Baada ya wakazi wa Israel kuondoka kutoka kwenye ukanda wa Gaza, udhibiti wa mamlaka ya taifa ya Palestina kwenye ukanda wa Gaza unakabiliwa changamoto kali ya chama cha upinzani cha kiislamu cha Palestina (Hamas) ambacho ni kundi la kijeshi lenye nguvu kubwa kabisa katika sehemu hiyo.
Kuondoka kwa Israel kumeleta nafasi nzuri sana kwa mamlaka ya utawala wa Palestina kujenga madaraka yake kwenye ukanda wa Gaza. Israel itaikabidhi mamlaka ya utawala wa Palestina ardhi ya ukanda huo na jumuiya ya kimataifa, pia imeahidi kutoa misaada mingi ya fedha kwa ujenzi wa kanda ya Gaza. Mambo hayo yataimarisha hadhi ya mamlaka ya taifa ya Palestina inayoongozwa na Abbas katika ukanda wa Gaza na kudhoofisha athari ya chama cha Hamas katika ukanda huo.
Lakini Hamas hairidhiki na mambo hayo. Kabla na baada ya Israeli kuondoka kanda ya Gaza, Hamas iliitisha maandamano kadhaa makubwa katika ukanda wa Gaza na kuonesha nguvu zake za kijeshi na kisiasa wakati wa kusherehekea kuondoka kwa Israel. Siku chache zlizopita, kiongozi wa Hamas alitoa taarifa mara kwa mara akisema kuwa, kuondoka kwa Israel ni matokeo ya mapambano ya watu wa Palestina, na Hamas itaendelea na mapambano hadi Jerusalem itakapokombolewa na eneo lote la kando ya magharibi ya mto Jordan. Msemaji wa Hamas Abu Sami Zuhri tarehe 22 katika tovuti alitangaza kuwa katika muda wa miaka 5 toka kuzuka mapambano mapya kati ya Palestina na Israel mwezi Septemba mwaka 2000 hadi Israel kuondoka kutoka kanda ya Gaza tarehe 15 mwezi Agosti, shabaha za Israel katika kwenye ukanda wa Gaza zimeshambuliwa mara zaidi ya 400 na zaidi 54% ya mashambulizi hayo yalifanywa na Hamas. Bw Zuhri alisema kuwa hesabu hiyo inaonesha kuwa Hamas ilifanya kazi muhimu sana katika kuondoka kwa Israel. Vyombo vya habari vinafanya uchambuzi kuwa maneno na vitendo vya Hamas vya hivi karibuni vinaonesha kuwa Hamas inagombea udhibiti wa ukanda wa Gaza na mamlaka ya taifa ya Palestina.
Asilimia 65 ya wakazi milioni 1.5 wa Gaza ni wakimbizi wa Palestina kutokana na vita kati ya Palestina na Israel, na ukosefu wa ajira katika ukanda huo imefikia 45%. Vita na umaskini wa miaka mingi vimechangia maendeleo ya chama chenye siasa kali cha Hamas. Katika miaka mingi iliyopita licha ya kushikilia mapigano ya kisilaha, Hamas pia ilianzisha asasi za kutoa msaada kwa watu maskini, ili kupata uungaji mkono wa umma. Upigaji kura za maoni ya watu uliofanywa unaonesha kuwa 41% ya watu wa Gaza wanaiunga mkono Hamas.
Ushindani wa Hamas kuhusu mamlaka ya kanda ya Gaza ulipingwa kithabiti na mamlaka ya taifa ya Palestina. Kabla ya Israel kuanza kuondoka Gaza, Hamas ilipendekeza kuanzisha kamati ya pamoja inayoshirikiwa na makundi mbalimbali ya kisiasa ya Palestina ili kutawala kwa pamoja ukanda wa Gaza baada ya Iarael kuondoka kutoka sehemu hiyo. Lakini mamlaka ya taifa la Palestina ilieleza wazi kuwa serikali ya mamlaka ya taifa ya Palestina ni serikali pekee katika ukanda wa Gaza, pendekezo la Hamas ni kujaribu kuanzisha serikali nyingine. Mwenyekiti wa mamlaka ya taifa ya Palestina Bw Mahmood Abbas tarehe 20 alisaini amri kuwa ardhi na mali zilizoachwa baada ya Israel kuondoka Gaza zitasimamiwa na serikali ya mamlaka ya Palestina.
Tokea mwishoni mwa mwaka uliopita Hamas ilijibadilisha hatua kwa hatua na kuwa chama cha kisiasa na kushiriki kwenye mchakato wa kisiasa wa Palestina. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa Palestina ulioanza mwishoni mwa mwaka uliopita, wanachama wa Hamas walishinda na kunyakua karibu nusu ya madaraka ya ukanda wa Gaza. Hamas iliyonufaika katika mambo ya siasa hivi sasa, inatumia zaidi mbinu ya kisiasa na kutoa shinikizo la kisiasa dhidi ya mamlaka ya Palestina na kujiandaa kushiriki kwenye uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria ya Palestina utakaofanyika mwezi Januari mwakani.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-23
|