Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-06 19:36:03    
Kitendo cha upande mmoja wa Israel kitakuwa na ufanisi mkubwa kiasi gani katika nchi za kiislam?

cri

Hivi karibuni serikali ya Israeli ikitumia fursa ya kutekeleza mpango wa vitendo wa upande mmoja ilifanya shughuli nyingi za kidiplomasia ili kuboresha uhusiano na nchi jirani za kiarabu, na ilipata maendeleo fulani. Lakini wachunguzi wanasema kuwa katika mazingira ya kuwepo kwa uhasama kwa nchi za kiarabu dhidi ya Israel, siyo kazi rahisi kuondoa uhasama uliokuwepo tangu miaka mingi iliyopita kati ya pande hizo mbili, hivyo watu wana mashaka kuhusu ufanisi wa utekelezaji wa mpango wa upande mmoja wa Israel.

Mwanzoni mwa mwezi huu, waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Bw. Khursheed Kasuri na waziri wa mambo ya nje wa Israel Bw. Silvan Shalom walikuwa na mazungumzo huko Istanbul nchini Uturuki. Mazungumzo hayo yalikuwa mazungumzo ya kwanza kati ya maofisa wenye vyeo vya juu wa pande hizo mbili na kusifiwa kuwa ni mafanikio makubwa ya kidiplomasia katika uhusiano wa nchi mbili. Bw. Shalom alisema kuwa mazungumzo hayo ni yenye "umuhimu wa kihistoria" na kuwa "baada ya Israel kuondoka kutoka sehemu ya Gaza, uhusiano kati ya nchi za kiarabu na kiislam pamoja na Israeli utakuwa mpya kabisa", aliongeza kuwa anatarajia mazungumzo hayo yatawezesha kujenga uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israel na Pakistan, hata na nchi zote za kiarabu na za kiislam.

Uhusiano kati ya Misri ambayo ni nchi kubwa katika mashariki ya kati na Israel, hivi karibuni umeboreshwa kwa kiwango fulani baada ya Israeli kuondoka kutoka sehemu ya Gaza. Waziri wa mambo ya nje wa Israel Bw. Shalom tarehe 5 alisema kuwa rais Mubarak wa Misri huenda atafanya ziara nchini Israel mwezi Novemba na kuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa Israeli Bw. Sharon. Licha ya hayo kulikuwa na habari nyingi zilizochapishwa kwenye magazeti kuhusu wizara ya mambo ya nje ya Israel kupeleka ujumbe kutembelea nchi jirani za Umoja wa Nchi za falme za Kiarabu na Tunisia.

Ikilinganishwa na matamshi ya Israel, nchi za kiarabu na za kiislam zinachukua msimamo kwa uangalifu zaidi. Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan tarehe 3 ilisema kuwa kuhusu suala la Israel, Pakistan haijabadilisha msimamo wake wa kikanuni. Kabla ya kuanzishwa kwa nchi ya Palestina, Pakistan haiwezi kuitambua Israel na kuwa na uhusiano wowote wa kiuchumi na kibiashara pamoja na Israel. Ilisema pia kuwa habari zinazosema kuwa rais Musharraf wa Pakistan katika kipindi cha mkutano wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Mataifa atakuwa na mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Israel ni uvumi mtupu. Licha ya hayo Ikulu ya Misri tarehe 5 ilikanusha tetesi kuhusu rais Mubarak kutembelea Israel.

Ni dhahiri kuwa vitendo vya Israel vya kuondoa makazi 25 ya wayahudi yaliyoko katika sehemu ya Gaza na kando ya magharibi ya mto Jordan si kama tu vimepongezwa na jumuiya ya kimataifa bali pia vimeleta fursa kwa Israel kuboresha uhusiano na nchi za kiarabu na nchi za kiislam. Hivi sasa Israel imekuwa moja ya nchi kubwa na yenye nguvu katika mambo ya kiuchumi na kijeshi kwenye sehemu ya mashariki ya kati, kuweko kwake kumekuwa ukweli usioweza kuepukwa, kuendeleza uhusiano wa kisiasa na kiuchumi pamoja na nchi hiyo kunaendana na maslahi halisi ya nchi za kiarabu. Kutokana na kuimarishwa kwa uhusiano huo, kunaweza kuimarisha hadhi na umuhimu wa Misri katika sehemu hiyo; Pakistan ikiimarisha uhusiano kati yake na Israel inaweza kuimarisha uhusiano wa kimkakati na Marekani ambayo ni mwenzi wa Israel na kupunguza lawama kali dhidi yake kutokana na kuimarisha uhusiano kati ya India na Israel katika miaka ya karibuni.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-06