Shughuli za Israel kuondoa makazi ya Wayahudi yaliyoko kwenye sehemu ya Gaza, tarehe 21 zilikaribia kukamilika. Hadi siku hiyo, makazi 20 kati ya makazi yote 21 yalikuwa tayari yameondolewa. Shughuli za kuondoa makazi hayo zilifanyika bila vikwazo na bila matarajio ya watu.
Polisi elfu kumi kadhaa wa Israel tarehe 15 walikwenda kwenye sehemu ya Gaza kutekeleza rasmi mpango wa upande mmoja wa kuondoa makazi ya Wayahudi yaliyoko kwenye sehemu ya Gaza na kando ya magharibi ya mto Jordan. Mpango huo ulisusiwa na baadhi ya wakazi hao, lakini polisi wa Israel walidhibiti hali hiyo kwa hatua mwafaka na kuepusha migogoro mikubwa isitokee. Katika muda usiotimia wiki moja, asilimia 95 ya makazi hayo yameondolewa.
Vyombo vya habari vinaona kuwa, shughuli za kuondoa makazi hayo zilifanyika haraka kutokana na mambo kadhaa yafuatayo.
Kwanza, shughuli za kuondoa makazi ziliandaliwa ipasavyo. Polisi wa Israel walianza kufanya mazoezi mwezi mmoja kabla ya kuanza shughuli hizo. Katika mchakato wa kuondoa makazi, polisi hao waliwapa wakazi siku mbili za kuamua kuondoka kwa hiari, la sivyo wataondolewa kwa nguvu. Baada ya kutofanikiwa kuwashawishi wakazi hao, polisi walichukua hatua madhubuti na kutowapa wakazi mawazo ya kubaki kwenye makazi hayo. Hatua hizo zilipunguza migongano kati ya polisi na wakazi na kuepusha kwa hatua mwafaka migogoro inayoweza kusababisha umwagikaji wa damu isitokee.
Pili, hatua za serikali ya Israel kuwapangia wakazi wanaohamia ni nzuri. Kila mkazi anafidiwa dola za kimarekani laki 3 hadi haki 5. Zaidi ya hayo, serikali imegharimia fedha nyingi kuwajengea wakazi nyumba za muda. Hatua hizo zimeondoa wasiwasi kwa wakazi wakataohamia makazi mapya.
Tatu, mwaka mmoja tangu mpango wa upande mmoja ulipotolewa, serikali ya Sharon ilifanya kampeni kubwa za kuondoa makazi hayo na kuwashawishi wakazi wapokee ukweli wa mambo. Kabla ya kufanya shughuli za kuondoa makazi, ingawa bado kulikuwa na asilimia 50 ya wakazi ambao walikataa kuondoka kwa hiari, lakini wengi wao waliona kuwa shughuli hizo zitafanywa bila kujali nia yao na kukataa kuondoka kwa hiari ni kwa ajili ya kueleza msimamo wao wa upinzani.
Wakati huo huo, shughuli za Israel kuondoa makazi ya Wayahudi zilipata ushirikiano mzuri kutoka upande wa Palestina. Askari elfu kadhaa wa jeshi la usalama la Palestina walipangwa nje ya makazi ya Wayahudi yaliyoko kwenye sehemu ya Gaza kuanzia tarehe 14, ili kuwazuia watu wenye silaha wa Palestina wasishambulie shabaha za Israel katika kipindi cha kuwaondoa wakazi. Mamlaka ya Palestina na kundi la upinzani la kiislamu la Palestina Hamas pia zilikubali kuweka kando tofauti zao na kuunda tume ya pamoja, ili kusimamia shughuli za kuondoa makazi ya wayahudi.
Hadi hivi sasa makazi pekee ambayo bado hayajaondolewa kutoka katika sehemu ya Gaza, ilifikia makubaliano na polisi wa Israel na kuamua kuondoka huko tarehe 22. Historia ya Wayahudi kukaa kwenye sehemu ya Gaza itaisha. Baada ya mwezi mmoja hivi, Israel itakabidhi sehemu ya Gaza kwa Palestina.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-22
|