Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-02 15:18:17    
Russia yaadhimisha mwaka mmoja wa tukio la utekaji nyara la Beslan

cri

Tarehe mosi mwezi Septemba ni siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu tukio la utekaji nyara litokee mjini Beslan, Jamhuri ya Osetia ya Kaskazini ya Russia. Siku hiyo watu wa sehemu mbalimbali nchini Russia waliomboleza vifo vya watu waliokufa katika tukio hilo na kueleza nia yao ya kuthamini amani na kupambana na ugaidi wa aina zote.

Saa tatu na dakika 15, asubuhi kengele za Beslan zilipigwa. Shughuli za maadhimisho zilianza na zitafanyika kwa siku tatu katika Jamhuri ya Osetia ya Kaskazini. Kabla ya mwaka mmoja, magaidi kumi kadhaa wenye silaha wakiwa kwenye magari matatu waliingia kwenye shule ya kwanza ya mji wa Beslan iliyokuwa inafanya sherehe ya ufunguzi wa muhula mpya wa masomo na kuwateka wanafunzi, walimu na wazazi wa wanafunzi wapatao zaidi elfu moja. Kutokana na takwimu mpya za serikali ya Russia, watu 331 walikufa katika tukio hilo. Beslan ni mji mdogo wenye wakazi zaidi ya elfu kumi na tukio hilo linaihusu karibu kila familia mjini humo.

Asubuhi ya tarehe mosi, mateka walionusurika, jamaa za mateka waliokufa, maofisa wa serikali ya Jamhuri ya Osetia ya Kaskazini, mjumbe wa rais wa Russia aliyeko katika sehemu ya Caucasian ya kaskazini na watu elfu kadhaa walichukua maua na mishumaa kwenda kwenye mabaki ya shule ya kwanza ya Beslan na kushiriki kwenye shughuli za maadhimisho hayo. Zaidi ya hayo waandishi wa habari zaidi ya 400 kutoka nchi 20 ikiwemo China walikwenda mjini Beslan kutoa maelezo kuhusu shughuli hizo.

Asubuhi ya siku hiyo, rais Putin wa Russia alikwenda kwenye chuo kikuu cha kilimo cha Kuban kilichoko kusini mwa Russia kufanya ukaguzi. Alishiriki kwenye shughuli kuwaomboleza watu waliokufa katika tukio la Beslan akiwa na wanafunzi na wahadhiri wa chuo kikuu hicho.

Waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergei Lavrov siku hiyo mjini Moscow alimpa mjumbe wa Jamhuri ya Osetia ya Kaskazini kitabu cha saini za watu wa nchi mbalimbali duniani walioomboleza vifo mateka waliokufa katika tukio la Beslan. Alisisitiza kuwa hakutakiwi kuwa na vigezo viwili katika kupambana na ugaidi, na jumuiya ya kimataifa lazima iungane na kupambana na ugaidi.

Tukio la mateka la Beslan lilizushwa na kundi haramu la ufarakanishaji la Chechnya, Russia. Ufarakanishaji ni chanzo cha kuleta ugaidi nchini Russia. Shughuli za kuadhimisha mwaka mmoja wa tukio la Beslan katika sehemu mbalimbali nchini Russia zinaonesha kuwa Russia inapiga moyo konde kuimarisha nguvu za kupambana na ufarakanishaji na ugaidi na kulinda muungano wa taifa na usalama wa raia.

picha husika>>

1  2