Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-13 15:21:15    
Tatizo la biashara ya nguo kati ya China na Ulaya latatuliwa kwa utulivu

cri

Tarehe 5 usiku wakati waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilei na mjumbe wa kamati ya biashara ya Umoja wa Ulaya Bw. Peter Mandelson walipotia saini kwenye kumbukumbu ya mazungumzo, sauti kubwa ya makofi ilisikika kwenye ukumbi wa wageni maarufu wa Hoteli ya Beijing. Washiriki waliokuwa ukumbini walifahamu kuwa mgogoro wa bidhaa za nguo kutokana na bidhaa za nguo zilizorundikana katika forodha za ulaya umetatuliwa. Hii ni hali inayonufaisha pande zote mbili.

Tokea mwaka huu uanze suala la nguo lilikuwa ni suala linalofuatiliwa sana katika uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Ulaya. Utaratibu wa biashara ya nguo usio na mgao ulianza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka huu kati ya nchi wanachama wa shirika la biashara duniani, lakini kutokana na kuinuka kwa nguvu inayotetea kuweka vizuizi vya kibishara ndani ya Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya ulidhibiti usafirishaji wa bidhaa za nguo za China kwa kisingizio cha ongezeko kubwa la bidhaa za nguo zilizosafirishwa kwa Ulaya kutoka China, hatua ambayo ilisababisha bidhaa za nguo zaidi ya milioni 80 kukwama katika bandari mbalimbali za nchi za Ulaya.

Vizuizi vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya bidhaa za nguo za China vilileta mashaka ndani ya umoja huo. Kiongozi wa jumuiya ya biashara ya Uingereza na China Bw. Peter Nightingale alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema,

"Kwa kufuata hali halisi ya utandawazi wa uchumi, ni vigumu kudumisha kwa muda mrefu sera za kuweka vizuizi vya biashara. Kwani ukifanya hivyo utadidimia katika vizuizi vya utaratibu wa uchumi. Sera za kuweka vikwazo vya biashara zimepitwa na wakati na haziwezi kuleta manufaa kwa watu wote katika utandawazi wa uchumi."

Bw. Nightingale alisema kuwa hali ya hivi sasa ya kufanya pande zote mbili kupata hasara inayosababishwa na kuwekwa kwa vikwazo vya biashara ndani ya Umoja wa Ulaya.

Habari zinasema kuwa kurundikana kwa wingi kwa bidhaa nyingi za nguo kutoka China katika bandari za nchi za Umoja wa Ulaya kumeleta hasara kubwa kwa wafanyabiashara wa rejareja wa Umoja wa Ulaya. Gazeti la Financial Times la Uingereza lilisema kuwa kwa bidhaa za sweta za sufu peke yake, wafanyabiashara wa rejareja wa nchi za Umoja wa Ulaya waliingia hasara ya Euro zaidi ya milioni 800.

Jambo lililo muhimu zaidi ni kuwa wafanyabiashara wa rejareja wa Umoja wa Ulaya hivi karibuni watakuwa na ununuzi mkubwa muhimu kwa siku kuu ya Krismas, wafanyabiashara wa nguo wa maduka yaliyoko katika sehemu za katikati ya miji ya Uingereza walinung'unika kuwa, endapo tatizo la kurundikana kwa bidhaa za nguo kutoka China halitaweza kutatuliwa kwa haraka, watakabiliwa na upungufu wa bidhaa za nguo katika wiki chache zijazo.

Meneja wa duka moja la mavazi ya ndani nchini Uingereza Bibi Mary Ailen alinung'unika kuwa, sidiria zilizouzwa katika duka lake zilitengenezwa nchini China, na anashindwa kupata viwanda vinavyofaa kwa uzalishaji wa bidhaa hizo katika nchi nyingine katika muda mfupi. Alisema,

"Ninaona kuwa mtu aliyeamua mgao wa bidhaa za nguo anatakiwa kushauriana na watu wa sekta husika na kuwauliza watu wanaohusika moja kwa moja wa sekta ya nguo. Ni dhahiri kuwa Mandelson hana uzoefu katika biashara ya rejareja ya nguo, hususan mauzo ya sidiria. Hakufahamu kuwa ushonaji wa sidiria ni kazi kubwa na hajui muda gani unaohitajiwa kutoka usanifu hadi kukamilisha ushonaji wake."

Aidha, kutokana na kupungua kwa bidhaa, bei ya nguo katika masoko ya nchi za Umoja wa Ulaya inakabiliwa na shinikizo la kupanda kwa bei. Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zina wasiwasi kuwa mabadiliko ya bei za nguo yataleta athari mbaya kwa uchumi wa nchi zao.

