Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-16 15:37:02    
Siku ya kwanza kwa Israel kuondoka kutoka Gaza

cri

Tarehe 15 ilikuwa siku ya kwanza kwa Israel kutekeleza mpango wake wa kuondoka kutoka Gaza. Siku hiyo ingawa vitendo vyake vya kuondoka huko vilisusiwa na wakazi fulani, lakini jeshi la Israel lilisema kuwa, kwa ujumla mpango ulitekelezwa vizuri.

Kutokana na mpango wa serikali ya Israel, siku hiyo askari polisi wa Israel wapatao elfu kadhaa waliingia kwenye sehemu zote za makazi yalikoyo kwenye kanda ya Gaza na kuwapa taarifa wakazi wa huko na kuwataka waondoke kwa hiari kabla ya saa moja usiku ya tarehe 17, ama sivyo askari polisi wa Israel watawaondoa kwa nguvu wakazi waliong'ang'ania huko.

Asubuhi ya siku hiyo waandishi wetu wa habari walipanda basi kubwa lililoandaliwa na jeshi la Israel wakifika sehemu ya makazi ya Ganei Tal ya wayahudi kwenye kanda ya Gaza kufanya mahojiano. Sehemu hiyo ya makazi ilijengwa mwaka 1979, ambapo kuna familia 65 za wakazi, wengi wao ni waumini watiifu wa dini ya kiyahudi. Waandishi wetu wa habari walipofika huko, mlango wa sehemu hiyo makazi ulifungwa, walinzi wa mlango wote walikuwa watoto wenye umri zaidi ya miaka 10 tu, ambao walikataa basi kubwa la jeshi la Israel kuingia kwenye sehemu hiyo ya makazi. Saa 3 asubuhi waliwaruhusu waandishi wa habari waingie mlango wa sehemu hiyo ya makazi, lakini hawakuwaruhusu waandishi wa habari waingie ndani ya makazi kuwahoji watu, na basi kubwa la jeshi la Israel na magari mengine ya waandishi wa habari yalilazimika kuegeshwa nje ya mlango. Saa 4 asubuhi ya siku hiyo, waandishi wetu wa habari waliona kuwa mabasi kadhaa ya askari polisi wa Israel yaliegeshwa kwenye sehemu yenye umbali wa mita mia kadhaa nje ya sehemu hiyo ya makazi, ambapo wakazi wa huko walitoka nje ya nyumbani na kufika kwenye mlangoni wa sehemu hiyo ya makazi, wakinyanyua bendera za rangi ya machungwa na kuimba nyimbo za dini ya kiyahudi, wakawazuia askari polisi wasiingie kwenye sehemu hiyo ya makazi. Askari polisi walifanya mazungumzo magumu na wajumbe wa wakazi wa sehemu hiyo, lakini walishindwa kuwabembeleza. Mwishowe walifikia makubaliano kwamba wajumbe wa wakazi watatoa taarifa ya kuondoka kwa wakazi wa huko, na askari polisi hawataingia kwenye sehemu hiyo ya makazi kwa muda.

Habari zilisema kuwa, hali kama hiyo ilitokea pia katika sehemu nyingine za makazi.

Asubuhi ya siku hiyo wakazi wayahudi wapatao 400 hivi waliopinga mpango wa upande mmoja kuondoka Gaza hata walizuia njia ya kuingia sehemu ya makazi ya Gush Katif ya Gaza, wakijaribu kuharibu mpango wa kuondoka ulioanza rasmi kutekelezwa.

Ingawa vitendo vya kuondoka Gaza vilisusiwa na watu kadha wa kadha, lakini siku hiyo familia 897 kati ya familia 1486 za wakazi wa huko zimekubali kuondoka kabla ya tarehe 17. Wakazi wa sehemu 3 za makazi katika sehemu ya kaskazini ya Gaza, na wakazi wa sehemu ya makazi ya kusini mwa Gaza wote waliondoka siku hiyo, hata kwenye sehemu za makazi ambapo wakazi fulani wanasusia vikali kuondoka huko, pia kuna wakazi wengi wameanza kufunga mizigo na kuajiandaa kuondoka kabla ya askari polisi kuchukua hatua ya kuwalazimisha.

Radio ya jeshi la Israel ilitangaza kuwa, baraza la mawaziri la Israel tarehe 15 lilipiga kura na kuidhinisha utekelezaji wa mpango wa upande mmoja wa kuondoka kutoka sehemu kubwa kabisa ya makazi ya Gush Katif kwenye kanda ya Gaza.

Usiku wa siku hiyo waziri mkuu wa Israel Sharon alitoa hotuba kwenye televisheni akisema kuwa, kutekeleza mpango huo ni chaguo la Israel la kufuata hali mpya ya mashariki ya kati, Israel haitabadilisha ratiba ya kutekeleza mpango huo bila kujali kukumbwa na vikwazo gani.

 

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-16