Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-23 20:14:22    
Mkutano wa Shirika la afya duniani wafuatilia suala la afya Barani Afrika

cri

Mkutano wa 55 wa kamati ya sehemu ya Afrika ya Shirika la afya duniani WHO, ulifunguliwa tarehe 22 huko Maputo, mji mkuu wa Msumbiji. Mawaziri wa afya na wawakilishi wao kutoka nchi wanachama wa WHO, wajumbe wa mashirika ya pande nyingi na pande mbili na jumuiya zisizo za kiserikali wapatao mia kadhaa wamehudhuria mkutano huo.

Kwenye mkutano huo wa siku 5, wajumbe wanaohudhuria mkutano huo watajadili masuala kuhusu kinga na udhibiti wa magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu na malaria, namna ya kutekeleza "mkataba wa udhibiti wa tumbaku", mzunguko wa wataalamu wa afya na madaktari wa sehemu ya Afrika. Katibu mkuu wa Shirika la WHO Bwana Lee Jong Wook alitoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano akidhihirisha kuwa, kila mwaka barani Afrika zaidi ya watu millioni moja hufa kwa sababu ya magonjwa ya ukimwi, homa ya damu ya Marburg, malaria, kifua kikuu, kipindupindu na surua, hali hii imeathiri vibaya juhudi za nchi mbalimbali za Afrika katika kutafuta maendeleo. Ili kusaidia Bara la Afrika kutibu magonjwa ya aina mbalimbali, Bwana Lee Jong Wook alitangaza kuwa, shirika la afya duniani litaongeza asilimia 30 ya bajeti yake kwa sehemu ya Afrika.

Katika muda mrefu uliopita, maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi yalikuwa mabaya zaidi barani Afrika, ugonjwa huo umekuwa tishio kubwa kabisa dhidi ya afya ya wananchi wa Afrika. Rais Armando Guebuza wa Msumbiji alipotoa hotuba kwenye mkutano huo alisisitiza kuwa, maambukizi mabaya ya ugonjwa wa ukimwi barani Afrika yameathiri vibaya afya ya nguvukazi ya nchi mbalimbali za Afrika na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya watu, hii imekuwa sababu moja kubwa ya kulifanya ongezeko la uchumi wa Bara la Afrika liwe la polepole .

Mbali na suala la ugonjwa wa ukimwi, hali ya magonjwa ya kifua kikuu, ukoma na surua pia ni mbaya katika nchi za Afrika, hata kiwango cha vifo vya watoto wachanga na kina mama vya sehemu hiyo pia ni cha juu zaidi kuliko sehemu nyingine duniani. Na sababu kubwa ya kuleta hali hiyo ya wasiwasi juu ya afya ya wananchi wa Afrika ni ukosefu wa wataalamu wa afya na madaktari, uhaba wa fedha na ukosefu wa teknolojia. Kwa upande mmoja, nchi nyingi za Afrika zina matatizo ya kiuchumi, ni vigumu kwao kutoa huduma za lazima za matibabu kwa wananchi wao. Wakati huo huo, hali ya kupoteza wataalamu wa afya na madaktari katika nchi za Afrika pia ni mbaya sana, na kuzifanya nchi za Afrika ziwe na ukosefu mkubwa wa madaktari na wauguzi. Kwa mfano nchi ya Lesotho ya kusini mwa Afrika ina idadi ya watu milioni 1.5, lakini ina wauguzi zaidi ya 200 tu nchini humo ambao wanaweza kufanya matibabu ya ugonjwa wa ukimwi. Lakini madaktari na wauguzi wenye asili ya kiafrika wanaofanya kazi katika nchi za magharibi wamefikia milioni 3.

Vyombo vya habari vinaona kuwa, mkutano huo si kama tu umetoa fursa ya kubadilishana maoni kwa nchi mbalimbali za Afrika kuhusu changamoto ya suala la afya inayoikabili kila nchi ya Afrika, pia mkutano huo umeleta fursa kwa nchi za Afrika kupata ufuatiliaji na uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa kwa suala la afya la Bara la Afrika. Watu wanatarajia kuwa mkutano huo utaweza kuzihimiza serikali za nchi mbalimbali za Afrika, jumuiya zisizo za kiserikali na jumuiya nzima ya kimataifa, zifanye juhudi kubwa zaidi kwa kutatua suala la afya la Afrika, ili kusaidia kutimiza lengo la maendeleo ya milenia la kupunguza kwa nusu idadi ya watu maskini barani Afrika ifikapo mwaka 2015.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-23