Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-18 21:19:20    
Israeli yatumia nguvu kutekeleza mpango wa vitendo

cri
    Askari polisi zaidi ya elfu 10 wa Israeli tarehe 17 waliingia kwenye makazi ya wayahudi ya sehemu ya Ghaza kuwaondoa kwa nguvu wakazi wayahudi waliong'ang'ania kubaki huko. Ingawa polisi hao walikutana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wakazi, lakini mpango wa kuondoa wakazi ulitekelezwa kama ulivyopangwa. Baadhi ya wakazi waliohamishwa kutoka huko, hivi sasa wanaishi kwenye makazi waliyopangiwa nchini Israeli.

    Wayahudi wanaoishi katika makazi ya Neveh Dekalim ambacho ni kitovu cha makazi ya wayahudi walioko katika sehemu ya Ghaza, walikuwa wa kwanza kukumbwa na mpango wa kuwaondoa kwa nguvu tarehe 17. Watu wa ukoo wa Woody Dorain walioishi huko Dekalim kwa miaka 19, tarehe 17 waliendelea kugoma kuondoka. Siku hiyo usiku askari polisi wa Israel waliingia kwa nguvu majumbani mwao na kuwaburura nje mmoja baada ya mwingine, ambapo samani zao pamoja na vitu vingine vyao vilipakiwa kwenye makontena. Askari polisi walisema kuwa watu wa ukoo huo hawatarudishiwa mali zao, kama hawataahidi kutorudi kwenye makazi yao.

    Licha ya hayo, askari polisi waliwakamata mamia ya waisraeli waliojipenyeza kwenye sehemu ya Ghaza wakiwa na lengo la kuzuia utekelezaji wa mpango wa kuwaondoa wakazi wa huko. Tarehe 17 kwenye kituo cha ukaguzi cha Kissufim kilichoko katika njia ya kuelekea Ghaza, kulikuwa na wakazi na walalamikaji waliokamatwa ambao walisafirishwa kwa mabasi kutoka sehemu ya Ghaza. Kijana mmoja wa kiyahudi alipaaza sauti kwenye dirisha la basi, akisema, "Wanafukuza wakazi wote wa huko, wanataka kurudisha Ghaza kwa wapalestina, serikali kwa nini inatufanyia hivyo?"

    Askari polisi wa Israel walipotekeleza amri ya kuondoa wakazi walipingwa vikali na baadhi ya wakazi wa huko ambao waliwatupia chupa za maji, mayai na vitu vingine, na askari mmoja mwanamke alijeruhiwa kwa kuchomwa kisu. Mbele ya upinzani wa wakazi, askari hao walichukua msimamo thabiti na kujizuia. Tarehe 17 askari walikuwa wakijaribu kuwaondoa walimu na watoto wa shule moja ya chekechea, askari walisimama kimya nje ya mlango wa shule hiyo na walitekeleza amri baada ya watoto wale kuamka katika usingizini. Mkuu wa jeshi wa sehemu ya kusini ya Israeli Uri Barlev alisema, "Askari walikuwa na shida sana, tunatarajia wakazi hao hatimaye watatambua kuwa sisi tuko katika taifa moja."

    Msimamo thabiti wa serikali ya Israeli umefanya wakazi wengi wa huko kutambua hali halisi ilivyo. Hadi tarehe 17 usiku, familia kiasi cha 1,000 kati ya familia 1,500 za huko zilihama huko, wakazi walioko katika baadhi ya makazi mengine waliomba polisi kuwapa muda mwingi zaidi ili wajiandae na kuondoka. Katika sehemu ya Nitzanim, kilomita 30 kaskazini mwa Ghaza, wakazi wa familia zaidi ya 250 wanaishi katika makazi ya muda waliyopangiwa na serikali. Ofisa msimamizi wa sehemu hiyo Arik Eldar alisema kuwa kijiografia, sehemu ile ni moja ya sehemu nzuri sana nchini Israeli, ambapo mtu akiendesha gari lake anaweza kufika Tel Aviv, ambayo ni mji wa kwanza kwa ukubwa kwa shughuli za biashara, kwa dakika 20 tu, na wanaweza kufika kando ya bahari ya Mediterranean kwa dakika chache tu, huko hakuna maroketi ya aina ya Qassam na ni salama kabisa.

    Mwanamke wa kiyahudi mwenye umri wa miaka zaidi ya 40 aliyejulikana kwa Maza Hadad, tarehe 16 aliondoka kutoka kwenye nyumba yake iliyoko katika sehemu ya kaskazini ya Ghaza na kuhamia kwenye nyumba moja ya muda yenye mita za mraba 90 hivi iliyoko katika sehemu ya Nitzanim. Alisema kuwa alihamia huko kutokana na kuwa marafiki zake wengi wanaishi huko, sasa hawana chaguo ila tu kuanza mapema maisha mapya, kwani wakihamia huko mapema watanufaika zaidi."

    Ingawa Hadad ana mashaka makubwa kwa kuanza maisha mapya ugenini, lakini alifahamu kuwa kuhama siyo kuangamia, maisha yataendelea.

Idhaa ya Kiswahili