Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-22 10:43:52    
Wananchi wa China waadhimisha miaka 60 ya ushindi wa vita vya kupambana na wavamizi wa Japan

cri

Tarehe 15 Agosti, ni siku ya kuadhimisha mwaka wa 60 tangu watu wa China kupata ushindi wa vita dhidi ya uvamizi wa Japan. Siku hizi wananchi wa China wanaadhimisha siku hiyo kwa njia mbalimbali.

Tarehe 7 Julai, mwaka 1937 jeshi la Japan kwa ujeuri lilishambulia jeshi la China katika daraja la Lugou, kusini magharibi mwa Beijing. Tokea hapo Japan ilianza kuivamia China kwa pande zote, na vita vya wananchi wa China kupambana na wavamizi wa Japani pia vilianza. Tarehe 15 Agosti mwaka 1945, Japan ilisalimu amri bila masharti yoyote. Watu wa China walipopambana kwa miaka minane walipata ushindi kwenye vita hivyo.

Ili kuikumbuka historia hiyo isiyosahaulika ya taifa la China, tarehe 7 Julai, maonesho makubwa ya maadhimisho ya vita dhidi wavamizi wa Japan yalianza kufanyika katika jumba la makumbusho lililoko karibu na daraja la Lugou. Maonesho hayo yameonesha watu wa China jinsi walivyoungana na kupambana na wavamizi kufa na kupona na hatimaye waliupata ushindi mkubwa katika vita hivyo. Kwenye maonesho hayo vitu zaidi ya 800 na picha zaidi ya 600 pamoja na nyaraka nyingi zinaoneshwa, kati ya vitu hivyo vitu 140 vinaoneshwa kwa mara ya kwanza. Mkuu wa jumba hilo Bw. Li Zongyuan alieleza, "Maonesho haya ni makubwa kati ya shughuli nyingi za maadhimisho ya ushindi wa miaka 60 wa vita vya watu wa China dhidi ya wavamizi wa Japan na ufashisti duniani. Lengo lake ni kuonesha kuwa taifa la China liliposhambuliwa wananchi wa China walivyoungana pamoja kama kitu kimoja katika mapambano ya kulikomboa taifa na hatimaye walipata ushindi. Huu ni ushindi mkubwa katika historia ya China, ni ushindi wa kuondoa fedheha ya taifa kwa damu zetu."

Inasemekana kwamba katika mwezi mmoja uliopita watu waliotazama maonesho hayo kutoka nchini na nchi za nje wamefikia zaidi ya laki nne. Mtazamaji Guo Linda kwa makusudi alimchukua mtoto wake kutoka mkoa wa mbali wa Hunan kuja kutazama maonesho hayo, alisema, "Nimemchukua mtoto wangu kwa makusudi kuja kuangalia maonesho, ili ajifunze uzalendo. Ni wajibu wangu kumfahamisha historia yetu iliyoonewa na awe na juhudi katika masomo yake."

Ili kuadhimisha miaka 60 ya ushindi wa vita dhidi ya wavamizi wa Japan, filamu nyingi mpya zinaoneshawa. Kati ya filamu hizo, filamu ya "Kwa ajili ya Ushindi" ni filamu iliyotengenezwa kwa nyaraka nyingi za historia, imeonesha ushupavu wa wananchi na wanajeshi walivyopambana na wavamizi. Filamu ya "Askari Mdogo Zhang Ga" ilitengenezwa kwa picha za katuni ikionesha hadithi inayojulikana kwa watu wengi, askari mdogo Zhang Ga jinsi alivyopambana na wavamizi wa Japan kwa ujanja. Filamu kama hizo zinaoneshwa televisheni. Mchezo wenye sehemu 25 wa TV unaoitwa "Jeshi la Njia ya Nane" kwa pande zote umeonesha jinsi Jeshi la Njia ya Nane lililoongozwa na majemadari wakuu wa Chama cha Kikomunisti cha China Zu De na Peng Dehuai, lilivyopambana na wavamizi wa Japan kwa nia imara na kumwaga damu, na kukomboa sehemu kubwa ya China, na hivyo lilitoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya wavamizi wa Japan na ufashisti duniani. Bw. Li Jingsheng aliyesimamia utengenezaji wa mchezo huo alisema, "Huu ni mchezo wa ushupavu, umeonesha vilivyo Chama cha Kikomunisti cha China kilivyokuwa nguzo katika mapambano dhidi ya wavamizi wa Japan, umeenzi moyo wa uzalendo. Hii ndiyo mada ya maadhimisho ya ushindi wa miaka 60 ya vita dhidi ya wavamizi wa Japan."

Katika michezo ya sanaa, opera mpya ya Kibeijing ya "Kijana Yang Jingyu" inaoneshwa siku hizi, opera hiyo inaonesha jinsi kijana alivyopambana na wavamizi wa Japan. Yang Jingyu alikuwa jemadari wa jeshi la kaskazini mashariki mwa China, askari wake wote walipokuwa wamekufa alibaki peke yake na kupambana na askari wa Japan mpaka risasi ya mwisho. Kwa ukatili askari wa Japan walimkata kichwa na kupasua tumbo lake, wakagundua kuwa ndani ya tumbo lake hakukuwa na chakula hata chembe, ila magome ya mti na pamba. Opera nyingine ya "Alizeti", ikieleza kuwa mkulima mwanamke Fang Dagu aliyegundua kuwa mwanawe alikuwa msaliti na kuongoza askari wa Japan kuwaua wapiganaji wazalendo alimwua mtoto wake. Opera ya wimbo uliotungwa kwa mujibu wa hadithi ya kusisimua, kwamba wapiganaji wanawake wanane wasiokubali kusalim amri mwishowe wajiua kwa kujitupa mtoni. Mwezi Oktoba, mwaka 1938 wapiganaji wanawake wanane walipoishiwa risasi katika mapambano na askari wa Japan, wote walijiua kwa kujitupa mtoni badala kusalim amri. Mwongozaji wa opera hiyo Bi. Li Daocuan alisema, "Kabla ya hapo tulikuwa hatuna opera ya kuonesha vita dhidi ya uvamizi wa Japan. Natunga opera hiyo kwa sababu hadithi hiyo inanisisimua kwa ushupavu wa wapiganaji hao, naona wanastahili kusifiwa kutokana na kujitoa mhanga kwa taifa lao. Moyo wao ndio moyo wa taifa la China."

Katika mji wa Xiamen kwaya 60 zenye waimbaji 3500 zilifanya maonesho ya nyimbo kuhusu mapambano dhidi ya wavamizi wa Japan.

Usemi wa Kichina unasema kuwa "mafunzo ya zamani yawe mwongozo wa siku za baadaye". Historia ikumbukwe, na amani ithaminiwe.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-22