Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-25 20:53:01    
Marekani yalegeza kwa kiasi fulani msimamo wake kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea

cri

Duru la 4 la mazungumzo ya pande 6 kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea linatazamiwa kuendelea ndani ya wiki moja itakayoanzia tarehe 29 mwezi huu. Wakati siku ya kufufua kwa mazungumzo hayo inapokaribia, pande mbalimbali zinazohusika zinafanya juhudi kubwa na mawasiliano ya kidiplomasia ya mara kwa mara.

Hali inayofuatiliwa zaidi ni kuwa hivi karibuni Korea ya kaskazini na Marekani zilifanya mawasiliano mara kwa mara ambapo Marekani imeonesha msimamo wake wenye unyumbufu kuhusu Korea ya kaskazini kutumia kiamani nishati ya nyuklia. Wachambuzi wanaona kuwa mabadiliko hayo huenda yatakuwa msingi wa kupatikana kwa maendeleo katika mazungumzo ya pande 6.

Baada ya kumalizika kwa mkutano wa kipindi cha kwanza cha duru la 4 la mazungumzo ya pande 6, suala kuhusu Korea ya kaskazini kuweza kuwa na haki ya kutumia kiamani nishati ya nyuklia au la, limekuwa suala lenye mabishano makubwa kati ya Marekani na Korea ya kaskazini. Marekani inaitaka Korea ya kaskazini iache miradi yote ya nyuklia ikiwemo miradi ya kutumia kiamani nishati ya nyuklia, lakini Korea ya kaskazini inaona kuwa kutumia kiamani nishati ya nyuklia ni haki inayostahili kwake ambayo imewekwa kwenye sheria ya kimataifa. Mgongano huo ni suala kubwa kabisa lililolifanya duru la 4 la mazungumzo ya pande 6 kutopata maendeleo. Ili kuondoa kikwazo hicho, Korea ya kaskazini na Marekani wiki iliyopita na wiki hii zilifanya mawasiliano mara tatu kwa kupitia "njia ya New York". Mbali na Korea ya kaskazini na Marekani, pande nyingine za China, Korea ya kusini, Japan na Marekani pia zilifanya mawasiliano ya pande mbili mbili, na kuweka mazingira yenye juhudi kwa mkutano wa kipindi cha pili wa duru la 4 la mazungumzo ya pande 6.

Na ufanisi wa juhudi hizo umeonekana kwa hatua ya mwanzo. Tarehe 23, mwakilishi wa kwanza wa Marekani katika mazungumzo ya pande 6 ambaye pia ni msaidizi wa waziri wa mambo ya nje Bwana Christopher Hill alisema kuwa, kwenye mkutano wa kipindi cha pili, huenda Marekani itachukua msimamo wenye unyumbufu kuhusu kuiruhusu au la Korea ya kaskazini kutumia kiamani nishati ya nyuklia. Alidhihirisha kuwa, suala la kutumia kiamani nishati ya nyuklia siyo kikwazo kikuu cha mazungumzo ya pande 6, ana imani ya kupata ufumbuzi wa suala hilo.

Mwanzoni Marekani ilipendekeza Korea ya kaskazini iache kwanza kabisa mpango wa nyuklia, maneno aliyosema Bwana Hill yameonesha kuwa mabadiliko yametokea katika msimamo wa sasa wa Marekani. Vyombo vya habari vinaona kuwa, mabadiliko hayo huenda yatakuwa njia ya kupatikana kwa maendeleo katika mazungumzo ya pande 6. Kama utatuzi wa suala kuhusu Korea ya kaskazini kutumia kiamani nishati ya nyuklia utapata maendeleo, basi huenda maendeleo yatapatikana katika mazungumzo ya pande 6. Kwani mabadiliko hayo ya Marekani yanalingana na matakwa ya Korea ya kaskazini.

Korea ya kaskazini siku zote inasisitiza umuhimu kwake wa kutumia kiamani nishati ya nyuklia. Korea ya kaskazini imeeleza mara kwa mara kuwa, kwenye msingi wa kupata uhakikisho wa usalama, nayo inaweza kuacha silaha za nyuklia na mpango wa nyuklia.

Wataalamu wanaona kuwa, mabadiliko ya msimamo wa Marekani yana ishara kuwa huenda migongano kati ya Korea ya kaskazini na Marekani kuhusu suala la kutumia kiamani nishati ya nyuklia itapungua. Lakini Marekani imesema kuwa itaweza kuchukua msimamo wenye unyumbufu, hii haimaanishi kuwa suala litatuliwa bila shaka. Kwani migongano kati ya pande hizo mbili bado ipo katika masuala mengine nyeti.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-25