   
Kimbunga kinachojulikana kwa jina la Katrina kimeikumba sehemu ya kusini ya Marekani, nguvu yake na uharibifu wake ulizidi makadirio ya watu. Meya wa mji wa New Orleans Bw. Ray Nagin tarehe 31 Agosti alisema, kimbunga kimewaua watu wsiopungua mia kadhaa, na idadi hiyo si ya mwisho kwa sababu bado kuna maiti nyingi ndani ya maji, pengine idadi hiyo inaweza kufikia elfu kadhaa.
Mji wa New Orleans uko kwenye kando ya Mto wa Mississippi katika sehemu iliyodidimia kama bakuli, na kwa wastani mji huo uko chini ya uso wa bahari na sehemu fulani hata iko mita tatu chini ya usawa wa bahari. Kimbunga kilikuwa na kasi ya kilomita 300 kwa saa kilipopita kwenye mji huo, kutokana na boma la kukinga maji ya bahari kubomoka asilimia 80 ya mji huo iligharikishwa, takataka zilizovujwa kutoka kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta zilifanya mji huo kuwa ni "ziwa la sumu".
Polisi wamesema, maiti nyingi zinaelea kwenye maji mjini humo, mkondo wa maji wenye nguvu ulibomoa daraja moja kubwa, mafuta na gesi vinavuja, nyaya za umeme zilizokatika zilisabisha moto, moshi mnene unatokea na wazima moto wanashindwa kuuzima kutokana na maji. Kiasi cha wakazi elfu 50 hadi laki moja wanaishi katika mji huo, kati yao karibu elfu 30 walikimbilia kwenye paa la jumba la michezo, kutokana na kukosa maji na umeme hali yao ni mbaya sana. Baadhi ya watu walitumia fursa hiyo "kufanya uporaji", walinyakua pesa taslimu, na hata walisafisha duka la silaha. Hivi sasa maji bado yanaongezeka. Mkuu wa Jimbo la Louisiana tarehe 31 Agosti alisema, hakuna chaguo lolote lingine ila kuuacha tu mji huo.
Hivi sasa ingawa kimbunga hicho kimepungua nguvu, lakini athari zake kwa majimbo ya Alabama, Mississippi na Florida pia zitakuwa kubwa. Popote kimbunga kinapopita mawimbi ni makubwa, mvua ni kama maji yaliyomwagika, mapaa yanafumuliwa, watu wasiopungua milioni nne wanakosa maji ya umeme. Habari zinasema kuwa kimbunga hicho kimesababisha vifo vya watu 110 katika jimbo la Mississippi. Kadhalika hasara iliyosababishwa na kimbunga hicho pia ni kubwa, kwamba asilimia 95 ya viwanda vya kusafisha mafuta katika Ghuba ya Mexico vimefungwa, na kusababisha bei ya mafuta kupanda hadi dola za Kimarekani 70 kwa pipa. Shirika la bima pengine litalipa fidia ya dola za Kimarekani bilioni 25, na hasara ya mali ambazo hazikukatiwa bima itafikia dola za Kimarekani bilioni nne hadi bilioni 10.
Siku chache zilizopita rais Bush wa Marekani alirudi ikulu baada ya likizo, na tarehe 31 Agosti alikagua sehemu iliyoathirika kwa ndege. Habari nyingine zinasema kuwa serikali ya Marekani imepeleka vikundi 32 vya madaktari, na wizara ya ulinzi ilipeleka helikopta tano na meli zilizosheheni vitu vya uokoaji kwenye sehemu zinazoathirika. Askari wa uhandisi wanatumia mifuko yenye mchanga na vipande vya saruji kuziba pengo la boma la kuzuia maji baharini. Msalaba mwekundu wa Marekani umeripoti kuwa umeandaa sehemu 200 za kuwahifadhi watu na kupeleka vifaa 185 kwa seti za uokoaji kwenye eneo la mafuriko.
Idhaa ya kiswahili 2005-09-01
|