Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-12 15:29:02    
Jeshi la Israel laanza kuondoka kutoka sehemu ya Gaza

cri

Jeshi la ulinzi la Israel tarehe 11 alasiri lilifanya shughuli ya kuaga na kushusha bendera ya taifa katika makao makuu yake yaliyoko karibu na makazi ya zamani ya Wayahudi katika sehemu ya Gaza. Jambo hilo lilitangaza kuwa ukaliaji wa kijeshi wa Israel katika sehemu ya Gaza kwa miaka 38 iliyopita kimsingi umemalizika.

Baada ya tarehe 23 mwezi uliopita, Israel ilipomaliza kimsingi shughuli za kuondoa makazi yaliyoko katika Gaza na baadhi ya makazi katika sehemu ya kaskazini ya kando ya magharibi ya mto Jordan, ilianza kuondoa askari wake. Tarehe 11 asubuhi, mawaziri wote wa baraza la mawaziri la Israel walipiga kura na kwa kauli moja waliidhinisha jeshi la ulinzi la Israel kuondoka kutoka sehemu ya Gaza. Saa kumi na mbili jioni, jeshi la Israel lilifanya shughuli ya kuaga katika makao yake makuu yaliyoko karibu na Neveh Dekalim, makazi makubwa kabisa ya Wayahudi yaliyoko kwenye sehemu ya Gaza. Mkuu wa sehemu ya kijeshi ya kusini mwa Israel Bw. Dan Harel alisema kwenye shughuli hiyo kuwa, kuwepo kwa jeshi la Israel katika sehemu ya Gaza kwa miaka 38 iliyopita kutamalizika na kuondoka kwa jeshi la hilokutaleta nafasi mpya kwa amani kati ya Israel na Palestina.

Kwa mujibu wa mpango, askari 3000 wa jeshi la Israel walianza kuondoka kutoka Gaza tarehe 11 usiku na kukamilisha shughuli za kuondoka saa mbili asubuhi ya tarehe 12. Kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Misri na Israel, tarehe 10 askari 200 wa Misri walianza kupangwa kwenye upande wa Misri wa mpaka kati ya Gaza na Misri. Hadi tarehe 15, askari 750 wote watapangwa kwenye sehemu hiyo. Jukumu la askari wa Misri ni kuzuia biashara ya silaha kwa njia ya magendo kwenye sehemu ya Gaza.

Jeshi la Israel lilipoondoka kutoka Gaza, jambo lisilowafurahisha watu lilitokea. Baraza la mawaziri la Israel tarehe 11 lilibadili mpango wa awali na kuamua kubakiza masinagogi zaidi ya 20 yaliyoko Gaza kabla ya kuondoka kwa askari wote wa Israel. Waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Shaul Mofaz alieleza kuwa, kubomboa masinagogi kutadhuru hisia ya imani ya Wayahudi, kwa hiyo alishindwa kuamuru jeshi lake kubomoa masinagogi hayo. Mshauri wa usalama wa taifa wa Palestina Bw. Jibria Rajoub siku hiyo alipohojiwa na radio ya Israel alieleza kuwa masinagogi hayo ni alama ya ukaliaji wa Israel, na Israel inapaswa kuwajibika kuyabomoa, na sio kuwaachia suala hilo gumu Wapalestina.

Zaidi ya hayo, bado kuna tofauti kati ya Palestina na Israel katika mamlaka ya udhibiti wa vituo vya ukaguzi, bandari na uwanja wa ndege ulioko Gaza. Kutokana na usalama, Israel bado itadhibiti milango kutoka sehemu ya Gaza baada ya kukamilisha shughuli za kuondoka, na Palestina ina wasiwasi kuwa Gaza itabadilika kuwa gereza kubwa.

Ili kuonesha malalamiko yake, Palestina ilikataa kushiriki kwenye shughuli ya kupokezana sehemu ya Gaza iliyopangwa kufanyika tarehe 11 alasiri, na kulazimisha shughuli hiyo ifutwe.

Wakati jeshi la Israel lilipoondoka, Wapalestina elfu kadhaa walikusanyika kwa furaha kwenye kando ya magofu ya makazi ya Wayahudi na kuwa tayari kuingia kwenye sehemu hiyo baada ya kuondoka kwa jeshi la Israel. Jeshi la Israel lilipofanya shughuli ya kuaga, askari wa Israel walipambana na Wapalestina ambao wanne wa Palestina walijeruhiwa. Kamanda wa Israel alieleza kuwa jeshi la Israel lilikuwa linafanya mashauriano na Palestina, ili kuhakikisha shughuli za kuondoka zinafanyika bila vikwazo.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-12