Polisi wa Afghanistan tarehe 28 walithibitisha kuwa mgombea mbunge mwingine wa Afghanistan tarehe 27 aliuawa katika mashambulizi yaliyotokea kusini mwa Afghanistan. Hadi hivi sasa wagombea wabunge wasiopungua 6 waliuawa na askari wa kundi la Taliban na wafanyakazi walioshughulikia uchaguzi wapatao zaidi ya 10 walijeruhiwa katika mashambulizi hayo. Hali hiyo imeongeza wasiwasi wa watu kuwa uchaguzi wa bunge la nchi hiyo utafanyika bila vikwazo au la.
Uchaguzi wa kwanza wa bunge la Afghanistan unatazamiwa kufanyika tarehe 18 mwezi Septemba mwaka huu baada ya kuahirishwa mara mbili. Wakati huo, wapiga kura zaidi ya milioni kumi watajitokeza kwenye vituo vya upigaji kura nchini humo na kuwachagua wabunge 249 wa baraza la chini la bunge na wabunge 420 wa mabunge ya mikoa mbalimbali. Lakini kadiri tarehe ya uchaguzi inavyokaribia, askari wa kundi la Taliban na wa makundi mengine yasiyojulikana waliimarisha mashambulizi dhidi ya serikali ya Afghanistan, wagombea na wafanyakazi wa uchaguzi huo na jeshi la Marekani lililoko nchini humo, hali ya usalama ya nchi hiyo imekuwa hatari. Jeshi la Marekani lilithibitisha tarehe 27 kuwa jeshi hilo lilipofanya doria katika mkoa wa Paktica, askari mmoja aliuawa. Tarehe 21 askari wanne wa jeshi la Marekani walipofanya doria katika mkoa wa Zabul waliuawa. Kutokana na takwimu, tangu mwaka huu askari 70 wa jeshi la Marekani waliuawa katika sehemu mbalimbali nchini humo.
Kutokana na kukabiliwa na hali ya usalama inayokuwa ya hatari siku hadi siku, msemaji wa kikundi cha kuipatia misaada Afghanistan cha Umoja wa Mataifa Bw. Edrian Edwards hivi karibuni alitoa hotuba mjini Kabul akieleza wasiwasi kwa hali ya usalama katika kipindi cha uchaguzi wa bunge la Afghanistan. Balozi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Bw. Jean Arnault hivi karibuni pia aliainisha kuwa, masuala muhimu yanayokabiliana na uchaguzi wa Afghanistan ni upungufu wa fedha na hali hatari ya nchi hiyo. Ingawa msemaji wa Taliban tarehe 22 alitoa taarifa akisema kuwa kundi hilo halitashambulia raia na vituo vya upigaji kura katika tarehe ya uchaguzi, lakini askari wa Taliban bado wanawashambulia wafanyakazi wa uchaguzi na wagombea ubunge katika sehemu mbalimbali nchini humo.
Ili kuhakikisha uchaguzi wa bunge unafanyika bila vikwazo, jeshi la serikali ya Afghanistan na jeshi la Marekani lililoko nchini humo limeimarisha mashambulizi dhidi ya askari wa Taliban. Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Afghanistan Bw. Zahir Azimi alisema kuwa jeshi la serikali ya Afghanistan na jeshi la Marekani tarehe 25 liliwaua askari 10 wa Taliban katika mkoa wa Kandahar.
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan tarehe 28 alisema kuwa shughuli za ugaidi zilizotokea hivi karibuni nchini humo hazitaathiri kufanyika kwa uchaguzi wa bunge la nchi hiyo. Wachambuzi wanaona kuwa suala la usalama ni jambo la kuamua kufaulu kufanyika kwa uchaguzi nchini humo na tarehe ya uchaguzi huo pia imeahirishwa mara mbili, kwa hiyo kadiri uchaguzi huo unavyokaribia, kuboresha haraka hali ya usalama ya nchi hiyo ni jambo muhimu sana.
Idhaa ya kiswahili 2005-08-29
|