Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-16 15:43:50    
Barua 0816

cri

        Msikilizaji wetu Fesbeth Melimah wa sanduku la posta 172 Bungoma Kenya ametuletea barua akisema kuwa, angependa kutupongeza kwa kazi yetu nzuri. Zaidi ya hayo amefurahi sana kusoma jarida dogo la daraja la urafiki tulilomtumia. Anasema kwa kweli walifurahi pamoja na baba hata mama yake pia.

Isitoshe tulichapisha shairi lililotungwa na baba yake liitwalo wahariri wema pamoja na picha yake. Anatufahamisha kuwa kwa niaba yake wamepata sifa nzuri kwa ajili ya uhusiano mwema wa kuwa marafiki na sisi. Kwa hivyo angefurahi iwapo tutamtumia jarida lingine, kwani mara kwa mara marafiki zao wanahitaji wasome na wanataka kuwa mashabiki wa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa. Na hii imekuwa vigumu kwani baba yake anataka jarida moja libakie kwake.

Anasema jambo lingine ni kuwa huwa wanafurahia mara kwa mara kusikiliza salamu kwa kupitia kipindi cha salamu zenu cha Radio China kimataifa. Na huwa wanamwarifu baba yao na hawakosi kununuliwa zawadi iwapo watamfahamisha mambo ya matangazo ambayo wameyasikia wakati yeye hayuko. Na wanatumai hata sisi tutaweza kuwakumbuka na kuwaletea zawadi. Hata hivyo wanashangaa China ni wapi? Na ni watu gani wanaoishi huko? Wanakula vyakula gani? Mwisho kuna watoto kama mimi na wenzangu?

Tunamshukuru msikilizaji wetu Fesbeth ambaye barua yake kwa kweli imetufurahisha. Tunapenda kukwambia kwa maneno machache kuwa, China iko barani Asia, mashariki ya dunia, na ni mbali na Bara la Afrika, idadi ya watu wa China ni kubwa ambayo imefikia bilioni 1.3. Wachina wanapenda kula wali, tambi, vyakula vya unga wa ngano, na vyakula vingi mbalimbali. Nchini China wapo watoto wengi kama yeye na wenzake.

Msikilizaji wetu Silas Stephano wa shule ya sekondari ya Bunda sanduku la posta 400 Bunda Mara Tanzania anaanza barua yake kwa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wa Radio China Kimataifa. Anasema amevutiwa sana na mfumo wetu tunaoutumia ili kuhakikisha kuwa matangazo yetu yanawafikia wasikilizaji wetu popote pale wanapotusikiliza duniani. Pia anasema ushirikiano wetu katika utendaji wetu wa kazi na kwa wasikilizaji, unamfanya awe na furaha kubwa kiasi cha kumfanya atuandikie barua hii ya kuomba urafiki wa kubadilishana maoni, fikra na hata kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali ya kujenga na hasa ukilinganisha kuwa mimi yeye bado ni mwanafunzi, hivyo ni hitaji lake kuelewa mambo mengi ya kijamii na hasa yale yote yanayojenga.

Pia anasema ametumia fursa hii ya kutuandikia barua, hasa kwa kuzingatia uhusiano mzuri uliopo kati ya mataifa yetu haya mawili, yaani China na taifa la Tanzania. Mataifa haya yamekuwa katika uhusiano huo wa kihistoria kwa miaka mingi sana, hivyo ana imani na matumaini makubwa kuwa., kwa kuzingatia maelezo yake hapo juu atakubaliwa kuwa miongoni mwa marafiki wetu na wasikilizaji wetu katika bara hili la Afrika.

Sisi tunafurahi na kumkaribisha awe msikilizaji wetu na rafiki yetu, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza kwa makini vipindi vyetu, ama akipata nafasi atembelee tovuti yetu kwenye mtandao wa internet, asisahau anuani yetu ya www.cri.cn, chagua kiswahili utasoma makala mbalimbali na kusikiliza pia vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Ahkert Anaris wa sanduku la posta 2995 Kisii Kenya ametuletea barua akisema kuwa, kwanza anatupongeza kwa vipindi vyetu na matangazo yetu ya Radio China Kimataifa na anatuombea baraka njema kwa matangazo yetu, ingawa ni mwaka jana tu alianza kufuatilia matangazo yetu ya radio, sasa vipindi vya Radio China kimataifa kwake ni kama desturi, kwani anasikiliza mara mbili kwa wiki, na siku za jumapili wakati kwa kipindi cha sanduku la barua.

Anasema vilevile anatembelea tovuti ya idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa inayofunguka kwa haraka, na tofauti na tovuti nyingine alizotembelea, aliweza kusoma makala na pia kusikiliza vipindi vyote vilivyowekwa kwenye tovuti. Hapo Kisii hali ya mawasiliano bado si nzuri sana.

Anasema kutokana na kuwa kuitembelea tovuti ya idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa ni gharama, na nia yake ni kuifahamu zaidi China, ndio maana anasikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa na vipindi vyetu. Vilevile ana wanachama wengi wanaopenda matangazo yetu lakini hawana njia ya kuwasiliana nasi kwani gharama ya kutuma barua zimepanda mara dufu, kwa hivyo wanachama wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China wamepokea bahasha yenye stempu ili waendelee kuwasiliana nasi kwa njia iliyo rahisi kabisa. Anasema kwa kuwa yeye ana wanachama wengi wanaotaka kuwasiliana nasi lakini hawana njia, kwa hivyo wanaomba watumiwe bahasha nyingi pamoja na kadi za salamu. Hali kadhalika na kitabu ya historia ya Radio China kimataifa, orodha ya vipindi na gazeti la daraja la urafiki.

 

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-16