Katibu wa kamati ya usalama wa taifa ya Iran ambaye pia ni mwakilishi wa kwanza katika mazungumzo ya suala la nyuklia la Iran Bw. Ali Larijani tarehe 25 alieleza kupitia kituo cha televisheni cha Iran kuwa, Iran inatumai nchi tatu za Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani zinazoshiriki kwenye mazungumzo ya suala la nyuklia zitaongezeka na kuwa nchi wanachama wote wa baraza la Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani. Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa, hii ni sehemu moja ya mawazo mapya wa kutatua suala la nyuklia yaliyotolewa na rais mpya wa Iran. Na Iran pia itatoa mapendekezo mapya kamili katika siku za baadaye.
Watu wanaona kuwa, hivi karibuni Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambazo zinauwakilisha Umoja wa Ulaya hazikuchukua hatua nyingi, na siku kadhaa zilizopita zilitangaza kufuta mazungumzo ya nyuklia ambayo yalipangwa kufanyika tarehe 31 mwezi Agosti. Hivi karibuni Iran inatunga mpango mpya wa kutatua suala la nyuklia. Kutokana na habari zilizodokezwa, mawazo ya Iran yamekuwa na mabadiliko kadhaa, na mabadiliko makubwa zaidi ni kutumai nchi zinazoshiriki kwenye mazungumzo ya nyuklia ziongezeke. Mawazo hayo yalitolewa baada ya Iran kuanzisha tena shughuli za kusafisha Uranium na kupinga matakwa ya baraza la Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani kuhusu kuitaka isimamishe shughuli husika. Vyombo vya habari vinaona kuwa hii ni hatua nyingine inayochukuliwa na Iran.
Lakini kwa nini Iran inatumai nchi zinazoshiriki kwenye mazungumzo ya nyuklia ziongezeke? Serikali inayoongozwa na rais mpya inaona kuwa, katika miaka miwili ya karibuni, mazungumzo kati ya Iran na Ufaransa, Ujerumani na Uingereza yalishindwa. Ingawa nchi hizo tatu zinapendekeza kutatua suala la nyuklia la Iran kwa amani, lakini lengo lao ni sawa na Marekani. Zinairuhusu Iran kutumia nishati ya atomiki katika sehemu chache tu, na kushikilia Iran iondoe vifaa vyote vya kusafisha Uranium na kuacha kabisa mpango wake wa nyuklia, ili kuonesha kuwa haina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia. Lakini mambo hayo hayawezi kukubaliwa na Iran. Iran inaona kuwa, nchi tatu za Ulaya zinashinikizwa na Marekani, na kufanya uamuzi kutokana na uamuzi wa Marekani, na kusababisha mazungumzo hayo yasiweze kupata maendeleo yoyote.
Lengo la Iran ni wazi sana. Imetangaza mara nyingi kuwa haina nia ya kutengenza silaha za nyuklia, lengo lake ni kuzalisha nishati kwa kinu cha nyuklia, hivyo haitaacha kamwe haki ya kusafisha Uranium. Kutokana na uzoefu wa miaka miwili iliyopita, Iran inajua vizuri kuwa, kama itaendelea kufanya mazungumzo na Marekani, Ufaransa, na Ujerumani, lengo lake halitaweza kutimizwa. Lazima iongeze nchi zinazoshiriki kwenye mazungumzo, ili ipate fursa mpya. Iran inaona kuwa, katika kutetea utaratibu wa kutoeneza silaha za nyuklia duniani, nchi nyingi zinazoendelea katika baraza la Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani zinapendekeza kutatua suala hilo kwa njia ya kidiplomasia na mazungumzo, na kupinga kuishinikiza Iran kwa nguvu. Katika miaka miwili iliyopita, kutokana na upinzani wa nchi hizo, nchi za magharibi zilishindwa kulihimiza baraza la shirika hilo kupitisha azimio la kuilaani vikali Iran. Kuna tofauti kubwa kati ya maoni ya nchi hizo na nchi za magharibi kuhusu kutumia nishati ya nyuklia kwa amani. Baadhi ya nchi, hasa nchi zisizofungamana na upande wowote ambazo zinachukua theluthi moja katika baraza hilo zinaonesha huruma yao kwa Iran. Na baadhi ya nchi zinaona kuwa, Iran kuanzisha tena shughuli za kusafisha Uranium nchini Iran chini ya usimamizi wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani hakuendi kinyume na makubaliano ya kutoendeleza silaha za nyuklia. Aidha, Russia pia inaiunga mkono Iran. Mambo hayo yote ni fursa za Iran.
Kwa ufupi, serikali ya Iran inaona kuwa, kama nchi zote wananchama za baraza hilo zitashiriki kwenye mazungumzo, basi itaweza kutumia tofauti kati ya nchi hizo kujipatia fursa nyingi za kushindana na nchi za magharibi, na kuongeza uwezekano wa kupata maslahi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-26
|