Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-06 19:34:06    
Mji mtangulizi wa maendeleo ya uchumi wa China

cri

Shenzhen ni mji uliostawi kwenye miaka ya karibuni katika sehemu ya kusini ya China. Siku chache zilizopita mji wa Shenzhen uliadhimisha miaka 25 tangu uwe eneo maalumu la kiuchumi. Katika muda huo mfupi wa miaka 25, Shenzhen ambayo ilikuwa tarafa ndogo sasa imekuwa mji mkubwa wa kisasa na kasi ya maendeleo yake imezidi zile za nchi nne zinazojulikana kwa "Dragon wanne barani Asia" ambazo zilifanya maajabu ya kiuchumi duniani. Kutokana na hadhi yake maalumu Shenzhen inasifiwa kuwa mji mtangulizi wa uchumi wa China.

Shenzhen ikiwa ni eneo maalumu ya kiuchumi nchini China, tangu ilipoanzishwa ilikuwa kama "dirisha" na "shamba la majaribio" la mageuzi na ufunguaji mlango nchini China. Shenzhen iko karibu na Hong Kong, ina ubora wa kijiografia, mwaka 1980 serikali ya China iliamua kuanzisha eneo maalumu la kiuchumi huko Shenzhen na kuipa hali nafuu katika matumizi ya ardhi na ukusanyaji wa kodi, ili kuwavutia wafanyabiashara wawekezaji wa kigeni, kujaribu kutatua tatizo la upungufu wa mitaji inayohitajika katika maendeleo ya uchumi wake kwa kutumia mitaji ya nchi za kigeni na kuhimiza maendeleo ya uchumi kwa kuingiza teknolojia ya kisasa na uzoefu wa usimamizi.

Mtafiti wa taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bw. Han Meng alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa, Shenzhen ikiwa ni "dirisha" na "shamba la majaribio" kwa mageuzi na ufunguaji mlango nchini China, inatakiwa kutafuta njia mpya ya maendeleo ya uchumi wa China na kutoa uzoefu na maarifa ya kuigwa.

"kwa nchi ya China, umuhimu mkubwa kabisa wa Shenzhen katika uchumi wa taifa ni kuonesha mfano wa kuelekea kwenye uchumi wa soko huria kutoka uchumi wa kimpango, kustawisha uchumi, kufungua mlango kwa nje na kufanya mageuzi ya uchumi wa soko huria."

Baada ya Shenzhen kuwa eneo maalumu la kiuchumi mwaka 1980, Shenzhen ilikuwa ya kwanza kufanya mageuzi dhidi ya utaratibu wa ajira, bei za vitu, kuingiza matumizi ya ardhi ya taifa katika mnada, kuanzisha utaratibu wa umilikaji hisa katika viwanda na kampuni na kuanzisha utaratibu wa uchumi wa kimasoko wa kiujamaa, kuleta nguvu ya kuhimiza maendeleo ya kasi na kuwa mtangulizi katika maendeleo ya uchumi wa China.

Katika miaka 25 iliyopita maendeleo ya Shenzhen yalifikia katika kiwango cha kushangaza: iliendelezwa na kuwa mji wa kisasa wenye eneo la kilomita za mraba karibu 600 kutoka tarafa ndogo iliyokuwa na eneo la kilomita za mraba 3; Pato lake limekuwa na wastani wa ongezeko la 28% kwa mwaka, ambapo pato lake lilifikia Yuan zaidi ya bilioni 340 mwaka jana; wastani wa thamani ya uzalishaji mali ulikuwa pungufu ya Yuan 1,000 kwa mtu mwaka 1980 uliongezeka na kufikia karibu wastani wa Yuan elfu 60 kwa mtu kwa hivi sasa.

Mstaafu Bw. Gan Lin ambaye alifanya kazi kwa miaka zaidi ya 20 huko Shenzhen ameshuhudia maendeleo ya Shenzhen alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

"Shenzhen ilikuwa sehemu ndogo, lakini sasa imekuwa mji mkubwa wenye idadi ya watu zaidi ya milioni 10. Nilipofika huko miaka 20 iliyopita, Shenzhen ilikuwa tarafa moja ndogo, jengo muhimu lilikuwa kituo cha garimoshi tena ni la zamani sana; hivi sasa sehemu ya mji imepanuliwa mara kadhaa tena imejengwa kwa mpango wa kisasa.

Bw. Gao ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya sekondari anaridhika na maisha yake ya hivi sasa. Alisema kuwa mwanzoni baada ya kufika Shenzhen alikuwa na mshahara wa Yuan 200 hivi, hivi sasa anapata kiinua mgongo cha uzeeni Yuan elfu 4 hivi kwa mwezi, amenunua nyumba na vyombo vya umeme vya nyumbani, yeye na jamaa zake wanakwenda kula mahotelini mara kwa mara.

