Mjumbe wa kamati ya Umoja wa Nchi za Ulaya Bw. Peter Mandelson tarehe 30 alipotoa hotuba kwenye kamati ya biashara ya bunge la Ulaya alitoa wito kuzitaka nchi za Umoja wa Ulaya ziruhusu bidhaa za nguo za China zilizozuiliwa kwenye bandari mbalimbali za Umoja wa Ulaya, ziingie kwenye soko la umoja huo. Wachambuzi wanaona kuwa wito wa Bw. Mandelson unaonesha kuwa kuna mgongano wa maoni ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu suala la bidhaa za nguo kutoka China.
Bw. Mandelson alisema kuwa endapo nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hazitaruhusu kupitisha mizigo ya nguo kutoka China iliyorundikana katika forodha, watu wa Ulaya watakabiliwa na tatizo la kupanda kwa bei za nguo zinazohitajiwa katika majira ya mpukutiko na baridi, vilevile wafanyabiashara wa rejereja wataathiriwa vibaya. Aliongeza kuwa amekosa imani kuhusu kuendelea kutekelezwa mkataba wa bidhaa za nguo kati ya China na Ulaya. Alionya kuwa kutoruhusu bidhaa za nguo za China kutaharibu umoja uliopatikana kwa shida kuhusu suala la bidhaa za nguo za China, hii siyo hali inayotarajiwa na wazalishaji wa nguo, wateja na uchumi wa Umoja wa Ulaya. Hivyo ametaka nchi za Umoja wa Ulaya ziunge mkono pendekezo lake na kupitisha bidhaa nyingi za nguo za China zilizozuiliwa katika forodha.
Bw. Mandelson alisema mara nyingi kuwa, kamati ya Umoja wa Ulaya haijabadilisha msimamo wake kuhusu mkataba wa bidhaa za nguo kati ya China na Ulaya, mkataba huo wenyewe hauna matatizo, mgogoro wa kurundikana kwa mizigo ya nguo kutoka China ni tatizo lililotokea katika utekelezaji wa mkataba huo. Ingawa amesema hivyo, lakini kamati ya Ulaya inakabiliwa na mashinikizo ya aina mbili. Kwa upande mmoja wafanyabiashara wa uagizaji bidhaa kutoka nje na wauzaji wa rejareja wa Umoja wa Ulaya, ni watu wanaoathirika moja kwa moja kutokana na bidhaa nyingi za nguo kutoka China kurundikana kwenye forodha za Umoja wa Ulaya; kwa upande mwingine nchi kubwa za uzalishaji wa bidhaa za nguo na jumuiya za bidhaa za nguo za Umoja wa Ulaya bado hazijakubali kuinua kiwango cha usafirishaji nguo za China au kufuta kabisa utaratibu huo. Bw. Mandelson alitoa wito huo kutokana na mgongano huo.
Wachambuzi wanaona kuwa kumetokea mabadiliko kidogo katika msimamo kuhusu suala la kurundikana kwa bidhaa za nguo. Katika mkutano uliofanyika tarehe 29 kwa waandishi wa habari alikanusha baadhi ya matamshi ya vyombo vya habari vya Ulaya yanayosema kuwa, bidhaa za nguo zilizorundikana zitazidisha hali ya upungufu wa bidhaa za nguo katika soko la Ulaya. Aliongeza kuwa tamko lile ni la kutia chumvi. Katika hotuba aliyotoa tarehe 30 Bw. Mandelson alionya nchi za Umoja wa Ulaya kuwa kuendelea kurundikana kwa bidhaa za nguo kutoka China kutasababisha upungufu wa bidhaa za nguo na kupanda kwa bei ya nguo katika soko la Ulaya. Mabadiliko hayo hasa yanatokana na mawazo ya aina mbili. Kwanza, kuendelea kurundikana kwa bidhaa za nguzo za China kutaleta hasara kubwa zaidi kwa wafanyabiashara wa uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje na wafanyabiashara wa uuzaji wa rejareja wa Umoja wa Ulaya, si kama tu hawawezi kupata bidhaa walizoagiza na kuathiri pato lao, bali pia itawabidi kulipa gharama kwa ajili ya bidhaa zao zilizorundikana forodhani.
Kwa upande mwingine tatizo la kurundikana kwa bidhaa za nguo za China ingawa halitafanya "Ulaya kukosa suruali za kuuza katika nusu ya pili ya mwaka huu" kama baadhi ya vyombo vya habari vinavyosema, lakini huenda kusababisha upungufu wa bidhaa za nguo katika soko la Ulaya. Kwani bidhaa za nguo zilizoagizwa kutoka China na kampuni nyingi za nguo za Ulaya zinafikia zaidi ya 30%.
Hivi sasa Bw. Mandelson amewasilisha pendekezo lake kwa kamati ya Umoja wa Ulaya kuhusu suala hilo. Vyombo vya habari vinaona kuwa pendekezo hilo ni kuhusu namna ya kutatua suala la kiwango cha usafirishaji nje wa bidhaa za nguo za China kwa Umoja wa Ulaya.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-31
|