Waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya Kusini Bwana Ban Ki-Moon tarehe 7 huko Seoul alisema kuwa, serikali ya nchi yake itashiriki kwenye mkutano wa kipindi cha pili wa mazungumzo ya duru la nne ya pande sita, kwa msingi wa matokeo ya majadiliano kati yake na pande husika nyingine. Vyombo vya habari vinaona kuwa, ingawa tarehe halisi ya kufanya mkutano wa kipindi cha pili bado haijathibitishwa, lakini pande mbalimbali zote zimefanya maandalizi ya kurejeshwa kwa mazungumzo hayo wiki ijayo.
Mazungumzo ya duru la nne ya pande sita yalifanyika mjini Beijing kuanzia tarehe 26 Julai, na kutangazwa kusimamishwa tarehe 7 Agosti. Mazungumzo hayo yanalenga kuifanya Peninsula ya Korea isiwe na silaha za nyuklia. Kwenye mazungumzo hayo, pande husika zilifikia makubaliano mengi, lakini zilishindwa kutoa waraka wa pamoja kuhusu mazungumzo hayo. Sababu muhimu ni kwamba, pande husika bado zina tofauti kubwa kuhusu kama Korea ya Kaskazini ina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani,
Katika muda huo baada ya kusimamishwa kwa mazungumzo, pande mbalimbali husika zimefanya juhudi kubwa za kidiplomasia, ili kutafuta utatuzi wa suala la nyuklia la Peninsula ya Korea. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Bwana Sean Mccormack alisema baada ya Korea ya Kaskazini na Marekani kukutana mara ya tatu kuwa, hali ya mkutano huo ulionesha matakwa ya pande hizo mbili ya kutaka kushirikiana katika kusukuma mbele mazungumzo ya pande sita.
Habari zinasema kuwa, Korea ya Kaskazini na Marekani bado hazijalegeza misimamo yao. Korea ya Kaskazini inashikilia kuwa, ina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani, na kushikilia ombi lake la kurejesha ujenzi wa kinu cha maji mepesi cha Shinpo ikidai kuwa, kama ombi hilo halitakubaliwa, basi itaendelea kuendesha kinu cha kaboni nyeusi (graphite) cha Yongbyon kwa ajili ya kuondoa upungufu wa umeme nchini humo. Lakini Marekani inashikilia kuwa, Korea ya Kaskazini inapaswa kuacha mpango wowote wa nyuklia.
Kwa kuwa suala la nyuklia la peninsula ya Korea ni la kutatanisha, hivyo pande husika zinakataa kufanya makadirio ya mustakabali wa mkutano wa kipindi cha pili, lakini zote zimeeleza kujitahidi kusukuma mbele mazungumzo hayo. Bw. Mccormack wa Marekani tarehe 29 Agosti alisema kuwa, Marekani itachukua msimamo wenye ujenzi katika mazungumzo ya pande sita. Aliongeza kuwa, mazungumzo hayo yatajadili hasa suala la nyuklia, wala siyo suala la haki za binadamu la nchini Korea ya Kaskazini. Na Korea ya Kusini pia ilieleza kuwa, itajitahidi kadiri iwezavyo kuhimiza mazungumzo hayo yapate maendeleo halisi na kusaini waraka wa pamoja.
Gazeti la serikali la Korea ya Kaskazini tarehe 6 lilitoa makala ya mhariri ikisema kuwa, nchi hiyo kamwe haitaacha haki yake ya kutumia nishati ya nyuklia kwa njia ya amani. Marekani ikijaribu kuishurutisha nchi hiyo kwa nguvu, si kama tu haitaweza kusukuma mbele mazungumzo hayo, bali itaongeza utata wa suala hilo. Makala nyingine ya mhariri ilisema kuwa, ili kutatua suala la nyuklia, Marekani inapaswa kufanya uamuzi wa kubadilisha mfumo wake wa kusimamisha vita kuwa mfumo wa amani. Ilisema kuwa, vitendo vya Marekani na Korea ya Kusini kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi, na Marekani kumteua mjumbe anayeshughulikia suala la haki za binadamu la Korea ya Kaskazini, vitaleta athari mbaya kwa mazungumzo ya pande sita.
Lakini vyombo vya habari vinaona kuwa, pande husika zote zinachukulia kuwa, kufanya mazungumzo ya pande sita ni njia nzuri kabisa ya kutatua suala la nyuklia la peninsula ya Korea kwa njia ya amani.
2005-09-08 Idhaa ya Kiswahili
|