Hivi sasa miaka 25 imeshapita, sera nafuu zinazohimiza maendeleo ya Shenzhen pamoja na uzoefu bora wa maendeleo ya Shenzhen vinaigwa na sehemu mbalimbali nchini. Hivi sasa China inafuata utaratibu wa uchumi wa kimasoko ya kijamaa kote nchini, viwanda na kampuni za serikali zimefanya mageuzi ya utaratibu wa umilikaji wa hisa na kuanzisha kampuni na viwanda vingi vilivyowekezwa na wafanyabiashara wa kigeni na binafsi. Utaratibu mpya umehamasisha juhudi na uvumbuzi wa watu, na uzalishaji wa viwanda umeleta bidhaa za kila aina kwenye maduka nchini China. Wakazi wengi wa mijini wanaiishi kwa raha mustarehe kama ilivyo kwa Bw. Gao.

Shenzhen ya leo imekuwa na majumba marefu na magari mengi na inaonekana kama mji mkubwa wa kisasa. Lakini pamoja na kuendelezwa kwa mfululizo mageuzi na ufunguaji mlango, sera na uzoefu vilivyoleta maendeleo makubwa ya uchumi vimetekelezwa katika sehemu mbalimbali nchini. Katika hali ya namna hiyo Shenzhen itaweza kuendelea kuwa "shamba la majaribio" na mtangulizi katika mageuzi na ufunguaji mlango nchini?

Wataalamu wa uchumi wanasema kuwa maendeleo ya Shenzhen katika siku za usoni ni kama sehemu nyingi nchini kuwa itazuiliwa na vitu vingi vikiwemo ardhi, nishati na raslimali ya maji, njia yake ya zamani ambayo viwanda vyake vilikuwa vinatumia wafanyakazi wengi na kubadilisha tekinolojia kwa masoko hivi sasa haifai tena. Kwa kuzingatia hali hiyo Shenzhen inatoa wito wa kuifanya Shenzhen iwe "shamba la majaribio" na mtangulizi wa kutekelza wazo la maendeleo ya kisayansi lililotolewa na serikali kuu, na kuiacha Shenzhen iendelee kutafuta njia mpya kwa maendeleo ya uchumi wa China.

Wazo la maendeleo ya kisayansi linalotajwa ni kuwa, katika maendeleo ya uchumi na jamii, tunatakiwa kupunguza shinikizo la raslimali na mazingira, kujitahidi kudumisha maendeleo endelevu ya uwiano kati ya binadamu na maumbile, kati ya miji, vijiji na maeneo mbalimbali. Hivi sasa, Shenzhen imefanya utafiti mwingi katika upande huo. Kabla ya miaka michache iliyopita, Shenzhen ilitangulia kuweka lengo la kujenga "mji wa uvumbuzi", ambalo ni kuanzisha sekta ya teknolojia mpya ya kiwango cha juu inayoleta nyongeza ya thamani.

Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa eneo la maendeleo ya teknolojia ya kisasa la Shenzhen Bw. Lin Po alisema, maendeleo ya Shenzhen katika siku za usoni yatategemea uvumbuzi, kuchukua nafasi za soko la China na masoko duniani kwa tekinolojia na bidhaa mpya. Hivyo wametia kipaumbele katika kutoa mazingira bora kwa taasisi mbalimbali katika utafiti na uvumbuzi wake na kutumia mafanikio yake katika uzalishaji mali. Alisema,

"Tunatakiwa kubadilisha mkusanyiko wa sekta za uzalishaji mali kuwa mkusanyiko wa sekta za utafiti na uvumbuzi, serikali inatakiwa kutoa msaada wa raslimali za umma kwa utafiti na uvumbuzi. Hivi karibuni sisi tumekuwa na ushirikiano na maabara muhimu 78 za taifa na kuanzisha mfumo wa mawasiliano ya maabara za umma. Licha ya hayo tumetoa huduma kwa viwanda katika ukusanyaji fedha, usimamizi wa viwanda na uuzaji wa bidhaa ili kupunguza gharama za viwanda katika shughuli za uvumbuzi na kujiimarisha."

Katika mwelekeo wa maendeleo ya uchumi, Shenzhen imetangulia mbele nchini. Tofauti ni kuwa safari hiyo maendeleo ya Shenzhen hayategemei sera nafuu za serikali bali ni nguvu ya uchumi, uvumbuzi wa kisayansi na uzoefu wake.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-06