Askari elfu kadhaa wa Israel walianza operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu Wayahudi kutoka katika sehemu ya Gaza kuanzia saa sita usiku wa manane tarehe 17. Israel imetekeleza mpango wa upande mmoja wa kuondoka kutoka katika sehemu ya Gaza kuanzia tarehe 15. Kutokana na mpango wa serikali ya Israel, Wayahudi walioko katika sehemu ya Gaza lazima waondoke kabla ya saa sita alfajiri ya tarehe 17, ama sivyo polisi wa Israel watawaondoa kwa nguvu wakazi Wayahudi waliokuwa watakaong'ang'ania huko.
Tarehe 16 alasiri, polisi karibu elfu moja waliingia kwenye sehemu ya makazi ya Neveh Dekalim ambayo makazi makubwa kabisa kwenye sehemu ya Gaza na kuwashawishi Wayahudi hao waondoke haraka. Ofisa wa Israel alisema kuwa hadi tarehe 16 adhuhuri, familia 800 kati ya familia 1500 zilizoko katika sehemu ya Gaza zilikuwa tayari zimeondoka. Lakini familia 700 nyingine zilikuwa bado hazijaondoka. Polisi wa Israel walifanya maandalizi ya mwisho ya operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu.
Wakati huo huo, wapinzani wa shughuli za kuondoka waliendelea kupambana na askari polisi wa Israel. Huko Neveh Dekalim, polisi na askari mia kadhaa walivunja milango ya sehemu ya makazi. Ili kuwazuia polisi wasiingie kwenye sehemu hiyo ya makazi, baadhi ya Wayahudi vijana wanaopinga shughuli za kuondoka walitumia magurudumu na mapipa ya takataka kuzuia barabara na kuchoma moto mapipa hayo, na baadaye pande mbili zilipambana. Polisi waliwakamata Wayahudi vijana 50 walioshiriki kwenye mapambano hayo.
Zaidi ya hayo, katika sehemu ya Negev ya Israel inayokaribia sehemu ya Gaza, polisi waliwakamata Wayahudi 800 wenye msimamo mkali waliojaribu kuingia kwenye sehemu ya Gaza na kuzuia shughuli za kuondoka. Waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Shaul Mofaz tarehe 16 alisisitiza kuwa Israel itawadhibu watu wote wanaozuia shughuli za kuondoka.
Ingawa shughuli za kuondoka zinapingwa, lakini jeshi la Israel bado lina imani kwa kukamilisha mpango wa kuondoka bila vikwazo. Kamanda mwandamizi wa Israel alisema kuwa jeshi la Israel linatazamiwa kukamilisha shughuli za kuondoka kwa wakazi wa sehemu za makazi 21 huko Gaza ndani ya siku 10.
Kwa upande mwingine, kazi za kufanya uratibu kuhusu shughuli za kuondoka kati ya Israel na Palestina pia zinaendelea bila vikwazo. Vyombo vya habari vya Israel vinaeleza kuwa hadi tarehe 16, Palestina imewapanga askari elfu 11 wa jeshi la usalama kwenye sehemu ya kusini hadi kaskazini mwa Gaza, ili kuhakikisha mpango wa kuondoka Israel unatekelezwa vizuri. Jeshi la Israel lilieleza kuwa katika saa 24 zilizopita, makundi yenye silaha ya Palestina yalifanya mashambulizi matatu tu dhidi ya shabaha za Israel, ambapo ni mashambulizi machache kuliko yale ya zamani. Jambo hilo linaonesha kuwa Palestina imefanya juhudi zenye mafanikio ili kuyazuia makundi yenye silaha yasifanye mashambulizi.
Idhaa ya kiswahili 2005-08-17
|