Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-08 21:14:23    
Mfuko wa kuhimiza maendeleo ya Tibet

cri

Katika mkoa unaojiendesha wa Tibet ulioko kwenye uwanda wa juu kabisa duniani, kutokana na kuwa kwenye mwinuko mrefu kutoka usawa wa bahari, kuna upungufu wa oxygen, na miale mikali ya jua, wakulima na wafugaji wengi wanaugua magonjwa ya macho, hasa aina ya mtoto wa jicho. Magonjwa hayo yameathiri vibaya maisha na uzalishaji mali wa wakazi wa huko. Tokea mwaka 1993 hadi leo, mradi wa kufufua uwezo wa kuona tena ulioanzishwa na mfuko wa kuhimiza maendeleo ya Tibet umewanufaisha wagonjwa elfu 20.

Jengo la mfuko wa kuhimiza maendeleo ya Tibet liko katika upande wa magharibi wa kasri ya Potala mjini Lahsa, naibu katibu mkuu wa mfuko huo Bwana Ngapo Jigyuan alisema:

"Mfuko huo ulianzishwa mwezi Aprili mwaka 1987. Waanzilishi wa mfuko huo ni Bangcang wa 10 na Bwana Ngapo Awanjinmei, ambaye ni naibu mwenyekiti wa baraza la mashauriano ya kisiasa la China."

Bw. Ngapo Jigyuan alisema kuwa, lengo la kuanzisha mfuko huo ni kushughulikia kujenga jamii yenye maelewano mkoani Tibet, na kuinua kiwango cha maisha cha wakazi wa Tibet ikishirikiana na serikali kuu. Mfuko huo umechangisha Yuan milioni 200, ambazo zimetumika katika kuanzisha miradi zaidi ya 640 katika maeneo mbalimbali ya elimu na utamaduni, afya, kuondokana na umaskini na kuwasaidia wakazi waliokumbwa na maafa, sayansi na teknolojia, uchumi na hifadhi ya asili.

Mradi wa kufufua uwezo wa kuona tena ni mradi unaoendelea kwa kipindi kirefu zaidi, kupata ufanisi mzuri zaidi na unaokaribishwa zaidi mkoani humo. Katika miaka kadhaa ya mwanzoni, kikundi cha matibabu kiliundwa hasa na madaktari kutoka nchi za nje. Bwana Ngapo jigyuan anasema:

"Tokea mwaka 1996 hadi 1997, tuliwaandaa madaktari wenyeji wa ugonjwa wa macho katika mchakato wa kutekeleza mradi huo, sasa madaktari hao wenyeji wameweza kufanya upasuaji pekee yao."

Ili kuwaandaa madaktari wa kienyeji wa ugonjwa wa macho, mfuko wa kuhimiza maendeleo ya Tibet umefanya semina kadhaa za kuwaandaa madaktari wenyeji ukishirikiana na mashirika ya kirafiki au mifuko ya nchi za nje, na hospitali mbalimbali za ugonjwa wa macho nchini China. Kwa ujumla mfuko wa kuhimiza maendeleo ya Tibet umetumia Yuan milioni 85 katika mradi huo, na kuwatibu wagonjwa elfu 20 hivi.

Bwana Ngapo Jigyuan alifahamisha kuwa, mradi mwingine mkubwa uliosaidiwa na mfuko huo unahusu elimu na hifadhi ya mabaki ya kihistoria, ambao umeanzisha au kupanua shule za msingi na sekondari zaidi ya 200, kwenye maeneo ya wakulima na wafugaji wa Tibet, na kufanya ukarabati na kuhifadhi mabaki zaidi ya 20 ya kihistoria. Tokea mwaka 2000, mradi huo umewasaidia wanafunzi zaidi ya 100 wenye matatizo ya kiuchumi kumaliza masomo yao ya shule za msingi, sekondari na chuo kikuu.

Katika miaka ya karibuni, mfuko huo umejenga shule nyingi za chekechea, nyumba za kuwatunza watoto, kujenga barabara, na kushiriki katika shughuli za uokoaji kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa ya kimaumbile na kadhalika.

Bw. Ngapo Jigyuan alisema kuwa, mfuko wa kuhimiza maendeleo ya Tibet si kama tu unachangisha fedha nchini China, pia umeyashirikisha mashirika ya kirafiki duniani . Anasema:

"Lakini mfuko huo siku zote unashikilia kanuni moja, yaani misaada yote haitakuwa na masharti yoyote, ni misaada inayotolewa bure. Katika miaka ya karibuni, mfuko huo umeanzisha uhusiano wa kuaminiana na mashirika mengi ya kirafiki na watu binafsi duniani, miradi ya misaada imepata mafanikio mazuri."

Kati ya mifuko ya kirafiki duniani, mfuko wa Misereor wa Ujerumani umetoa misaada mingi zaidi, umesaidia kuboresha hali ya kuishi ya nyumba nyingi maalum za kuwatunza wazee, kujenga shule moja ya msingi katika sehemu ya Ali, na kutoa Yuan za RMB milioni tatu kusaidia sehemu ya Ali iliyokumbwa na maafa ya theluji.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-08