Kutokana na athari kubwa ya kimbunga kiitwacho "Katrina", mji wa New Orleans ulikumbwa na fujo, watu elfu kumi kadhaa walipoteza makazi. Hilo ni janga kubwa katika historia ya Marekani. Serikali ya Marekani ilichukua hatua nyingi kuwaokoa waathirika, hivi sasa hali ya mji huo inaelekea kutulia, na kazi ya kuwahamisha waathirika kwenye sehemu salama imeanza kupata mafanikio.
Kimbunga cha Katrina kilifika Marekani tarehe 25 Agosti, na tarehe 29 kilifika katika majimbo ya Louisiana, Mississippi na Alabama, nguvu yake na uharibifu wake mkubwa ulizidi makadirio. Mpaka sasa watu elfu kadhaa wamekufa na laki kadhaa wamepoteza makazi yao, hasa mji wa New Orleans ambao 80% imekumbwa na mafuriko, watu kiasi cha elfu 80 walikwama ndani ya mji wakisubiri msaada. Katika siku hizo mji ulikuwa katika hali ya vurugu mbaya.
Baada ya kutokea maafa hayo, serikali ya Marekani ilichukua hatua nyingi za dharura. Rais George Bush wa Marekani tarehe 31 Agosti alikatisha likizo yake na kurudi ikulu, akaunda kikundi cha kuongoza uokoaji kilichoongozwa na waziri wa ulinzi, na kumwagiza mkuu wa Shirika la Dharura kushughulika na uokoaji katika sehemu ya maafa. Katika siku hiyo rais Bush alitangaza kuanza kutumia akiba ya mafuta ili kuziba pengo lililosababishwa na kimbunga hicho. Tarehe 2 Septemba Bush alikagua sehemu ya maafa kwa ndege.
Bunge la Marekani tarehe 2 Septemba lilipitia idhini ya matumizi ya dola za Kimarekani bilioni 10.5 kwa ajili ya uokoaji na fedha hizo zilianza kutumika siku hiyo. Serikali ya Marekani imepanga kupeleka askari 11,200 kufanya uokoaji na sasa askari 4000 wamefika mahali wanapotakiwa. Kati ya askari wa ulinzi elfu 40, elfu 30 wameanza kazi ya uokoaji. Rais Bush pia aliongeza askari 7200 wakiwemo wanamaji kwenda kwenye Ghuba la Mexico. Isitoshe, meli 10 ikiwemo manowari moja yenye vituo vya ndege zilitumwa kwenye Ghuba ya Mexico, na meli ya matibabu yenye vitanda elfu moja itafika kwenye ghuba hilo katika siku chache zijazo. Shirika la Dharura la Marekani lilikodi mabasi elfu mbili kwenda kuwasafirisha waathirika. Mpaka tarehe tatu jioni, waathirika elfu 42 wameondolewa kutoka sehemu ya maafa.
Tarehe 3 rais Bush alisema, hivi sasa kazi ya uokoaji ni ya kipaumbele, na serikali haitapumzika kabla ya kukamilisha jukumu la uokoaji.
Waathirika kiasi cha laki 2.4 wa Mji wa New Orleans wamepata makazi ya muda katika mji wa Huston, mji uliopo mbali na New Orleans kwa kilomita 500. Mji wa Huston ulishirikisha idara zote za umma na za binafsi na idara zisizo za biashara kuwapokea waathirika hao na kutatua matatizo ya mahitaji ya waathirika. Inasemekana kwamba, siku hizi shule zimeanza muhula mpya nchini Marekani, shule za mjini Huston zimewapokea watoto wa waathirika kiasi cha elfu nane. Mkuu wa jimbo la Texas amekuwa akiwasiliana na wakuu wa majimbo mengine akitumai majimbo mengine yatapokea waathirika vilevile.
Idhaa ya kiswahili 2005-09-05
|