Israel imeanza kutekeleza mpango wa upande mmoja wa kuondoka kutoka sehemu ya Gaza na kando ya magharibi ya mto Jordan kuanzia tarehe 15 alfajiri. Ili kuhakikisha kuwa mpango huo unatekelezwa bila vikwazo, pande mbili Israel na Palestina zinafanya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kufanya shughuli hizo bila vikwazo.
Kuanzia tarehe 14 alasiri, Israel nzima tayari iliingia kwenye hali ya kuwa macho na hali hiyo itamalizika baada ya kukamilisha mpango huo. Alasiri ya siku hiyo, polisi wa Israel walianza kuweka vizuizi katika sehemu ya kusini mwa Israel inayopakana na sehemu ya Gaza na kufanya ukaguzi kwa magari yote yaliyoelekea kwenye makazi ya Wayahudi yaliyoko katika sehemu hizo, ili kuwazuia wapinzani wa mpango huo wasiingie kwenye sehemu ya Gaza. Kuanzia usiku manane wa tarehe 14, kituo cha ukaguzi cha Kisufim kilifungwa kwa magari yote ya raia wa Israel kuingia katika sehemu ya makazi.
Zaidi ya hayo, jeshi la Israel lilidokeza kuwa Israel itawatuma polisi elfu 42 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kuondoka Israel.
Ili kuhakikisha Israel inaondoka kwa usalama, jeshi la Israel liliwapanga kwa makini polisi wanaoshughulikia mpango huo kwa taratibu za mizunguko sita.
Kutokana na mpango uliowekwa, mpango huo wa upande mmoja utatekelezwa kwa wiki nne. Lakini waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Shaul Mofaz hivi karibuni alieleza matumaini yake kuwa, pande mbalimbali zitashirikiana vyema na kukamilisha mpango huo mapema kabla ya tarehe 4 mwezi Septemba.
Wakati huo huo, Palestina pia inafanya maandalizi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa kuondoka Israel. Tarehe 14, askari elfu kadhaa wa jeshi la usalama la Palestina walipelekwa nje ya makazi ya Wayahudi ili kuyazuia makundi yenye silaha ya Palestina yasishambulie Wayahudi waliokuwa wakiondoka huko Gaza. Hadi usiku wa tarehe 14 askari wote wa jeshi la usalama la Palestina wapatao elfu 7.5 walikuwa tayari wapo kwenye nafasi zao. Isitoshe, pande mbili Israel na Palestina zimeanzisha ofisi ya shughuli za pamoja katika sehemu ya mpaka wa Gaza, kusimamia mchakato wa kuondoka Israel na kufanya uratibu wa mambo ya usalama.
Hivi karibuni, idara mbalimbali za Palestina zilifanya kampeni kubwa kusherehekea kuondoka kwa Israel kutoka sehemu ya Gaza. Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas hivi karibuni alisema kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika mjini Gaza: "Leo, Wapalestina wanasherehekea ukombozi wa Gaza na kando ya magharibi ya mto Jordan na kesho tutasherehekea ukombozi wa Jerusalem". Makundi ya upinzani ya Hamas na Jihad pia yalifanya maandamano makubwa. Kiongozi wa Hamas alieleza kuwa kuondoka Israel kutoka sehemu ya Gaza ni matokeo ya mapambano ya kisilaha ya Palestina na Hamas itaendelea na mapambano baada ya kuondoka kwa Israel kutoka sehemu ya Gaza. Kama Israel haitamaliza ukaliaji wake katika Palestina, kamwe Kundi la Hamas halitasalimisha silaha.
Idhaa ya kiswahili 2005-08-15
|