Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-29 21:20:31    
Mkutubi mkuu wa maktaba ya taifa ya China, Bw. Zhan Furui

cri
Mkutubi mkuu wa maktaba ya taifa ya China Bw. Zhan Furui ni mtaalamu wa utafiti wa mshairi mkubwa Li Bai wa Enzi ya Tang (618-907). Alisema, moyo wa mshairi Li Bai ambao mtu lazima atoe mchango hata akiwa kabwera kabisa, unamhimiza siku zote katika kazi yake ya utafiti na usimamizi wa shughuli za maktaba.

Maktaba ya Taifa ya China ni kubwa kabisa barani Asia, na ni kituo kikubwa cha nyaraka duniani. Zhan Furui alikuwa naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Hebei. Miaka mitatu iliyopita alipata uhamisho na kuwa mkutubi mkuu wa maktaba ya taifa badala ya mwanafalsafa mkubwa Ren Jiyu.

Bw. Zhan Furui ana umri wa miaka 52, alizaliwa katika ukoo wa wakulima, alipata utaalam kutokana na juhudi zake. Alipokuwa mtoto alisoma vitabu vingi, na huu ulikuwa ndio msingi wake wa kujihusisha na taaluma baadaye. Alisema, "Ukoo wangu ni wa kawaida kabisa, watu wa ukoo wangu wote ni wakulima. Nilipokuwa mtoto nilipenda fasihi, nilijaribu kusoma vitabu kila nilipopata nafasi, tabia hiyo imeathiri sana maisha yangu ya baadaye."

Aliposoma katika shule ya sekondari, Bw. Zhan Furui alipenda kuandika mashairi, lakini hakupata mafanikio makubwa. Mwishoni mwa miaka ya 60 ya karne iliyopita alianza kusoma fasihi ya kale ya China katika Chuo Kikuu cha Hebei, na kufanya utafiti kuhusu mshairi mkuu Li Bai.

Li Bai ni mshairi mkubwa katika Enzi ya Tang, alizaliwa katika ukoo maskini, lakini elimu yake ilikuwa kubwa, alikuwa mmojawapo wa washairi wakubwa wa Enzi ya Tang. Mshairi huyo kwa upande mmoja alitumai kupata wadhifa fulani ili kuwahudumia raia, lakini kwa upande mwingine alichukia ubovu ulioenea katika jamii na kudharau matajiri wenye madaraka; mara kwa mara alikuwa akiwahurumia raia kutokana na uchungu wa maisha yao akitumai kuwaondolea usumbufu, hata alipokuwa katika hali mbaya aliendelea kuwa na wasiwasi kwa taifa na raia. Kwa kiasi fulani maadili ya Li Bai ni maadili ya wasomi wote wa kale nchini China.

Zhan Furui alipofanya utafiti juu ya Li Bai aliathiriwa sana na fikra zake. Alisema, mashairi ya Li Bai yanaonesha wazi jinsi alivyothamini maisha yake. Mtu hata akiwa kabwera kabisa pia lazima atoe mchango wake na anafaa kwa wengine. Huu ndio moyo wa Li Bai. Alisema, "Li Bai alizaliwa katika ukoo maskini, kwa hiyo rohoni mwake alikuwa na moyo wa kuwahurumia na kuwahudumia watu wengine. Nilitumia muda mrefu kutafiti moyo huo wa wasomi wa China ya kale, naona hata jamii ya leo moyo huo pia una maana. Moyo huo ni moyo wa kuwajibika kwa jamii, ingawa ni watu wa kawaida lakini inawapasa wafuatilie mambo ya taifa na usumbufu wa raia."

Bw. Zhan Furui alisema, jinsi Li Bai alivyothamini maisha yake inamkumbusha mara kwa mara kuwa muda wa maisha ni mfupi, na ni lazima ajitahidi kutoa mchango mkubwa zaidi katika muda huo, na kutokana na sababu hiyo Zhan Furui alipata mafanikio makubwa. Aliwahi kuwa profesa kijana kabisa katika Chuo Kikuu cha Hebei, aliandika vitabu vingi vya taaluma na kupata tuzo ya kitaifa. Hivi sasa Bw. Zhan Furui pia ni mjumbe wa Kamati ya Wataalamu ya China.

Mwaka 2002 baada ya kuwa mkutubi mkuu, Zhan Furui mara alianza kufanya mageuzi, aliingiza kompyuta iliyo ya kisasa ya kuwahudumia wasomaji na kufunga mashirika zaidi ya kumi yaliyokuwa chini ya maktaba yake, ingwa mageuzi hayo yalifanywa katika mkondo wa mageuzi ya taifa, lakini yanahusika moja kwa moja na moyo wake wa kufanya mambo kwa jamii.

Miezi kadhaa iliyopita mradi wa pili wa ujenzi wa maktaba uliowekezwa yuan bilioni 1.2 ulizinduliwa. Bw. Zhan Furui aliona kuwa hii ni fursa nzuri ya kutimiza lengo lake la kuifanya maktaba ya taifa iwe ya kisasa duniani. Alisema. "Naona kushughulikia mradi huo pia ni mchango wangu kwa maendeleo ya utamaduni. Kwa juhudi nitajenga maktaba iwe ya kisasa na iwe na huduma bora nchini China."

Bw. Zhan Furui alisema, lengo lake sio tu la kuijenga maktaba ya taifa iwe ya kisasa bali ataijenga maktaba hiyo iwe kituo cha kufanya utafiti wa utamaduni wa kale. Kutokana na jinsi jamii inavyoendelea, watu wathamini zaidi utamaduni wa kale, na mkataba ya taifa lazima itoe mchango wake katika kuenzi utamaduni huo.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-29