Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-30 15:47:17    
Barua 0828

cri

       Shindano la chemsha bongo kuhusu ujuzi wa "Taiwan?kisiwa cha hazina cha China" linaloandaliwa na Radio China kimataifa limeanzishwa, na idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa itawasomea mfululizo wa makala 4 za shindano hilo la chemsha bongo kuanzia tarehe 4 mwezi Septemba.

Tunawakaribisha wasikilizaji wetu mshiriki kwenye shindano hilo, msikilize matangazo yetu ya makala 4 juu ya ujuzi wa "Taiwan?kisiwa cha hazina cha China" na kujibu maswali yetu, baadaye kutuletea majibu.

Kutokana na makubaliano ya ushirikiano kati ya Radio China kimataifa na Shirika la utangazaji la Kenya KBC, kuanzia tarehe 1 Septemba mwaka huu matangazo ya Kiswahili na Kiingereza ya Radio China kimataifa yataongezwa muda na kuwa saa moja badala ya nusu saa, na matanagazo hayo yataanza saa 9 hadi saa 10 jioni kwa saa za Afrika ya mashariki, ambapo mabadiliko yatatokea kwenye vipindi vyetu. Vile vinavyopendwa zaidi na wasikilizaji wetu, kama vile kipindi cha salamu zenu na burudani za muziki na nyimbo za China na Afrika, vitaongezwa muda. Na kuanzia tarehe 1 Septemba matangazo yetu kwenye masafa mafupi pia yataongezwa muda na kuwa saa moja badala ya nusu saa, ambayo yataanza saa moja hadi saa mbili usiku na marudio yake yataanza saa mbili hadi saa tatu usiku kwa saa za Afrika ya mashariki.

Msikilizaji wetu Mogire Machuki wa kijiji cha Bogeka sanduku la posta 646, Kisii Kenya ametuletea barua akisema kuwa, muda kidogo umepita tangu awasiliane nasi. Hii isiwe shaka kwa CRI kwa sababu kila wakati huwa anatembelea tovuti ya CRI mara moja kwa wiki. Kujuliana hali kwa njia ya barua, kwake anaamini ni njia moja ya kudumisha udugu. Anasema hadi alipokuwa anaandika barua hii, mbele yake kulikuwa na barua kadhaa tulizomwandikia wakati alipokuwa nje ya Kisii. Hivi sasa ndio ameanza kuzishughulikia barua hizo moja baada ya nyingine.

Aidha anaifahamisha Radio China kimataifa kuwa tayari amepokea zawadi yake ambayo alipewa kwenye shindano la chemsha bongo maalum lililoandaliwa na Radio China kimataifa mwaka jana. Anatoa shukrani za dhati. Anasema ni kawaida kwa msikilizaji kuwa na matarajio anaposhiriki kwenye shindano au bahati nasibu, lakini kuibuka mshindi ni bahati. Thamani ya zawadi huwa si hoja sana, bali hoja ni kutangazwa mshindi.

Ilikuwa ni matarajio ya wasikilizaji wa Radio China kimataifa kuchaguliwa kuitembelea China, na kwa kuwa kamati ya shindano hili ilitoa nafasi chache, bahati ilimwangukia rafiki yake Xavier L.Telly Wambwa wa Bungoma Kenya. Anasema kuchaguliwa kwa Bwana Wambwa ni ndoto ambayo ilitimia, anasema yeye binafsi alifurahi kiasi kwamba aliona kama ni yeye aliyetunukiwa tuzo hiyo. Akiwa ziarani nchini China, anaamini kuwa alikusanya habari kadha wa kadha kuhusu China, taifa lenye wakazi wengi kuliko taifa lolote lile duniani kote. Bila shaka ni kumbukumbu ya maisha kwa Bwana Xavier Telly Wambwa.

Bwana Machuki anasema, alipofungua ukurasa wa tovuti ya Radio China kimataifa www.cri.cn na kuchagua Kiswahili, aliona ukurasa maalum uliotengwa na Radio China kimataifa kwa ajili ya ziara ya Bwana Xavier ambapo kumewekwa picha zikionesha maeneo mbalimbali ya Beijing na vitongoji vyake. Alivutiwa sana na mfululizo wa mahojiano kati ya waandishi wa Radio China kimataifa na Bwana Wambwa .

Bwana Machuki anasema, anatoa hongera zake za dhati kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kutokana na kupigania nafasi hii maalum, anasema kwa kweli hili limewatia moyo sana wasikilizaji wengi. Huu ndio urafiki unaostahili na hii inadhihirisha jinsi idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa inavyowajali wasikilizaji wake. Ni nadra sana vituo vingine vya kimataifa kubeba jukumu la kuwaalika wasikilizaji kutembelea mataifa yao. Ni matumaini yetu kuwa huduma hii itazidi kuwepo kwa miaka kadha ijayo, ili wasikilizaji wengi zaidi wapate fursa ya kuitembelea China.

Mwaka 2008 uko karibu sana, na ni matumaini yake kuwa mji mkuu Beijing unaendelea kujiandaa kupokea wageni kutoka duniani kote kwa ajili ya michezo ya Olimpiki. Aidha ana imani kuwa msikilizaji mmoja wa idhaa ya Kiswahili ya CRI atakuwa miongoni mwa wageni maalum watakaoshiriki kwenye ufunguzi wa michezo hiyo. Anasema mengi atatuandikia kwenye barua inayofuata, anamaliza kwa kumpa hongera Bw Wambwa kwa kupata nafasi ya kutembelea China, na anamwambia anaomba ampigie simu kwa namba 0733341272, mara tu namba hizi zitasomwa hewani. Anasema wakiongea anaweza kumwalika Kisii pamoja na msikilizaji wa Tanzania Ras Franz Manko Ngogo ambaye Bwana Wambwa ana zawadi yake.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mogire Machuki kwa barua yake ambayo ametueleza vizuri maoni yake na pia tunamshukuru kwa ukarimu wake kwa wengine wote. Tunaamini kuwa kutokana na msaada wake Bwana Franz Manko Ngogo ataweza kupata zawadi yake katika siku chache zijazo.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-30