Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-05 16:06:29    
Fasihi ya Makabila Madogo Madogo Iliyojaa Ustawi nchini China

cri

Maandishi ya kikabila yaliyopata tuzo ya "farasi hodari" yamechaguliwa hivi karibuni. Maandishi 30 yaliyoandikwa na waandishi wa makabila madogo madogo 15 yamepata tuzo hiyo.

"Tuzo ya Farasi Hodari" ilianza kutolewa mwaka 1981, hii ni moja ya tuzo za aina nne za fasihi nchini China. Tuzo hiyo inatolewa kwa mandishi bora ya makabila madogo madogo tu, wanaoshiriki kugombea tuzo hiyo ni waandishi wa makabila madogo madogo, na maandishi yanaweza kuandikwa kwa lugha za kikabila au lugha ya kawaida ya Kichina. Maandishi 30 yaliyopata tuzo hiyo yalichaguliwa kutoka maandishi 343. Kati ya maandishi hayo 30, kuna riwaya ndefu 5, riwaya ndefu kiasi 5, mikusanyiko ya mashairi mitano, na maandishi ya aina nyingine.

Ili kustawisha maandishi ya makabila madogo madogo, serikali ya China imeweka tuzo hiyo ambayo haipo katika nchi nyingine. Serikali ya China inatilia maanani namna ya kuwahimiza waandishi wa makabila madogo madogo waandike maandishi yao kwa lugha za kikabila. Nchini China kuna makabila madogo madogo 55 licha ya kabila kubwa la Wahan, na kati ya makabila hayo, makabila 21 yana maandishi yake. Kati ya maandishi yaliyopata "tuzo ya farasi hodari", 10 yaliandikwa kwa lugha za kikabila, ambayo ni theluthi moja ya maandishi yote yaliyopata tuzo. Mkurugenzi wa kundi la wachaguzi wa maandishi ambaye pia ni mshairi wa kabila la Wayi, Jidimaja, alisema kuwa "tuzo ya farasi hodari" inalenga kuwatia moyo waandishi wa makabila madogo madogo. Alisema, "Tuzo hiyo imezingatia maandishi ya makabila madogo madogo, maandishi hayo yanaambatana moja kwa moja maisha ya watu wa makabila madogo madogo. Serikali ya China inatilia maanani sana maendeleo ya lugha za kikabila na kuheshimu utamaduni wa makabila hayo."

Katika miaka 20 iliyopita, limetokea kundi la waandishi wa makabila madogo madogo, maandishi yaliyoandikwa kwa lugha za kikabila au kwa Kichina yote yameonesha mila na desturi za watu wa makabila yao, kwa riwaya au kwa mashairi. Riwaya iliyopata tuzo "Mbingu na Ardhi" imeeleza hatima ya wakulima wa China. Riwaya hiyo ndefu ilichapwa mara nyingi, na hivi sasa imehaririwa kuwa mchezo wa televisheni wenye sehemu 24, na utaoneshwa kwenye televisheni hivi karibuni.

Hivi sasa fasihi nchini China ni ya utamaduni wa aina nyingi ikiwemo fasihi ya makabila mengi madogo madogo, huu ndio utamaduni mkubwa wa China, na ustawi wa utamaduni huo hauwezi kutengana na juhudi za waandishi wa makabila madogo madogo. Waandishi 32 waliopata tuzo, wote ni wa makabila madogo madogo, ambao wanazingatia sana historia na hali ya makabila yao, na wameonesha kuwajibika kwa makabila yao na taifa la China. "Waandishi wengi hasa vijana, wana fikra za kuendana na wakati, maandishi yao yenye fikra za kisasa yana umuhimu kwa makabila yao. Waandishi hao wanaingiliana, wanafunzana na wanapeana uzoefu."

Pamoja na ustawi wa maandishi ya makabila madogo madogo, kazi ya utafiti wa fasihi ya makabila madogo madogo pia imeanza na imeenea. Utafiti huo unafanywa pamoja na historia ya fasihi, isimu, elimu ya dini, saikolojia, na historia ya makabila kwa ujumla.

Bw. Baomingde ni mshairi wa kabila la Wamongolia, na mhariri mkuu wa jarida la "Uhakiki wa Fasihi". Alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, hiki ni kipindi kizuri cha maendeleo ya fasihi ya makabila madogo madogo, waandishi wengi hodari wa makabila hayo wameibuka, baadhi yao wanaandika maandishi kwa lugha ya Kichina na wengine wanaandika kwa lugha za kikabila. Alisema, "Ustawi wa fasihi katika taifa fulani unahitaji fasihi na utamaduni wa makabila tofauti, na unahitaji maingiliano ya fasihi tofauti."

Bw. Baomingde aliongeza kuwa fasihi ya makabila madogo madogo ina nafasi kubwa ya kuendelea, kila kabila lina utajiri mkubwa wa utamaduni. Aina tofauti za utamaduni zinaimarika hivi sasa. Kutokana na uchumi unavyoendelea, fasihi na utafiti wa fasihi wa makabila madogo madogo hakika utapata maendeleo makubwa.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-05