Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-24 21:18:54    
Mswada wa katiba mpya ya Iraq wakabiliwa na hatari ya kutofanikiwa

cri

Usiku wa manane wa tarehe 22 kwa saa za Iraq, Bunge la mpito la Iraq lilipokea mswada wa katiba mpya ulioungwa mkono na madhehebu ya Shia na Wakurd. Kutokana na mswada huo kutokubaliwa na madhehebu ya Sunni, bunge la mpito halikuupigia kura mswada huo, bali kuamua kutoa siku tatu nyingine za kufanya majadiliano zaidi, ili katiba hiyo mpya ikubaliwe na makundi mbalimbali.

Wachambuzi wana wasiwasi kuwa, tarehe ya kupitisha mswada wa katiba mpya imeahirishwa mara kwa mara, na mswada huo unakabiliwa na hatari ya kuharibika.

Kutokana na katiba ya muda ya Iraq, kamati ya utungaji wa katiba ya Iraq ilipaswa kulikabidhi bunge la mpito mswada wa katiba kabla ya tarehe 15 Agosti, ili uweze kupigiwa kura za maoni ya raia kabla ya tarehe 15 Oktoba, na kufanya uchaguzi mkuu kutokana na utaratibu wa katiba mpya mwezi Desemba mwaka huu. Kutokana na kwamba, waarabu wa madhehebu ya Shia, Wakurd na madhehebu ya Sunni walikuwa na maoni tofauti kuhusu mambo kadhaa makubwa yaliyomo ya katiba hiyo, hivyo bunge la mpito tarehe 15 lilipaswa kuahirisha tarehe ya mwisho ya kukabidhi mswada wa katiba mpya hadi tarehe 22. Hivi sasa tofauti kubwa kati ya makundi mbalimbali ni mfumo wa shirikisho, jina la chama cha Arab Baath Socialist Party, na madaraka ya rais, bunge na baraza la mawaziri. Tarehe 23, makundi mbalimbali yalifanya majadiliano ya dharura ili kupunguza tofauti zao. Lakini wachambuzi wanaona kuwa, kutokana na tofauti kubwa kuhusu suala la mfumo wa shirikisho, ni vigumu kwao kuafikiana katika muda mfupi.

Madhehebu ya Shia na Wakurd wanatetea kuandika wazi kwenye katiba kanuni ya kufuata mfumo wa shirikisho nchini Iraq, lakini madhehebu ya Sunni yanachukulia kuwa, kufanya hivyo kutaifarakanisha Iraq. Madhehebu ya Sunni yana wasiwasi kuwa, baada ya kufuata mfumo wa shirikisho, sehemu za kusini na kaskazini zenye maliasili nyingi za mafuta zitadhibitiwa na madhehebu ya Shia na Wakurd, kwa sababu sehemu inayodhibitiwa na madhehebu ya Sunni ni sehemu ya jangwa isiyokuwa na maliasili, hivyo sehemu hiyo itakumbwa na umaskini na vurugu wa kivita siku zijazo. Hivyo madhehebu ya Shia yanatetea kithabiti kufuata mfumo wa serikali kuu, ili kudhibiti kwa ufanisi maliasili za mafuta na kugawana mali za nchi hiyo kwa uhalali.

Pengine, tofauti kati ya Wakurd na madhehebu ya Shia bado haijatatuliwa. Wakurd wanashikilia kuongeza madaraka ya kujiendesha, kushikilia kutunga katiba ya kimila na kadhalika. Maoni ya Wakurd hayataungwa mkono na madhehebu ya Shia na Sunni. Na madhehebu ya Shia pia hayatalegeza msimamo wake kuhusu suala la umuhimu wa dini ya kiislamu katika maisha ya kisiasa ya nchi hiyo.

Wachambuzi wameainisha kuwa, ikiwa mswada wa katiba hauwezi kuungwa mkono na madhehebu ya Sunni, hata kama bunge la mpito litaweza kupitisha mswada huo siku mbili baadaye, lakini utasusiwa na madhehebu ya Sunni kwenye upigaji kura za maoni ya raia katikati ya mwezi Oktoba., hivyo katiba rasmi bado inakabiliwa na hatari ya kuharibika.

Kwa mujibu wa katiba ya muda ya Iraq, mswada wa katiba rasmi utapitishwa kwenye bunge ukipata kura za ndiyo za theluthi mbili ya wabunge 275, madhehebu ya Shia na Wakurd wanachukua viti 215 bungeni, hivyo wanaweza kuhakikisha mswada huo unapitishwa bila uungaji mkono wa madhehebu ya Sunni. Lakini katiba ya muda pia ilisema kuwa, katika upigaji kura za maoni ya raia unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, ikiwa theluthi mbili ya wapiga kura wa mikoa mitatu kati ya mikoa 18 nchini Iraq wanapiga kura za hapana, basi katiba hiyo haitapitishwa. Na waarabu wa madhehebu ya Sunni wanachukua kiasi kikubwa katika mikoa zaidi ya mitatu, hivyo kura zao zitafanya umuhimu mkubwa katika upigaji kura za maoni ya raia.

Tarehe 21, elfu kadhaa ya wapiga kura wa madhehebu ya Sunni waishio mjini Fallujah walijiandikisha kushiriki kwenye upigaji kura za maoni ya raia utakaofanyika mwezi Oktoba, na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Desemba. Wachambuzi wanaona kuwa, jambo hilo limeonesha kuwa, watu wa madhehebu ya Sunni wako tayari kupinga mswada wa katiba rasmi ambao haukubaliki.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-24