Tarehe 23 usiku, mpango wa upande mmoja wa Israel wa kuwaondoa walowezi wayahudi kutoka kwenye ukanda wa Gaza na kaskazini ya sehemu ya magharibi wa mto Jordan ulimalizika kimsingi. Vyombo vya habari vinasema kuwa, utekelezaji wa mpango huo umetoa fursa nzuri kwa kuanzisha tena mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, lakini mustakabali wa hali ya Palestina na Israel bado unakabiliwa na mabadiliko yasiyojulikana.
Jeshi la Israel limekadiria kuwa, wanajeshi wa Israel walioko katika ukanda wa Gaza wote wataondoka kutoka sehemu hiyo kabla ya mwishoni mwa Septemba. Hii inamaanisha kuwa, ukaliaji wa Israel kwenye ukanda wa Gaza uliodumu kwa miaka 38 umekomeshwa kimsingi, ambapo Palestina itakabidhiwa mamlaka ya sehemu hiyo. Japokuwa pande hizo mbili bado zina tofauti kuhusu udhibiti wa mawasiliano ya barabarani, baharini na angani wa ukanda wa Gaza siku zijazo, lakini kuondoka kwa Israel kumeiwezesha Palestina kushughulikia na kujenga upya ukanda wa Gaza.
Kutokana na kuwekewa vikwazo na Israel kwa kipindi kirefu, uchumi wa ukanda wa Gaza uko nyuma sana, wakazi wanaishi maisha duni sana, na kusababisha hali ya kuweko kwa makundi mbalimbali yenye siasa kali, madaraka na heshima ya mamlaka ya utawala wa Palestina yatakabiliwa na changamoto kubwa. Hivyo jukumu la kwanza kwa mamlaka ya utawala wa Palestina, ni kusawazisha migongano kati yake na vikundi hivyo vya wanamgambo, kukabidhiwa madaraka ya kuutawala ukanda wa Gaza kwa mafanikio, kufufua utaratibu wa kisheria, kukarabati na kustawisha uchumi, kuhakikisha usalama wa wakazi na kutoa nafasi za ajira. Ikiwa nchi muhimu iliyoelekeza mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, Marekani imeanza kuiwekea shinikizo mamlaka ya utawala wa Palestina. Rais Bush tarehe 23 alisema kuwa, baada ya Israel kuondoka kutoka kwenye ukanda wa Gaza, mamlaka ya utawala wa Palestina inatakiwa kwanza kuanzisha serikali yenye nguvu na heshima kwenye sehemu hiyo, ama sivyo mchakato wa amani ya sehemu hiyo hautaweza kupata maendeleo.
Lakini bado haijajulikana kuwaIsrael itaendelea kuondoka kutoka kwenye ardhi zilizokaliwa za Palestina za sehemu ya magharibi ya mto Jordan kama inavyotarajiwa na Palestina na jumuiya ya kimataifa. Mwaka kesho Israel itafanya uchaguzi mkuu, waziri mkuu wa nchi hiyo Bwana Sharon amewapa picha mbaya wapiga kura wengi wenye mrengo wa kulia kutokana na kutekeleza mpango wa kuchukua vitendo kwa upande mmoja. Ili kubadilisha hali hiyo, hivi karibuni alisema kuwa, Israel haitakuwa na mpango wa pili wa kuondoa jeshi. Msimamo huo wa Sharon umetia mashaka kwa mustakabali wa mchakato ya amani wa Palestina na Israel.
Palestina ina wasiwasi kuwa, Israel itaimarisha udhibiti wa vituo vikubwa vya makazi ya wayahudi vilivyoko kando ya magharibi ya mto Jordan, ili kuzuia juhudi za kuanzisha nchi ya Palestina. Vyombo vya habari vya Israel vinasema kuwa, wakati utekelezaji wa mpango wa upande mmoja ulipokaribia kumalizika, idara husika za kisiasa na kijeshi za Israel zimetoa amri ya kuchukua ardhi kwa ajili ya kujenga ukuta wa utenganishaji kwenye kituo cha Ma'aleh Adumim, ambacho ni kituo kikubwa kabisa cha wayahudi katika sehemu hiyo. Ukuta huo utatenganisha Jerusalem na kando ya magharibi ya mto Jordan, kugawanya sehemu ya magharibi ya mto Jordan, na kuharibu vibaya ukamilifu wa ardhi wa Palestina.
Vyombo vya habari vimeona kuwa, pande hizo mbili zilishirikiana vizuri wakati Israel ilipotekeleza mpango wake wa upande mmoja, na kuhimiza uaminifu kati yao, na kuweka msingi mzuri kwa kuanzisha tena mchakato wa amani. Lakini wachambuzi wameainisha kuwa, baada ya Israel kuondoka kutoka kwenye ukanda wa Gaza, Israel itaweza kurudi nyuma au la kuhusu ujenzi wa ukuta wa utenganishaji, hadhi ya Jerusalem, na suala la wakimbizi wa Palestina bado ni sababu muhimu za kuamua mwelekeo wa mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-25
|