Tarehe 19, wabunge wa Burundi watamteua rais wa nchi hiyo katika harakati za kumaliza mapigano ambayo yamesababisha vifo vya watu wapatao 300,000.
Kiongozi wa kundi la zamani la waasi la Wahutu-Forces for the Defence of Democracy (FDD), Bw. Pierre Nkurunziza amehakikishiwa ushindi kwa kuwa hana mpinzani. Bw. Nkurunziza mwenye umri wa miaka 41, alikuwa mhadhiri katika chuo kikuu.
Uteuzi wa tarehe 19 ni hatua ya mwisho katika uchaguzi wa kidemokrasia unaokusudia kumaliza mapigano na uhasama baina ya Wahutu wengi na Watutsi walio wachache ambao wamekuwa madarakani.
Wawakilishi wa FDD walishinda viti vya ubunge katika uchaguzi wa amani uliofanyika tarehe 15. Katika kampeni zake, FDD ilitangaza kufufua demokrasia na kuyahusisha makundi yote katika serikali. Bw. Carolyn Mcaskie anayesimamia shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Burundi alisema kuwa, hii ni siku ya historia. Wagombeaji wengine wamejiondoa na sasa Nkurunziza na uhakika wa kushinda, kwa sababu anaungwa mkono na wananchi wengi.
Wananchi wa Burundi waliochoshwa na mapigano walijitokeza kupiga kura ili kuimarisha amani. Ingawa uchaguzi wa urais ni hatua ya mwisho katika mpango wa amani usiotiwa saini huko Arusha nchini Tanzania mnamo mwaka 2000, wengi wanasema amani ya kuduma itafika mwaka 2010, wakati amabapo waburundi wenyewe watamchagua rais wao.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, wanaowawakilisha wananchi kumteua rais ni hatua ya kwanza ya kufikia demokrasia halisi.
Ingawa mapigano yamepungua, lakini bado kuna kundi la wahutu linaloshambulia wananchi na jeshi mara kwa mara. Hata hivyo, Burundi inaendelea kujijenga kama mfano wa nchi za Afrika inayotaka kutatua matatizo yake yenyewe. Kadhalika imeinua matumaini katika eneo la machafuko la Maziwa Makuu.
Vita hivyo vililipuka kwa mara ya kwanza mwaka 1993 watutsi wenye siasa kali walipomuua rais mhutu Melchior Ndadaye aliyeteuliwa kidemokrasia.
Wachunguzi wanasema kuwa, Bw. Nkurunziza atakabiliwa na matatizo chungu nzima yakiwemo ya kusawazisha mamlaka baina ya vyama vya kisiasa vya waHutu na waTutsi. Chini ya mkataba wa amani, serikali inapanga kuwapa wahutu asilimia 60 ya wahutu asilimia 40 bungeni.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-18
|