Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-15 15:36:26    
Mtarizi wa kabila la Wamiao, Zhang Chunying

cri

Utarizi wa kabila la Wamiao ulianza zamani sana, utarizi huo unarithiwa kutoka kizazi hadi kizazi miongoni mwa wanawake wa kabila hilo. Lakini kutokana na jinsi jamii inavyoendelea?ufundi huo uliokuwa na historia ndefu umezorota, kama ni ua lililochanua sana katika bustani ya maua ya sanaa, sasa limeanza kusinyaa.

Kabila la Wamiao ni moja kati ya makabila madogo madogo nchini China. Watu wa kabila hilo wanaishi katika mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China. utarizi ulikuwa ni ufundi ulioenea sana miongoni mwa wanawake wa kabila hilo. Tokea watoto wenye umri wa miaka kumi hivi hadi wanawake wazee wenye mvi, wote walikuwa hodari katika utarizi wa mapambo ya aina mbalimbali kwenye nguo za kawaida, mavazi ya sikukuu, mashuka na vitambaa vya mezani. Wasichana wa kabila hilo wanaanza kujifunza ufundi huo tokea wanapokuwa na umri wa miaka saba hivi na wanapokuwa na umri wa miaka 14 au 15 wanakuwa mafundi wakubwa wa utarizi. Ufundi wa kutarizi haufundishwi na walimu, bali mama huwafundisha mabinti na dada huwafundisha ndugu zao wadogo. Mtarizi hodari Zhang Chunying alipohojiwa na waandishi wa habari alisema,

"Tumezoea kuvaa nguo tulizotarizi toka tulipokuwa watoto. Katika miji, pengine watu wasiosoma wanadharauliwa, lakini kwetu watu wasiokuwa na ufundi wa kutarizi wanadharauliwa, wasichana kama hao hata ni shida kupata wachumba. Kwa hiyo toka tunapokuwa watoto lazima tujifunze utarizi."

Bi. Zhang Chuying ana umri wa miaka 36, amefungua duka la vitu vya utarizi wa kabila la Wamiao katika mji wa Guiyang, mji mkuu wa mkoa wa Guizhou, anauza vitu vilivyotariziwa na yeye na ndugu wenzake. Alipozungumza na waandishi wa habari, kwa makusudi alivaa nguo aliyotarizi mwenyewe. Kwenye shati, sketi, aproni na hata viatu vyake, vyote vilitariziwa kwa mapambo ya aina mbalimbali. Tarizi hizo zinamng'arisha na kumpendeza sana.

Bi. Zhang Chunying alisema, nguo alizovaa zote alizitarizi yeye mwenyewe. Bi. Zhang Chunying alikuwa mwepesi wa kujifunza utarizi tokea alipokuwa mtoto, na sasa amekuwa fundi mkubwa.

Wanawake wa kabilala Wamiao, wana mila ya kujifungia ndani na kufanya kazi majumbani, hawatoki na hawasomi, kwa hiyo kati ya wanawake hao Bi. Zhang Chunying ni mwanamke mwenye bahati ya kuona mengi. Alipokuwa na umri wa miaka 20 alikwenda mji wa Guangdong kufanya kazi ya utarizi katika kiwanda kimoja. Ingawa alishuhudia utarizi wa mashine lakini anaona utarizi wa jadi kwa mikono ni mzuri zaidi. Wakati wa mapumziko anaendelea kutarizi kwa mikono. Baadaye alipeleka tarizi zake kushiriki katika maonesho ya tarizi mjini Beijing, aligundua kwamba tarizi za kabila lake zinakaribishwa sana, basi alifungua duka la kuziuza. Wageni walioko mjini Beijing wanapenda sana, na wanazichukua tarizi kurudi nyumbani kama ni mapambo ya nyumbani.

Ingawa biashara yake ilikuwa nzuri, lakini aliiacha na kurudi nyumbani kwa sababu ya kuwajibika kuwatunza wazee na watoto wake. Kutokana na biashara yake alifahamu kuwa utarizi wa kabila lake ni sanaa inayowapendeza sana wageni, na huku aliona kuwa wasichana wengi wameacha utarizi wa jadi, bali wanajitahidi kuondoka majumbani kuchuma pesa, utarizi wa kabila lake unakabiliwa na hatari ya kutoweka. Kutokana na hali hiyo alitumia fedha zake kuanzisha kiwanda cha utarizi na kuwaajiri wafanyakazi sitini na kuuza tarizi katika nchi za nje. Bi. Zhang Chunying alisema,

"Bei ya vitu vya utarizi imekuwa ghali siku hadi siku kwa sababu wanaofanya kazi hiyo wamekuwa wanapungua. Kutarizi kunataka fundi awe na moyo mtulivu, akifikiri mambo mengine atashindwa kutarizi vizuri. Hivi sasa watu ninaowashirikisha kwenye kazi ya utarizi nawapatia nafasi ya kusoma, ili wapate ufundi na elimu kwa pamoja."

Bi. Zhang Chunying alisema, seti moja ya nguo iliyotariziwa kwa makini inaweza kuuzwa kwa dola za Kimarekani elfu sita.

Licha ya kutarizi nguo kwa ufundi wa jadi, kiwanda chake pia kinatoa tarizi moja moja ili kukidhi mahitaji ya sokoni. Alisema,

"Nafikiri, sio kila mtu anapenda kitambaa tulichofuma cha kabila letu, lakini wanapenda aina fulani za tarizi zetu, kwa hiyo tunatarizi maua kwenye vipande vya kitambaa na kutundika dukani, wateja wanaweza kuchagua vipande wapendavyo na kutia kwenye nguo yao au kuvichukua nyumbani kama ni mapambo."

Katika duka lake mjini Guiyang kwenye ukuta alitundika tarizi zake, na tarizi hizo pia ni maonesho ya sanaa ya kabila la Wamiao.

Bi. Zhang Chunying alisema, utarizi wa kabila la Wamiao ni utajiri na ufahari wa kabila lake, kama usiporithishwa kwa kizazi kipya utatoweka kabisa. Alisema nia yake ya kuchuma fedha sio kwa ajili ya kujenga nyumba kama wengine walivyo, bali ni kwa ajili ya maendeleo ya utarizi wa kabila lake.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-15