Baada ya majadiliano, baraza la Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani tarehe 11 huko Vienna lilipitisha azimio likionesha ufuatiliaji mkubwa kwa Iran kuanzisha tena shughuli za kusafisha uranium, na kuitaka Iran isimamishe shughulizo zote, lakini azimio hilo halitaji kama shirika hilo litaliwasilisha suala hilo kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Azimio hilo linaitaka Iran iruhusu Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani lifunge tena vifaa vya kusafisha Uranium vilivyofunguliwa hivi karibuni, na kutaka katibu mkuu wa shirika hilo Bw. Mohamed el-Baradei atoe ripoti kuhusu hali ya Iran kutekeleza mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia kwenye baraza la shirika hilo kabla ya tarehe 3 mwezi Septemba. Azimio hilo lilisema kuwa, shirika hilo bado halijaweza kufahamu kama Iran imeficha shughuli za nyuklia. Hivyo, masuala kadhaa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran bado yanatakiwa kuchunguzwa.
Azimio hilo lilitolewa baada ya Umoja wa Ulaya na nchi nyingine wanachama wa baraza la Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani hasa nchi zisizofungamana na upande wowote kujadiliana na kuafikiana. Baada ya mkataba huo kupitishwa, Bw. Baradei alisema kuwa anatumai Iran itafikiria msimamo wake tena, kwani majadiliano ni njia pekee ya kutatua suala la nyuklia la Iran. Alisema kuwa, mgogoro uliosababishwa na Iran kuanzisha tena shughuli za kusafisha uranium bado unaweza kutatuliwa kwa mazungumzo. Pia alisema wazi kuwa, baada ya Iran kusimamisha shughuli hizo basi itakuwa na uaminifu kwa jumuiya ya kimataifa.
Iran ilipinga azimio hilo mara moja, na kuonesha ghadhabu yake. Mwakilishi wa kudumu katika Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani Bw. Cyrus Nasseri alisema kuwa, Iran haitasalimu kwa shinikizo la nje, na itaendelea na njia yake. baada ya miaka 10, Iran itakuwa nchi inayozalisha nishati ya uranium. Lakini pia alisema kuwa, Iran itaendelea kutekeleza ahadi yake ya kutoeneza silaha za nyuklia na kushirikiana na Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa, maneno yaliyotumiwa kwenye azimio hilo si makali sana. Sababu yake ni kuwa, kwanza, nchi nyingi wanachama wa baraza hilo zinapinga azimio lenye maneno makali, pili, Umoja wa Ulaya pia una lengo lake. Katika muda mrefu uliopita, Umoja wa Ulaya ulisisitiza kutatua suala la nyuklia la Iran kwa mazungumzo, na kuipinga siasa kali ya Marekani. Umoja wa Ulaya unajua vizuri kuwa, hivi sasa Iran inalinda haki yake "isiyoweza kunyimwa" bila ya kujali kama itasababisha mgogoro wa kimataifa. Kama Iran inawekewa shinikizo kubwa, mgogoro utakuwa mkubwa zaidi, hata Iran haitashiriki kwenye majadiliano. Na itamaanisha kushindwa kwa juhudi na mawazo ya kidiplomasia ya Umoja wa Ulaya. Umoja wa Ulaya unaona kuwa, hivi sasa bado haujafikia muda wa mwisho wa kukabiliana na Iran, hautaki kuona kuwa suala la nyuklia la Iran linashindwa kudhibitiwa.
Watu wanaona kuwa, suala la nyuklia la Iran ni ushindani kati ya Marekani na Iran. Lakini hivi sasa Marekani haijachukua hatua nyingi. Sababu yake ni kuwa, Marekani inasumbuliwa na suala la Iraq na Afghanistan, na inataka ushirikiano wa Iran kutuliza hali ya Iraq, hivyo Marekani haitaki kuikasirisha Iran.
Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa, baada ya baraza la Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani kupitisha azimio hilo, sasa ni wakati wa Iran kuchukua hatua zake. Iran ina wakati wa kutosha kufikiria hatua zake kabla ya katibu mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani kuwasilisha ripoti kwenye baraza la shirika hilo. Lakini mambo mengi yameonesha kuwa, Iran haitafuata kikamilifu azimio hilo, upinzani kati yake na Umoja wa Ulaya na Marekani hauepukiki. Lakini pande mbili bado zina fursa ya kufanya majadiliano. Watu wanatumai kuwa Umoja wa Ulaya na Iran zitashikilia mazungumzo na kuacha upinzani, ili hatimaye suala hilo litatuliwe.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-12
|