. Kwa mfano ukuta mkuu wa China ni kitu cha ajabu, ukiangalia na kukumbuka kuwa, Wachina walikuwa wakijenga ukuta huo wakati teknolojia ilikuwa nyuma sana, lakini unaweza kuona mawe makubwa sana yalikuwa yamebebwa na yakachongwa kwa njia nzuri sana."

"Pia kuna njia nyingine ambazo watu wa China wanaendeleza mambo yao hasa vile wanavyopanga kujifunza mambo kutoka nchi za magharibi, halafu wanayabadilisha kuwa ya kichina na kuwafaa watu wa China, au hata kuyaboresha zaidi. Kitu kama hicho kinafaa kuigwa na Waafrika, sisi Waafrika tukichukua kitu au utaalamu kutoka magharibi, unabaki vile vile. Tunangoja tubadilishwe, ingefaa tubadilishe, halafu utaalamu uwe wa kwetu na kuwafaa watu wetu, hata kwa njia ya maana zaidi."

Waswahili husema, kusikia siyo kuona. Bwana John Osoro anaifahamu historia ya China tokea utotoni, na kupitia vyombo vya habari anafahamu kuwa, China imepata maendeleo makubwa katika miaka ya karibuni, lakini kujionea mwenyewe kumempa mshangao usio na kifani. Anasema:

"Sana kinachoshangaza ni kuona jinsi mji wa Beijing ulivyoendelea, kutokana na historia nafahamu kuwa mwaka 1979 China ilikuwa nyuma. Lakini sasa ukiangalia Beijing, huwezi kuutofautishana na Washington, Beijing inaendelea kwa kasi, na maendeleo mengine yanaendelea pia. Kwa hivyo kule kuja hapa na kuona si kuwa najua kwamba London itakuwa nyuma ya Beijing, lakini nafika hapa na nawaambia wale wanaotusikiliza kweli Wachina wanaenda mbio."

Bwana John Osoro alitembelea kituo kikuu cha televisheni cha China (CCTV), Radio ya serikali kuu ya China (CNR) na Radio China Kimataifa (CRI). Alipozungumzia kuhusu ushirikiano kati ya KBC na CCTV na CRI, anasema:

  

"Vipindi vya China ni kama Wachina, hawapendi kugombana, ni kuongea kwa njia ya urafiki, na pia huwa ni vipindi ambavyo vina desturi ambazo ni tofauti kabisa kuliko na desturi ambazo tumezizoea kutoka magharibi, kwa hivyo inafaa pia iwe tuendelee kwa namna hiyo, kwa sababu kwa miaka mingi sisi Wakenya tumekuwa tukiangalia magharibi sisi Wakenya. Tukiangalia magharibi, pia tuangalie mashariki, inaonekana kama tutaendelea zaidi kuliko vile hapo awali."

Kuanzia tarehe mosi Septemba mwaka huu, vipindi vya Radio China Kimataifa vya lugha ya Kiswahili vitaongezewa muda wa matangazo na kuwa saa moja kutoka muda wa nusu saa wa hivi sasa. Bwana John Osoro alitoa maoni yake kuhusu jambo hilo, anasema:

"Kwa kawaida katika kipindi chochote cha radio na televisheni ni muhimu kutilia maanani kwenye habari, kisha baada ya hiyo inafuatwa na kipindi cha maelezo baada ya habari, na vipindi maalum. Pia ni muhimu kutuletea muziki wa kichina kama unavyojua kwamba muziki ni lugha ya dunia. Hii itaboresha matangazo yenu. Kwa sababu Kiswahili kinapanuka sana, kinaenda Sudan, Somalia kwa vile viongozi wao walikuwa Kenya kwa muda mrefu. Kiswahili sasa kimefika Zaire ya zamani, Rwanda, Burundi, Msumbiji kwa miaka mingi. Kiswahili si lugha ya Wakenya, Waganda na Watanzania, ni lugha ya watu wote, na inaendelea kupanuka. Na tungependa vile lugha ya Kiswahili inavyopanuka, pia Radio China Kimataifa iwe inapanua matangazo yake."

Idhaa ya kiswahili 2005-08-12