Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-01 16:44:03    
Mtibet Dan Zeng Qunpei na mtalii wa Uswizi

cri

Mkoa unaojiendesha wa Tibet ulioko kwenye uwanda wa juu kabisa duniani, una mandhari nzuri ya maumbile ya kiasili, milima inayofunikwa na theluji siku zote, maziwa yanayotapakaa hapa na pale, swala wa kitibet na punda pori wanaokimbia katika sehemu zisizokuwa na wakazi, pamoja na dini ya kibuddha ya kitibet, mahekalu na watawa waliovaa majoho mekundu wanaowavutia sana watalii kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mbali na waongoza watalii, wenyeji waliowasiliana zaidi na watalii kutoka nchi mbalimbali ni madereva wanaoendesha magari ya kuwatembeza watalii?Dan Zeng Qunpei ni mmoja wa madereva hao.

Dan Zeng Qunpei mwenye umri wa miaka 33 amefanya kazi ya dereva kwa miaka zaidi ya kumi, na anapendwa na watalii kutokana na uaminifu wake na huduma bora anazotoa. Ingawa kazi yake ni kuendesha gari, lakini yeye huwaelezea wageni mambo ya utalii, kutafsiri kwa lugha ya Kitibet, na kuwabebea mizigo yao mizito.

Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, alizawadiwa gari la kuwatembeza watalii na kiongozi wa ujumbe wa watalii kutoka Uswisi. Mwanzoni Bwana Dan Zeng alikuwa akifanya kazi ya dereva kwenye shirika la utalii na kuwapeleka watalii wa nchi za nje kutembelea kwenye uwanda wa juu. Miongoni mwa wageni wake, wengi walitoka nchini Uswisi, baadhi yao wanapenda kutembelea mahekalu, wengine wanapenda kufurahia mandhari nzuri ya uwanda.

Mwezi Julai mwaka huu, Bw. Dan Zeng na madereva wengine wawili walipokea ujumbe wa watalii kutoka Uswisi, na kuwatembeza kwa mwezi mmoja katika sehemu ya katikati na kusini mwa Tibet. Safari ilipoisha, kiongozi wa ujumbe huo, mwanamke mwenye umri wa makamo alimpa kifuta jasho kikubwa. Miezi miwili baadaye, Bw. Dan Zeng aliambiwa apokee ujumbe mwingine kutoka Uswisi, kumbe mama huyo wa Uswisi alikuja tena pamoja na ujumbe wa watalii. Mama huyo alipofahamu kuwa, Bw. Dan Zeng alitaka kununua gari lake mwenyewe, alimwambia kuwa, atamnunulia gari moja kwa ajili ya kuwatembeza watalii. Mwanzoni Bw. Dan Zeng alidhani kuwa ni mzaha tu, lakini siku ya pili baada ya kurudi mjini Lahsa, mama huyo wa Uswisi kweli alimnunulia gari la kuwatembeza watalii aina ya Toyota lililotumika, kwa yuan laki 1.7.

Alipoulizwa kwa nini mama huyo wa Uswisi alimnunulia gari wala siyo madereva wengine? Bw. Dan Zeng anasema:

"Walisema kuwa, tofauti na madereva wengine, mimi ni mwaminifu. Mama huyo amekuja hapa kwa mara tatu, niliwapeleka watalii mahali popote walipotaka kuelekea bila ya malalamiko yoyote. Nafikiria kuwa, wamekuja kutoka mbali sana, lazima niwahudumie vizuri."

Licha ya hayo, Bw. Dan Zeng huwasaidia kubeba mizigo, kudumisha usafi wa mizigo, na anakuwa na tahadhari wakati wa kuendesha gari ili kulinda usalama wa watalii.

Alipozungumzia kuhusu mpango wake wa siku zijazo, Bw. Dan Zeng anasema:

"Siku zijazo, nitaendelea kuendesha gari kwa tahadhari na kwa bidii ili kulimbikiza pesa. Nitampeleka mtoto wangu asome katika shule bora, na tunataka kutembelea hapa na pale. Ikiwezekana, nitaenda kuwatembelea marafiki zangu wa Uswizi."

Bw. Dan Zeng alisema kuwa, mwaka kesho amepanga kununua gari jipya la kuwatembeza watalii ili kuendelea kuwapokea watalii. Baada ya kutimiza umri wa miaka 50, ataacha kazi ya dereva, na kuendesha mkahawa wa chai mjini Lahsa. Yeye na mke wake walikutana kwa mara ya kwanza kwenye mkahawa wa chai miaka kumi iliyopita.

Bwana Dan Zeng alisema kuwa, mama huyo wa Uswisi alimpigia simu kuwa, atakuja Tibet kwa mara nyingine tena, na yeye alitakiwa kuwapokea watalii kutoka mji wa Chengdu, ambao wanatarajia kwenda Tibet kwa kufuata barabara kuu ya Sichuan-Tibet. Alipozungumzia uhusiano kati yake na mama huyo wa Uswisi hakuweza kuficha furaha yake kubwa usoni.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-01