Kutokana na kushindwa kusafirisha bidhaa kwa nchi za Umoja wa Ulaya, viwanda vya nguo vya China pia vimeingia hasara kubwa. Bw. Zhu Wenxi ni naibu meneja mkuu wa kampuni ya sweta ya Xuelian mjini Beijing, alikabidhiwa jukumu la kushughulikia usafirishaji bidhaa kwa nchi za nje. Bidhaa za sweta zinazozalishwa katika kampuni yao zinasafirishwa kwa nchi na sehemu zaidi ya 30 zikiwemo za Umoja wa Ulaya. Hivi karibuni baadhi ya wafanyabiashara kutoka Italia walisema kuwa wanataka kuagiza bidhaa za kampuni hiyo, lakini walishindwa kufanikisha biashara ya nguo kutokana na kushindwa kupata mgao. Bw. Zhu Wenxi alisema,

"Kwa mfano, wafanyabiashara kutoka Italia na Ujerumani walifika kwenye kampuni yetu kuangalia sampuli. Lakini kutokana na mkwaruzano wa biashara kati ya China na Umoja wa Ulaya katika sekta ya nguo, shughuli zetu za kusafirisha bidhaa za nguo kwa nchi za nje zimeathiriwa. Hivi sasa tumelazimika kuacha kwa muda masoko ya nchi za Umoja wa Ulaya.

Kutokana na kukabiliwa na shinikizo kutoka kwa wafanyabiashara wa rejereja na wateja wa Umoja wa Ulaya ambao wanataka suala la kurundikana kwa bidhaa za nguo kutoka China litatuliwe haraka iwezekanavyo, maofisa wa Umoja wa Ulaya waliwasili Beijing mwishoni mwa mwezi Julai ili kujadili suala hilo na maofisa wa wizara ya biashara ya China. Lakini mazungumzo ya duru la kwanza hayakupata mafanikio kutokana na pande hizo mbili kushindwa kufikia makubaliano kuhusu mgao wa bidhaa za nguo zilizorundikana katika forodha za Umoja wa Ulaya.

Kutokana na shinikizo kubwa linaloukabili Umoja wa Ulaya, mjumbe wa kamati ya biashara wa umoja huo Bw. Mandelson alilazimika kuja Beijing yeye mwenyewe tarehe 4 akitaka kufanikisha makubaliano hayo kwa kutumia nafasi ya kufanyika hivi karibuni mkutano wa viongozi wa nchi za China na Umoja wa Ulaya. Baada ya kufanya mazungumzo ya saa zaidi ya 10 katika siku mbili, hatimaye pande mbili za China na Umoja wa Ulaya zilikubaliana kuhusu suala la bidhaa za nguo za China zilizozuiliwa katika bandari za nchi za Umoja wa Ulaya. Kutokana na maagizo ya mapatano ya mazungumzo, Umoja wa Ulaya utapitisha nguzo zote zilizozuiliwa katika bandari za nchi za umoja huo, Umoja wa Ulaya utaruhusu nguo zaidi ya milioni 80 zilizozuiliwa katika bandari mbalimbali za nchi za umoja huo. Utatuzi kamili ni nusu ya nguo hizo zinahesabiwa ni ongezeko la mgao wa mwaka huu na nusu nyingine itakatwa kutoka katika mgao wa mwaka ujao au kukatwa kutoka katika mgao wa bidhaa nyingine za nguo.

Baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai na mjumbe wa kamati ya biashara ya Umoja wa Ulaya Bw. Mandelson walifanya mkutano pamoja na waandishi wa habari. Bw. Bi Xilai alisema kuwa makubaliano hayo yalifanikishwa kutokana na wazo la ushirikiano wa kunufaisha pande zote mbili, aliongeza kuwa kuhusu nguo zilizokwama kwenye bandari, tumechukua hatua ya kubeba mzigo kwa usawa yaani kila upande unabeba jukumu linaloukabili. Mazungumzo hayo yanaendana na kanuni za haki na usawa si katika kanuni kubwa tu, bali pia katika vipengele vidogo vidogo. Uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Ulaya ni wenye uhamasa.

Bw. Mandelson alisema kuwa ingawa pande mbili za China na Ulaya zilikutwa na baadhi ya shida za muda, tena mazungumzo yalikuwa magumu, lakini haiwezekani kulipuka "vita ya biashara" kati ya China na Umoja wa Ulaya. China ni nchi kubwa ya biashara inayoendelea kwa mfululizo, hali ya kunufaishana ya uchumi wa pande hizo mbili imeamua kuwa ushirikiano wa pande hizo mbili una uwezo mkubwa ambao bado haujatumika.

Bw. Mandelson alisema kuwa mapatano hayo yanatarajia kupitishwa na nchi 25 za wanachama, na matokeo yake yatafahamika katika siku chache zijazo. Baada ya mapatano hayo kuidhinishwa, nguo zilizokwama kwenye bandari za nchi za Umoja wa Ulaya zitaingia kwenye masoko ya nchi hizo kuanzia katikati ya mwezi Septemba.

Viwanda vya nguo vya China na wafanyabiashara wa Umoja wa Ulaya wote wamefurahishwa na matokeo hayo.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-13