Katika miaka ya hivi karibuni uhusiano kati ya China na Kenya unaendelea vizuri na kwa utulivu katika sekta mbalimbali, ambapo pande hizo mbili zimeimarisha siku hadi siku maingiliano na ushirikiano katika sekta za siasa , uchumi, utamaduni na elimu na utalii. Ziara ya Rais Mwai Kibaki nchini China kuanzia tarehe 15 hadi 19 hakika itasukuma mbele zaidi maendeleo ya uhusiano kati ya China na Kenya.
Tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Kenya tarehe 14 Desemba, 1963, hasa katika zaidi ya miaka 20 iliyopita ya hivi karibuni, uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaimarishwa barabara siku hadi siku, ambapo viongozi wa nchi wanatembeleana mara kwa mara. Mwezi Februari, mwaka huu, Rais Kibaki wa Kenya alipokutana na naibu waziri mkuu wa China Bwana Zeng Peiyan aliyetembelea Kenya alisisitiza kuwa, serikali ya Kenya inashikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja, na alisema Kenya siku zote inaichukulia China kuwa ni mmoja kati ya marafiki zake wakubwa kabisa. Mwezi Machi mwaka huu, serikali ya Kenya na bunge la taifa la Kenya zote zilieleza kuunga mkono Bunge la umma la China kupitisha "Sheria ya kupinga kufarakanisha taifa". Mwezi Mei mwaka huu, kwenye mkutano wa afya wa dunia uliofanyika huko Geneva, Ujumbe wa Kenya ulitoa hotuba ukiunga mkono msimamo wa China na kutoa mchango wenye juhudi na kupinga pendekezo lililohusika na Taiwan. Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Bwana Chirau Mwakwere mwezi Juni mwaka huu alipofanya ziara nchini China aliishukuru serikali ya China kwa misaada mbalimbali inayotoa kwa maendeleo ya uchumi wa Kenya. Alisema Kenya inapenda kushirikiana na China katika kuhimiza uhusiano wa nchi hizo mbili uendelee siku hadi siku.
Wakati huo huo, mwelekeo wa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya unaridhisha. Tokea miaka ya 90 ya karne iliyopita, biashara kati ya China na Kenya imeendelea kwa haraka, ongezeko la biashara kati ya nchi hizo mbili lilizidi lile la jumla la biashara ya China na nje na kuzidi lile la biashara ya China na nchi za Afrika. Mwaka 1995, thamani ya biashara kati ya China na Kenya ilizidi kwa mara ya kwanza dola za kimarekani milioni 100.
Misaada ya China kwa mambo ya uchumi wa Kenya imesifiwa sana na serikali ya Kenya na watu wa sekta mbalimbali wa jamii ya Kenya. Tokea Kenya ipate uhuru, misaada ya aina mbalimbali ya China kwa Kenya imefikia renminbi yuan milioni 820, kati ya hizo mikopo isiyo na riba imefikia yuan milioni 460, na misaada bila malipo ilifikia yuan milioni 210.
Mwezi Januari mwaka huu China ilitoa msaada wa dola za kimarekani laki 1 na vifaa vya msaada vyenye thamani ya yuan milioni 2.85 kwa Kenya kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa baada ya tetemeko la ardhi lililotokea kwenye bahari ya Hindi. Wakati huo huo, makampuni ya China na ya Kenya yamesaini mikataba ya miradi mbalimbali kuhusu mawasiliano ya habari, na mfumo wa upashanaji habari.
Aidha, ushirikiano kati ya China na Kenya kwenye sekta ya utalii pia unaendelea vizuri. Mwezi Desemba mwaka 2004, makubaliano ya utalii kati ya China na Kenya yalianza kutekelezwa rasmi, Kenya imekuwa nchi moja kati ya nchi zinazowapokea watalii. Kutokana na takwimu zilizotolewa na idara ya utalii ya Kenya, toka mwezi Januari hadi mwezi Mei mwaka huu, watalii wa China waliokwenda kutalii Kenya waliongezeka kwa asilimia 38.6. Idara za utalii za Kenya zinaongeza nguvu kuvuta watalii wa China.
Na ushirikiano kati ya China na Kenya katika sekta ya elimu vilevile unaendelea kwa utulivu. Hivi sasa kuna kituo cha mafunzo ya kichina katika Chuo kikuu cha Egton cha Kenya. Na chuo cha Confucius katika Chuo kikuu cha Nairobi kitaanzishwa na kufunguliwa mwezi Septemba mwaka huu.
Hivi karibuni, serikali ya Kenya imeiruhusu China ianzishe kituo chake cha FM huko Nairobi. Hiki kitakuwa kituo cha kwanza cha FM kitakachojengwa na China katika nchi za nje.
Idhaa ya kiswahili 2005-08-15
|