Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-12 18:23:31    
Mchakato wa amani wa Sudan wakabiliwa na changamoto na kuendelea kusonga mbele

cri

Kiongozi wa chama cha ukombozi wa umma cha Sudan Salva Kiir Mayardit tarehe 11 huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan aliapishwa kuwa makamu wa kwanza wa Sudan ambaye pia ni mwenyekiti wa serikali ya kusini ya nchi hiyo badala ya John Garang aliyefariki dunia katika ajali ya ndege mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kutokana na kifo cha Bw John Garang, mgogoro mkubwa uliwahi kutokea huko Khartoum na kusini mwa Sudan, mgogoro huo ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 130, jumuiya ya kimataifa ilikuwa na wasiwasi kuwa, huenda mchakato wa maafikiano ya amani ya nchi nzima ya Sudan utakwamishwa.

Bwana Mayardit alipoapishwa alitoa hotuba kwenye sherehe alisema, ataitii Jamhuri ya Sudan, ataendelea kutekeleza makubaliano ya amani ya pande zote yaliyosainiwa kati ya chama chake na serikali ya Sudan mwezi Januari mwaka huu kuhusu kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 21. Na amewataka wananchi wote wa Sudan wafanye juhudi kujiunga na mchakato wa maafikiano ya amani ya nchi nzima ya Sudan, pamoja na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa sehemu ya Darfur ya magharibi ya Sudan, ili wananchi wote wa Sudan wakiwemo wananchi wa kusini mwa Sudan watimize tena mshikamano.

Bwana Mayardit pia alimsifu rais Omar el Bashir kwa juhudi zake kubwa katika kusaini makubaliano ya amani ya pande zote. Alisema, yeye mwenyewe kamwe hawezi kwenda kinyume cha njia ya amani iliyochaguliwa na marehemu John Garang aliyekuwa kiongozi wa chama cha ukombozi wa umma cha Sudan na malengo ya chama hicho.

Rais Bashir pia alitoa hotuba kwenye sherehe. Alisifu chama cha ukombozi wa umma cha Sudan juu ya ushupavu wake wa kudhamiria kuendelea na juhudi katika mchakato wa maafikiano ya amani ya nchi nzima baada ya kiongozi wake wa zamani kufariki dunia katika ajali ya ndege. Rais Bashir alisema, serikali ya Sudan itafanya juhudi pamoja na chama cha ukombozi wa umma cha Sudan katika kutokomeza mambo yaliyopita, kuvumiliana, kuaminiana na kushirikiana ili kutokomeza umaskini na balaa zilizoikumba Sudan katika miaka mingi iliyopita.

Kutokana na makubaliano ya amani ya pande zote yaliyosainiwa kati ya serikali ya Sudan na chama cha ukombozi wa umma cha Sudan mwezi Januari mwaka huu, sehemu ya kusini mwa Sudan itapiga kura za maoni ya raia baada ya miaka 6, ili kuamua kama sehemu ya kusini ya Sudan itatangaza kujitawala au la. Kabla ya hapo kulikuwa na uvumi kuwa, kiongozi wa zamani wa chama cha ukombozi wa umma cha Sudan John Garang alishikilia kuifanya sehemu ya kusini ya Sudan ijiendeshe kwa kiwango cha juu chini ya msingi wa muungano wa taifa la Sudan, na Bwana Mayardit alitaka kuifanya sehemu ya Sudan ijitenge na taifa la Sudan. Hivyo watu wengi walikuwa na wasiwasi kwamba kiongozi mpya wa chama cha ukombozi wa umma cha Sudan Mayardit baada ya kuchaguliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Sudan na mwenyekiti wa serikali ya kusini huenda atakwenda kinyume na sera zilizofuatwa na kiongozi wa zamani, na kwenda mrama katika njia ya amani, na kuisaidia kusini mwa Sudan ijitenge na taifa. Kutokana na uvumi huo, Bwana Mayardit tarehe 11 alipohojiwa na Radio ya taifa ya Sudan alisema kwa kiarabu akieleza wazi kuwa, kazi anayotaka kuifanya ni kutekeleza kwa pande zote makubaliano ya amani. Alisema, lazima kuangalia vitendo vyake halisi badala ya kuamini uzushi.

Wachambuzi wanaona kuwa, kuchaguliwa kwa Mayardit kumeonesha nia ya serikali ya Sudan na chama cha ukombozi wa umma cha Sudan ya kuendelea kusukuma mbele mchakato wa maafikiano ya amani ya nchi nzima.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-12