Mkuu wa tume ya uchunguzi wa kimataifa wa kesi kuhusu kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Al-Hariri Bw. Detlev Mehlis alifanya mazungumzo na mshauri wa sheria wa wizara ya mambo ya nje ya Lebanon Bw. Riad Daoudi tarehe 12 mjini Damascus Syria. Pande mbili zilifikia makubaliano kuhusu ratiba na mpango wa tume hiyo kusikiliza ushahidi kutoka kwa watu husika wa Syria. Hayo ni maendeleo halisi aliyoyapata Mehlis kwa mara ya kwanza katika ushirikiano na Syria kwenye suala la uchunguzi wa tukio hilo, ambayo pia ni kurudi nyuma tena kulikofanywa na Syria chini ya shinikizo la nchi za magharibi ikiwemo Marekani.
Detlev Mehlis aliyelindwa na askari wengi alipanda gari na kufika Damascus kutoka Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Baada ya kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano na Riad Daoudi, Mehlis alirudi mjini Beirut alasiri ya siku hiyo. Mwisho wa wiki ijayo, Mehlis ataitembelea tena Syria.
Habari zinasema kuwa Mehlis atawahoji maofisa wa Syria wasiopungua wanane, wakiwemo mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi ya Syria Bw. Rustom Ghazaleh na wasaidizi wake wawili. Kabla ya hapo, Mehlis alieleza kuwa bado hajathibitisha mtuhumiwa yeyote wa Syria na maofisa wa Syria watahojiwa wakiwa mashahidi. Lakini alieleza pia, mbali na maofisa wanne wa zamani wa idara ya usalama ya Syria waliokamatwa, watu wengi zaidi wanahusika na tukio hilo.
Tarehe mosi mwezi huu, mjini Beirut Mehlis aliishutumu Syria kutotoa ushirikiano kwa tume hiyo, na kusababisha maendeleo polepole ya kazi ya uchunguzi. Kutokana na kukabiliwa na shinikizo la jumuiya ya kimataifa, serikali ya Syria imekubali kumwalika Mehlis aende Syria kufanya uchunguzi.
Wachambuzi wanaona kuwa kuitembelea Syria kwa Mehlis kwa mara ya kwanza, sio tu ni maendeleo makubwa kuhusu uchunguzi wa kimataifa wa tukio la kuuawa kwa Bw Hariri, bali pia ni kurudi nyuma kulikofanywa na Syria chini ya shinikizo la jumuiya ya kimataifa.
Syria siku zote inakabiliana na shinikizo kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa katika tukio la kuuawa kwa Hariri. Hadharani inaonesha kuwa Marekani na nchi za magharibi zilifanya hivyo kwa uhuru wa Lebanon, lakini katika mambo halisi inaonesha kuwa ni mapambano kati ya Syria na Marekani katika mambo ya kikanda. Syria imechukua msimamo mkali wa kuzipinga Marekani na Israel katika suala la amani ya Mashariki ya kati. Marekani siku zote imeishutumu Syria kuunga mkono watu wenye msimamo mkali wa Palestina na kuwaruhusu watu hao waingie nchini Iraq kwa kupitia mpaka kati ya Syria na Iraq. Tena Marekani ilizusha uvumi mbalimbali kuhusu tukio la kuuawa kwa Hariri, ili kuilazimisha Syria ibadilishe msimamo wake. Syria haina uwezo wa kupambana na Marekani na Ufaransa, na haina budi kurudi nyuma tena na tena katika msingi wa kulinda heshima ya taifa. Kadiri uchunguzi wa kesi ya Hariri unavyoendelea, ndivyo maendeleo ya siku za usoni ya uhusiano kati ya Syria na nchi za magharibi yatafuatiliwa.
Idhaa ya kiswahili 2005-09-13
|